Jinsi Matiang’i anajipanga kwa urais ‘chini ya maji’ – Taifa Leo


TAKRIBAN miezi mitano baada ya aliyekuwa waziri Dkt Fred Matiang’i kuripotiwa kuteua kampuni ya kimataifa ya Dickens & Madson yenye makao yake makuu Montreal, Canada kumsaidia kupanga mikakati ya kampeni ya urais 2027, chama cha kisiasa kinachohusishwa naye sasa kimeongeza juhudi zake za kujiimarisha.

Chama cha United Progressive Alliance (UPA), ambacho kinatumia pikipiki, rangi nyekundu, kijani na nyeupe kwa utambulisho wake, sasa kinajitahidi kuondoa nembo ya ‘chama cha kabila moja’ ambayo imekuwa ikihusishwa nacho.

Wachanganuzi wa siasa wanasema, yamkini waziri huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa wakati wa utawala wa Jubilee anaweka msingi wa kuzindua kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

“Naona anajiimarisha ili kuungana na vigogo wengine wa kisiasa kama aliyekuwa bosi wake Uhuru Kenyatta. Bila uungwaji mkono na wanasiasa wengine wenye ushawishi, kujipanga kwake ni mzaha,” akasema mchanganuzi wa siasa Tom Maosa.

Alisema ni rahisi Bw Matiang’i kupata uungwaji mkono kwa kuwa ana sifa kitaifa.

Akizungumza baada ya mkutano wa Baraza Simamizi la Kitaifa (NGC) uliofanyika Nyamira, kiongozi wa chama hicho Amos Nyaribo alieleza kuwa, NGC imeazimia kukabidhi baadhi ya nyadhifa za chama kwa watu kutoka maeneo mengine ya nchi kama mkakati wake wa upanuzi.

“Tumekutana kama NGC kujadili mipango yetu ya upanuzi. Tunajiandaa kutikisa nchi nzima. Tutakuwa tunasalimisha nyadhifa fulani za chama kwa watu binafsi kutoka kaunti zingine ili kutufanya tuwe na nguvu zaidi,” akasema Bw Nyaribo.

Upanuzi wa chama hicho pia utahusisha ufunguzi wa angalau afisi mpya 26 za chama kote nchini kufikia katikati ya 2025, alieleza Bw Nyaribo, ambaye ni gavana wa Kaunti ya Nyamira.

Mnamo Aprili 2023, Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) wa UPA ulifanyika Nairobi ambapo viongozi waanzilishi wa chama hicho walibadilishwa na watu ambao kwa kiasi kikubwa walitoka kwa jamii ya Abagusii.

Viongozi wa sasa ni Bw Nyaribo (Kiongozi wa Chama), Mbunge wa Bonchari Charles Onchoke (Naibu Kiongozi wa Chama), MCA wa Wadi ya Rigoma Nyambega Gisesa (Mwenyekiti wa Kitaifa), Damaris Nyanchoka (Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa), Naibu Spika wa Bunge la Kaunti ya Kisii Jacob Bagaka (Katibu Mkuu), Joel Ombongi (Naibu Katibu Mkuu) na Derick Mosiany (Mweka Hazina wa Kitaifa).

Wengine ni Ibrahim Isaak (Naibu Mweka Hazina), Alice Kiongo (Katibu Mratibu), William Serem (Naibu Katibu Mratibu), Julias Anyoka (Masuala ya Sheria), Edna Obara (Masuala ya Wanawake), Mildred Okero (Masuala ya Vijana) na Hellen Misati (Katibu wa Walemavu).

Elijah Abere anasimamia masuala ya bunge, Amiss Nzao (Masuala ya Kimataifa), John Asakhulu (Sera ya Umma) na Florence Achieng (Upelelezi).

Viongozi waanzilishi waliofukuzwa ofisini baada ya mzozo wa muda mrefu katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) na Mahakama ya kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa walikuwa Eliki Tom (Mwenyekiti wa Kitaifa), Martin Mutua (Naibu Mwenyekiti), Josiah Omolo (Naibu. Katibu Mkuu) na James Gichana (Mweka Hazina).

Wengine ni Enock Ombuna (Katibu Mratibu), Nixon Lugadiru (Katibu wa Walemavu), Brian Inzai, Diana Makomere, Grace Mwashigadi (Masuala ya Vijana), Sarah Mbogai, Nancy Omweri, Meshack Mwambi, Aggrey Kwamesa, Enock Onsembe, Thomas Orina, Kafadzi Charo na Vivian Cherono.

Bw Nyaribo alisema kuwa NGC iliyofanyika Nyamira pia ilihudhuriwa na wajumbe kutoka Kwale, Uasin Gishu, Kakamega, Kisumu, Wajir na Narok ambao ama ni wanachama wa NGC au Halmashauri Kuu ya Kitaifa (NEC).

“Kwa hivyo, hupaswi kusema kwamba UPA ni chama cha Gusii. Ni chama cha kitaifa,” alisema.

Katibu Mkuu Bw Bagaka, alisema Dkt Matiang’i ni mwanachama wa muda mrefu wa chama hicho na ndiye mtu pekee anayeweza kutoa uongozi mbadala ambao Wakenya wanautamani kwa sasa.

“Kama chama, hatutaki kuzungumzia mengi kuhusu 2027. Lakini ukweli ni kwamba, sisi ni chama cha kuangazia. UPA ina mgombea urais. Mwanzilishi wa chama hiki anaitwa Fred Okeng’o Matiang’i, mtu mwenye sifa ya juu. Hatimaye atakapokuja,United Democratic Alliance – UDA – kitaenda nyumbani,” alisema Bw Bagaka.

Mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema muungano wowote ambao utahusisha Matiang’i utaweza kuzoa kura za jamii ya Gusii na vijana ikiwa atadumisha ushawishi uliojitokeza wakati wa maandamano ya mwaka jana.

“Bila shaka uwaniaji wake chini ya muungano utavutia vijana akidumisha mwamko wa mwaka jana,” akasema.

Bw Bagaka alisisitiza kuwa, Wakenya wamestahimili kutozwa ushuru usio na maana chini ya UDA na kwamba ni UPA pekee ambayo ‘inaweza kubeba matarajio ya Wakenya kwa umoja’.

Hivi majuzi, Dkt Matiangi alionekana akitangamana na wafanyabiashara wa soko katika Kaunti ya Kitui.

Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kuonekana hadharani baada ya miezi mingi.

Kujitokeza kwake kulionekana kuwasisimua Wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii huku wito wa kumtaka agombee urais ukiongezeka huku akinyamaza kuhusu suala hilo.

Picha za harusi ya mwanawe baadaye zilionekana kwenye mitandao ya kijamii, huku Rais wa zamani Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka wakihudhuria.

UPA inayoongozwa na Dkt Matiang’i, Bw Bagaka aliongeza, itakumbatia utiifu wa kikatiba na kuzingatia matakwa ya ushiriki wa umma kuhusu suala lolote linaloathiri raia.

UPA ilishiriki katika uchaguzi kwa mara ya kwanza kabisa mnamo 2022, na kushinda kiti kimoja cha ugavana, mbunge mmoja na madiwani 18.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*