Mahakama yazima uteuzi wa Obodha kama Mkurugenzi Mkuu wa East Africa Portland – Taifa Leo


MAHAKAMA Kuu ya Milimani, Nairobi imetoa agizo kumzuia Bw Bruno Oguda Obodha kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya East Africa Portland Cement (EAPCC) wiki mbili baada ya kuteuliwa na Rais William Ruto.

Maagizo hayo yalitolewa na Jaji Bahati Mwamuye akisubiri kusikilizwa kwa kesi iliyowasilishwa  na mwenyehisa wa EAPCC akitaka uteuzi wa Bw Bruno na Rais Ruto ubatilishwe akisema sababu za mgongano wa kimaslahi.

“Kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi  iliyowalishwa Januari 2 2025 , (Taarifa ya Hatua ya Rais ya  20 Desemba 20 2024  agizo linatolewa kuzuia kumteua Bw Bruno Oguda kama Mkurugenzi Mkuu wa Mshtakiwa wa Pili kufuatia  notisi ya gazeti la serikali,” Jaji alisema.

Maagizo hayo ya mahakama yalitolewa siku chache baada ya bodi ya EAPCC kumwandikia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji barua ikimshauri kufikiria upya uteuzi wa Bw Obodha ikitaja masuala ya uadilifu na mgongano wa kimaslahi.

Bodi ya Kampuni ya East Africa Portland Cement (EAPCC)  ilikataa kuidhinisha uteuzi wa Bw Bruno Oguda Obodha kama Mkurugenzi Mkuu mpya na Rais Ruto mnamo Desemba 20 2024.

Katika kikao cha bodi Ijumaa katika afisi za Kampuni, bodi hiyo ilimwandikia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ikikataa uteuzi wa Bw Obodha ikitaja masuala ya uadilifu na mgongano wa kimaslahi.

Katika barua iliyoonekana na Taifa Leo na kutiwa saini na Mwenyekiti wa bodi Brig (mstaafu) Richard Mbithi, bodi ilitaja masuala kadhaa ibuka yaliyorejelewa kwenye barua iliyoandikwa Aprili 20 2022 Na.OP/CAB.9/1A na katibu wa wizara kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma aliyesema Mkurugenzi Mkuu mteule alikuwa anafanya biashara na Portland na alikuwa akijihusisha na udanganyifu.

“Ingawa EAPCC iliteua M/s Geoner Systems & Massel Real mnamo Desemba 22 2023 kama ajenti wa kuuza sehemu ya ardhi LR No.10424 ambayo inaendelea kwa sasa, imebainika Bw Bruno Obodha ni mkurugenzi wa kampuni hiyo, na huu ni mgongano wa kimaslahi,” inasema sehemu ya barua.

Iliongeza: “Ingawa EAPCC ilitoa zabuni No.EAPCCPLC/OT/340/2 23 Oktoba 23 2024 ya kutoa huduma za ulinzi, M/s Brumec International Security Company Limited iliwasilisha zabuni ambayo ilijumuisha nyaraka ghushi. Imebainishwa kuwa ,Bw Obodha ni mkurugenzi wa Kampuni.”

Bodi hiyo pia ilijiondolea lawama yoyote ikisema ilipowasilisha majina matatu kuzingatiwa, haikuwa na habari kuhusu mambo ambayo yana athari mbaya za kibiashara kwa kampuni iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE).

Mkurugenzi ambaye alizungumza na Taifa Leo kwa sharti asitajwe jina alisema kuidhinisha uteuzi wa Bw Obodha kutakuwa sawa na kuidhinisha uongo ambao na ulaghai jambo ambalo litasumbua kampuni hiyo.

“Hatupingi uamuzi wa Rais Ruto kumteua Bw Obodha lakini tunamshauri tu, hafai kwa kazi hiyo,” alisema.
Wakati wa mkutano wa bodi ya wakurugenzi uliofanyika katika afisi ya kampuni hiyo katika Taj Towers mnamo Ijumaa Novemba 22, 2024, iliandaa ripoti ikionyesha Bw Mohammed Osman Adan aliibuka mgombeaji bora kwa kupata asilimia 88.15 Bruno O Obodha aliibuka wa pili kwa kupata asilimia 64 akifuatiwa kwa karibu na Dkt Justa Mwangi aliyezoa asilimia 63.86.

Mnamo Disemba 23 wafanyikazi wa EAPCC walifunga kiwanda cha Athi River wakipinga kuteuliwa kwa Bw Obodha.
Kesi kadhaa zimewasilishwa mahakamani kupinga uteuzi huo.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*