Mipasuko yazidi katika Mlima Kenya vigogo wa kisiasa wakishambuliana – Taifa Leo


MIPASUKO mipya imejitokeza katika Mlima Kenya huku viongozi wakikosoana kuhusu mustakabali wa eneo hilo kisiasa baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.

Huku Bw Gachagua akiahidi kupatia eneo hilo mwelekeo wa kisiasa baadaye mwezi huu, aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga amejitokeza kumpiga vita na wazee wa jamii wakijitenga naye na kuunga mbunge huyo wa zamani wa Mathira.

Hayo yanajiri huku aliyekuwa rais wa nne wa Kenya, Uhuru Kenyatta akikumbatia serikali baada ya kuondolewa kwa Bw Gachagua na washirika wake kuteuliwa mawaziri.

Wiki jana, Bw Njenga alijitangaza kuwa mbabe wa siasa za Mlima Kenya na kuapa kwamba hataruhusu mrengo wa Bw Gachagua kuchochea eneo hilo dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.

“Tunazungumza kuhusu umoja wa watu wa Mlima Kenya, Wakikuyu, Embu, na Wameru na najua tutaungana na kuzungumza kwa sauti moja ili kutetea maslahi yetu,” alisema Jumanne wakati wa mkutano katika uwanja wa maonyesho wa -Kabiruini ambao ulivutia mamia ya vijana.

Wakati wa mkutano huo ambapo makumi ya bendera za Kenya zilipeperushwa katika onyesho lililoonekana kupangwa na wafuasi kutoka sehemu mbalimbali za nchi, Bw Njenga alitoa wito kwa wakazi wa eneo la Mlima Kenya kumuunga mkono Rais Ruto na viongozi wengine waliochaguliwa katika juhudi za maendeleo mashinani.

Njenga ni “mcheshi”

Alipuuzilia mbali madai kuwa eneo hilo limeacha utawala wa Kenya Kwanza kufuatia kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.’Eneo linasalia kuungana na serikali,’ Njenga alisema.

“Kinyume na uvumi wa watu wengi walioasi, ni mtu mmoja tu ambaye ameachana na Kenya Kwanza.”Hata hivyo, Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa Kikuyu Bw Wachira Kiago alimtaja Bw Njenga kuwa “mcheshi” akisema watu wa Mlima Kenya hawatamfuata.

“Kiongozi wetu mkuu ni Rigathi Gachagua na tuko nyuma yake kwa dhati. Hatutayumbishwa kujiunga na Bw Njenga kwa sababu tunajua hatatupeleka popote. Wakati huo huo, hatumpingi Naibu Rais wa sasa Kithure Kindiki ambaye pia ni mtoto wetu,” Bw Kiago aliambia Taifa Leo mnamo Ijumaa, Januari 3, 2025.

Tangu Bw Gachagua ang’atuliwe mamlakani Oktoba 17, 2024, baadhi ya wafuasi wa Ruto viongozi wa Kati mwa Kenya – haswa wabunge waliopiga kura ya kumfukuza – wamekabiliwa na uhasama na wametajwa kuwa wasaliti.Ni tamko la Bw Njenga kwamba “jeshi” lake litawapa usalama baadhi ya wabunge watakapozuru mashinani, ambalo limezua taharuki kwa viongozi.

 

Aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Bw Maina Njenga ahutubia wanahabari nyumbani kwake Ongata Rongai katika Kaunti ya Kajiado mnamo Januari 1, 2024. PICHA | Maktaba

Bw Njenga alisema ulinzi huo ni muhimu ili wabunge waweze kusimamia utekelezaji wa miradi ya Rais Ruto na kushirikiana na jamii ili kulinda rasilimali za Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF).Aliapa kuanzisha mashambulizi ya kisiasa dhidi ya Bw Gachagua.

Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wameuliza ni kwa nini utawala wa Rais Ruto, iwe moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, umegeuka na sasa unamtegemea Bw Njenga katika eneo la Mlima Kenya katika kile kinachoonekana kupinga ushawishi unaoongezeka wa Bw Gachagua.

“Kundi hilo huenda lisijihusishe na uhalifu kwa sasa lakini changamoto inaweza kutokea wakati mahitaji yao yote hayatatimizwa,” mchambuzi wa masuala ya kisiasa ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina akitaja unyeti wa suala hilo.

 

 

Wazee waunga Gachagua

Baadhi ya wazee wa Kikuyu pia wametahadharisha kuwa huenda kundi hilo likafufuka, wakisema watakuwa macho na kuhakikisha halifanyiki.

“Tutaangalia shughuli zao kwa umakini baada ya mkutano huo. Sisi wazee hatupingi msaada wao kwa serikali na utekelezaji wa miradi lakini hatutakubali wageuke kuwa wahalifu. Hii ni kwa sababu baadaye watalengwa na serikali ile ile,” akasema mzee ambaye pia aliomba kutotajwa jina kutokana na masuala ya usalama.

Hatua za kisiasa za hivi punde za Bw Njenga zimezua hisia, huku mkosoaji mkali wa Rais Ruto sasa akigeuka kuwa mtetezi wake mkuu. Bw Njenga kwa muda wa miaka miwili iliyopita amekuwa akiwindwa na maafisa wa usalama, na alishtakiwa kwa kupatikana na silaha haramu.

Hata hivyo, kesi hii iliondolewa Novemba mwaka jana. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2022,  Bw Njenga alikuwa miongoni mwa waathiriwa wa kwanza wa Kenya kwanza kuteswa kutokana na ushawishi wake mkubwa hasa kwa vijana katika Mlima Kenya.

Haikuchukua muda kabla ya uongozi kuanza kuwakandamiza wafuasi wake na kutafuta sababu zilizofanya ashtakiwe mahakamani.Mara nyingi Njenga angeitwa kuhojiwa katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai jijini Nairobi pamoja na wasaidizi wake wa karibu na washirika wake.

Aliyekuwa gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria naye anataka serikali kuchunguza vuguvugu jipya la kisiasa linalohusishwa na Bw Gachagua.Wafuasi wa Gachagua, wakiwemo viongozi waliochaguliwa hivi majuzi wamekuwa wakijiita ‘Itungati’, jina linalopewa wapiganaji wa Mau Mau waliopigana na wakoloni.

Lakini Wa Iria alisema vuguvugu hilo linafaa kuchunguzwa kwani linahatarisha usalama katika eneo la Mlima Kenya.

Vuguvugu hilo, gavana huyo wa zamani alidai, limekuwa likifanya mikutano ya mashinani na kuitumia kuwatisha viongozi ili wawaunge mkono huku wakiweka chuki kwa wale wanaoshindwa kuwaunga mkono.

“Vazi hili limechukuliwa kuwa la kitamaduni lakini halijasajiliwa kama kikundi cha kitamaduni. Linapenda kuajiri wanachama kutoka sehemu nyingine za nchi. Hili ni vazi la kudumaza maendeleo katika kaunti za eneo la Mlima Kenya,’”Bw Wa Iria alisema.

Mnamo Ijumaa, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichungwa alidai Bw Gachagua anahusika na utekaji nyara unaondelea nchini madai ambayo naibu rais huyo wa pili alipuuza.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*