MWENYEKITI mpya wa bodi ya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) Bw Ndiritu Muriithi anataka makubaliano rasmi ya muungano kati ya Rais William Ruto, kinara wa upinzani Raila Odinga na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Bw Ndiritu (pichani) , ambaye aliapishwa Jumatatu, anasema makubaliano hayo yatasaidia kuwa na njia moja ya sera za kupanga utawala wa Kenya Kwanza na muungano wa Azimio la Umoja, kuimarisha umoja na amani nchini na kuchangia pakubwa katika kuleta maendeleo kwa Wakenya.
Licha ya kujiunga na serikali ya Rais Ruto kupitia washirika wake ambao ‘alichanga’ kwa Kenya Kwanza, Waziri Mkuu wa zamani Odinga ameshikilia kuwa chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM) bado kilikuwa katika upinzani, na kuibua shutuma kali.
Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua amemkashifu Bw Odinga kwa kuwasaliti Wakenya kwa kujiunga na Dkt Ruto badala ya kusalia upinzani ili kuipiga darubini serikali.
Baada ya maandamano yaliyotikisa nchi mwezi Juni dhidi ya Mswada wa Fedha wa 2024, Rais Ruto alilazimika kutupilia mbali sheria hiyo na kutimua baraza lake lote la mawaziri.
Aliwateua washirika wa Bw Odinga serikalini katika kile alichokitaja kama Serikali Jumuishi.Wiki mbili zilizopita, Dkt Ruto aliwataja washirika wa zamani wa Rais Uhuru Kenyatta kuchukua nyadhifa za baraza la mawaziri, wakuu wa mashirika ya umma na mabalozi katika utawala wake.
Jumapili iliyopita, Rais alisema ataifanya serikali yake kuwa pana zaidi mwaka wa 2025 ili iwe ‘jumuishi’ zaidi kwa lengo la kuwahudumia Wakenya vyema.Sasa, Bw Muriithi, ambaye alikuwa mshirika wa Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, anasema ili manufaa kamili ya umoja huo yatimizwe, makubaliano rasmi ya muungano ni muhimu.
“Inapaswa kuwa ilifanyika jana. Tunapoingia katika Mwaka Mpya mpya, makubaliano rasmi yatatoa mfumo wa sera uliooanishwa ili kuwaongoza wataalam kutoka pande zote mbili kuelekea lengo moja. Muungano kama huo utarahisisha kazi kwani utaruhusu Azimio na UDA kuwa na matokeo mahususi ambayo tunajaribu kufikia kwa manufaa ya Wakenya,” Bw Muriithi aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano.
Alionya kuwa kukosekana kwa mkataba kunaweza kuhatarisha sera huku maamuzi ambayo hayawiani yakifanywa, na akawataka Rais Ruto, Bw Odinga, rais wa zamani Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wakuu katika miungano hiyo miwili kusonga mbele kwa kasi na kurasimisha ndoa hiyo
.Alisisitiza kuwa licha ya Azimio kuporomoka kufuatia nia ya baadhi ya vyama vya kisiasa kujiondoa katika muungano huo, vyama vilivyosalia bado vinaweza kusonga mbele.
“Ninaamini kuwa umoja huu ni kwa manufaa ya Wakenya. Ukiangalia mwanzo wa serikali Jumuishi, unagundua kuwa ulikuja kufuatia maandamano ya Wakenya wasioridhika. Maandamano na uasi wa Juni 2024 ulihusu uchumi na tuna deni kwa raia ambalo tunapaswa kulipa kwa kutimiza matarajio yao,” Bw Muriithi alisema.
Gavana huyo wa pili wa Laikipia anasema atapendekeza hatua kadhaa ambazo anaamini zitageuza uchumi. “Jambo la kwanza kati yao ni kupanua wigo wa ukusanyaji ushuru ambapo ‘sio watu wachache kulipa ushuru kwa kutozwa zaidi bali kupata watu wengi zaidi kulipa,” anasema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply