KUNA uwezekano mkubwa kwamba iwapo joto la kisiasa lilishuhudiwa mwaka jana litaendelea mwaka huu, sekta muhimu zitaathiriwa na kuweka nchi katika mustakabali mbaya.
Mbali na joto la kisiasa, baadhi ya sera za serikali zilizopingwa na raia zikiendelea, itakuwa balaa kwa nchi kwa kuwa zitaendelea kufanya maisha ya Wakenya kuwa magumu zaidi.
Wale watakaoumia ni raia wa kawaida ambao sera za serikali ya Kenya Kwanza kwa miaka miwili ambayo imekuwa mamlakani zimeongeza gharama ya maisha, kufanya elimu kuwa ghali zaidi na huduma za matibabu katika hospitali za umma kutoaminika.
Zaidi ya hayo, ucheleweshaji wa mgao kwa serikali za kaunti ambazo zinapaswa kutoa huduma mashinani umekuwa na athari hasi kwa raia ingawa serikali haitaki kukubali.
Iwapo joto la siasa lililoibuka baada ya kutimuliwa ofisini kwa Rigathi Gachagua kama naibu rais, lawama zilizoibuka kutokana na muundo wa ufadhili wa vyuo vikuu na matatizo yaliyokumba sekta ya afya kutokana na kuanzishwa kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii litazidi huku raia wakilia njaa kutokana na ushuru wanaobebeshwa na serikali, hali itakuwa mbaya zaidi. Itakuwa sawa na kuongezea mafuta katika moto.
Bila kudaganyana, dalili zote zinaonyesha kuwa joto hili litapanda iwapo utawala wa sasa hautabadilishwa mwelekeo na kuwasikiliza raia zaidi kabla ya kuanzisha mpango na mradi unaowaathiri moja kwa moja.
Masaibu ya serikali katika miaka miwili ambayo imekuwa mamlakani yalitokana na mtindo wa kupuuza maoni ya umma na kuwalazimishia sera wanazohisi zinawakandamiza.
Dalili nyingine ya kuonyesha joto litazidi ni kuungana kwa familia za tabaka la wanasiasa hatua ambayo wengi wanahisi ni ya kuwagandamiza zaidi. Hisia za raia kufuatia hatua ya Rais William Ruto kufufua ukuruba wake na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta siku chache kabla ya mwaka jana kuisha, ni dalili nyingine kwamba joto la kisiasa litapanda.
Hii ni kuongezea hatua ya serikali ya kutumia mkono wa chuma dhidi ya wakosoaji wake kwa kuwateka nyara. Ushirikiano wa vigogo hao watatu wa kisiasa wenye ushawishi kitaifa na hasa katika maeneo wanayotoka, vitendo vya maafisa wa usalama dhidi ya raia wasio na hatia vinaonyesha mwaka huu, raia watakuwa peke yao huku tabaka la wanasiasa likiungana kulinda maslahi yao.
Katika hali kama hii, nafasi ya mwananchi wa kawaida kupata haki huwa finyu sana.
Leave a Reply