50 wathibitishwa kufa, maelfu wajeruhiwa kimbunga Chido kikitesa pwani ya Afrika mashariki – Taifa Leo


IDADI rasmi ya watu ambao wamefariki kutokana na kimbunga Chido imefika 53 baada ya vifo vingine kuripotiwa nchini Msumbiji na Zambia, kwa mujibu wa ripoti za mamlaka Jumanne.

Hata hivyo, inahofiwa kuwa idadi hiyo inaweza kutinga maelfu katika kisiwa Mayotte cha Ufaransa kwani ndicho kilikuwa kitovu cha kimbunga hicho kilichotua Jumapili katika pwani ya mashariki mwa Afrika kwenye Bahari Hindi.

Nchini Msumbiji watu 34 waliropitiwa kufariki Chido ilipotua Jumapili, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu (OCHA) iliyotolewa Jumanne. OCHA ilinukuu takwimu kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Kushughulikia Majanga (INGD) ya nchi hiyo.

“Kufikia Desemba 17, 2024 inakisiwa watu 174,158 waliathirika – 34 wamefariki na 319 kujeruhiwa,” OCHA ilisema kwenye taarifa yake.

Uharibifu uliosababishwa na kimbunga Chido katika wilaya ya Mecufi mkoani Cabo Delgado, Msumbiji, mnamo Desemba 16, 2024. PICHA | REUTERS

Kimbunga hicho kilitua eneo la pwani la Cabo Delgado kabla kuchomoza bara hadi Niassa na Nampula, ambako msichana mdogo wa miaka mitatu alikuwa miongoni mwa waliofariki.

Wengi wa waliouawa walipigwa na vitu vilivyokuwa vikiporomoka kama vile kuta za mawe, msemaji wa INGD, Paulo Tomas, aliongeza.

Katika kisiwa cha Mayotte idadi rasmi ya vifo ilifika 22 Jumanne, japo inahofiwa mamia na hata maelfu ya watu yawezekana wamefariki kwani sehemu nyingi bado hazifikiki na baadhi ya miili kuzikwa kabla zoezi rasmi la kuhesabu wafu kufanyika.

Kisiwa hicho kidogo – kilicho chini ya usimamizi wa Ufaransa na maskini zaidi kati ya himaya zake za ng’ambo – kilishuhudia maafa makubwa zaidi kutoka kwa kimbunga Chido kabla pepo hizo kali haribifu za mvua kuteremka chini Msumbiji na Zambia.

Maafisa walikuwa mbioni kukabiliana na njaa, maradhi na utovu wa usalama ili zisienee kisiwani humo kufuatia maafa yaliyoshuhudiwa.

Watoto wakipita karibu na nyumba zilizoharibiwa na kimbunga Chido katika eneo lingine la Mecufi mkoani Cabo Delgado, Msumbiji. PICHA | REUTERS

Njaa, giza, maradhi na uhalifu

Pamoja na idadi rasmi ya vifo pia watu zaidi ya 1,400 walithibitishwa kujeruhiwa, alisema Meya Ambdilwahedou Soumaila wa jiji kuu Mamoudzou katika mahojiano na kituo cha redio cha Radio France Internationale, Jumanne asubuhi. Isitoshe watu 34,000 nchini humo sasa hawana makao.

“Cha muhimu ni maji na chakula. Kwa bahati mbaya kuna watu wameaga dunia na miili yao imeanza kuoza na hivyo kusababisha tatizo la kiafya na usafi,” Soumaila alisema.

Akaongeza: “Pia hatuna umeme. Usiku unapowadia kuna watu wanatumia fursa hiyo kutenda uhalifu.”

Video zilizonaswa na droni zilionyesha paa za nyumba zimeangushwa karibu na bichi, miti michache pekee ya mnazi ikisalia japo imejikunja, na mali za watu zikitapakaa katika mkoa wa Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Madaktari wakimhudumia mmoja wa majeruhi katika uwanja wa ndege wa Dzaoudzi–Pamandzi mnamo Desemba 17, 2024, katika eneo la Pamandzi kisiwani Mayotte. PICHA | REUTERS

Katika kisiwa cha Mayotte kitovu cha kimbunga, video moja iliyonaswa kutoka angani ilionyesha mabaki ya nyumba zilizoharibika yakiwa yametapakaa kote. Maboti ya polisi yaliyoharibiwa yalikuwa ufuoni huku miti ya minazi ikiwa imeanguka kwenye paa za majengo.

Kisiwa hicho kinapatikana katika Bahari Hindi kati ya mataifa ya visiwa ya Madagascar na Msumbiji.

Ni himaya inayosimamiwa na Ufaransa ingawa utamaduni wake asilia unawiana zaidi na ule wa watu wa kisiwa cha Comoros.

Kimbunga Chido kilipiga Mayotte saa za usiku, lilisema shirika la utabiri wa hali ya hewa la Meteo-France huku upepo wa kasi ya kilomita 200 kwa saa ukiharibu nyumba, majengo na hospitali..

Ni kimbunga kikali zaidi kuwahi kushuhudiwa kisiwani humo katika kipindi cha zaidi ya miaka 90, shirika hilo liliongeza.

Imeandaliwa na CECIL ODONGO



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*