Mpenzi asema amechoshwa na uhusiano bila tendo! – Taifa Leo


Shikamoo shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa. Kwa muda wote huo hatujashiriki mapenzi na sasa analalamika akidai mapenzi bila ngono si mapenzi. Je, ni kweli?

Mpenzi wako anakuhadaa. Mapenzi yanaweza kudumu bila tendo hilo. Kuna watu wanaoshiriki mapenzi kabla ya ndoa. Lakini hatari iliyopo ni kuwa baadhi ya wanaume huonja na kutoweka. Zingatia haya katika uamuzi wako.

Adai anipenda lakini nadhani anyemelea hela

Kuna mwanamke jirani yangu ameungama kuwa ananipenda. Nimeshangaa kwa sababu hiyo si kawaida kwa wanawake. Ninafanya biashara na nadhani amevutiwa na pesa zangu.

Ingawa si kawaida kwa mwanamke kuwa wa kwanza kuomba mapenzi, inawezekana huyo anakupenda kwa dhati na amelemewa na hisia akaamua kufungua moyo. Kama wewe pia unampenda, mpe nafasi. Hatimaye utajua nia yake.

Mpenzi ananiudhi mno kupekua simu yangu!

Mpenzi wangu ameanza tabia inayonichukiza. Nisipokuwa naye hunipigia simu mfululizo akitaka kujua niko wapi na ninafanya nini. Anapenda pia kukagua simu yangu kujua walionipigia. Nifanye nini?

Hilo si jambo geni katika mapenzi. Ni wivu unaotokana na mapenzi ya dhati. Mpenzi wako anakupenda na anataka kuhakikisha kwamba wewe ni mwaminifu kwake. Akishathibitisha atatulia.

Ameamka tu ghafla na kuniambia hanipendi!

Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili. Lakini alinishangaza juzi aliponiambia hanipendi. Nilikuwa nimepanga kumuoa na uamuzi wake huo umeniumiza moyoni. Nifanye nini?

Ukweli ni bora hata kama ni mchungu. Mpenzi wako amekufungulia moyo wake. Kubali kwamba huo ndio mwisho wa uhusiano wenu na hutaweza kuishi naye kama mke wako.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*