Gachagua atisha kumpeleka Njenga ICC, asema hatasaidia Ruto kutoboa mlimani – Taifa Leo


ALIYEKUWA naibu rais Rigathi Gachagua, ameitaka serikali kukoma kumtumia aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga kumzima pamoja na washirika wake eneo la Mlima Kenya.

Bw Gachagua alisema hata Rais Ruto akimtumia Bw Njenga na kumpatia ulinzi, hataweza kurejesha ushawishi aliopoteza katika eneo la Mlima Kenya.

“Maina Njenga alitumiwa na serikali ya Daniel Moi kuwaadhibu watu wa Mlima Kenya kwa upinzani wao. Alihangaisha watu wetu kikatili. Kuwakata vichwa, kutahiri wanawake wetu, kunyang’anywa uchumi wetu. Siku moja genge lake liliwakata vichwa watu 29 katika kaunti ya Nyeri. Ilimchukua John Michuki miaka 4 kushinda genge hilo. Historia inajirudia.

‘Kutulazimisha tukubali rais na naibu wake’

“Ametumwa Mlima Kenya ili kutulazimisha tukubali rais na naibu wake na vile vile kuwasindikiza wasaliti waliokataliwa kuanza shughuli zao mashinani,” alidai na kutisha kuwasilisha ukatili ambao Mungiki ilitendea wakazi katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).

“Tutampeleka Maina Njenga ICC Rais anapaswa kufika Mlima Kenya ana kwa ana na kuzungumza na wananchi. kupata moja kwa moja kile ambacho kimemomonyoa umaarufu wake. Lakini Maina Njenga hata akiwa na silaha chafu hatatulazimisha kukupenda kwa nguvu,” alisema.

Naye Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga amemwambia Rais William Ruto akome kutumia kila mbinu ili kuvutia eneo la Mlima Kenya, akisema wakazi wanataka muda wa kupona kufuatia kutimuliwa kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.

“Walipomfukuza mtoto wetu serikalini walisherehekea lakini tulisikitika. Tuko katika maumivu makali na huu si wakati mwafaka wa kutuma wajumbe ili kujaribu kutuvutia tena. Baada ya kupoteza, tulichanganyikiwa na wanapaswa kutupa muda wa kupona, tafadhalini tuacheni,” Bw Kahiga aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano.

Kurejesha ushawishi wake mlimani

Jaribio la hivi punde zaidi la rais kutaka kurejesha ushawishi wake eneo hilo lilikuwa ni kitendo cha aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga kuingia katika kaunti ya Nyeri mkesha wa mwaka mpya alipohutubia mamia ya vijana katika uwanja wa Kabiru-Ini chini ya ulinzi mkali.

Bw Njenga alitangaza kuwa eneo hilo linaunga mkono serikali ya Rais Ruto, akisema ataongoza kampeni za rais mlimani.Tangu Bw Gachagua aondolewe mamlakani Oktoba 17, 2024, Dkt Ruto na naibu wake Profesa Kithure Kindiki wamekabiliana na chuki katika eneo hilo huku wakazi wengi wakisema walisalitiwa.

Wabunge waliopiga kura kumtimua naibu wa rais wa zamani pia wamelazimika kusalia Nairobi wakihofia mashambulizi nyumbani.Bw Njenga alisema atamkabili Bw Gachagua ana kwa ana, akiongeza kuwa hatamruhusu naibu rais huyo wa zamani kuendelea na kampeni zake dhidi ya bosi wake wa zamani.

Vijana kuwalinda wabunge

Aliwataka vijana kuwalinda wabunge wanaposimamia miradi ya maendeleo katika maeneobunge yao. Bw Gachagua, ambaye ameahidi kutoa mwelekeo wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya baadaye mwezi huu, hivi majuzi amezidisha mikutano na viongozi hasa kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wameendelea kumiminika nyumbani kwake Wamunyoro,Mathira.

Bw Kahiga alisema kuingia kwa Bw Njenga hakukuwa na maana na ‘hakutabadilisha chochote’, akiongeza kuwa ‘kutafanya eneo hilo kutengwa zaidi’ kwa kuwa ‘ ni watu wachache sana’ wanakubali aina yake ya siasa.

“Aambiwe kuwa sisi ni watu wapenda amani. Hatujasahau shughuli zake za zamani ambazo zinatutia uchungu na hatutaki kumbukumbu hizo. Wanaomtuma watuheshimu. Wanapaswa kujua kwamba hatashawishi mtu yeyote upande wake,” gavana alisema.

“Pia wanafaa kukoma kumshambulia Bw Gachagua kwa sababu inatufanya tuhisi tumetumiwa na kutupwa. Hakuna mtu anayepaswa kutusukuma kufanya uamuzi kuhusu tunakoelekea kama jamii. Yeyote anayejaribu kumuondoa Bw Gachagua katika ulingo wa kisiasa atapatwa na mshtuko. Tukutane 2027,” akasema Bw Kahiga.

Gavana huyo pia alipuuzilia mbali uteuzi wa waliokuwa washirika wa Rais Uhuru Kenyatta katika serikali, akisema watu hao walishindwa katika uchaguzi na kwamba hawakuwa maarufu.

Walioteuliwa kuchukua nyadhifa za Mawaziri wanaosubiri kuchunguzwa na Bunge ni aliyekuwa Seneta wa Nyeri Mutahi Kagwe (Kilimo), aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo (ICT) na aliyekuwa gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui (Biashara).

Bw Ndiritu Muriithi, aliyekuwa gavana wa Laikipia aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) na kuapishwa rasmi mnamo Desemba 30, 2024. Bw Kahiga alisema walioteuliwa ‘hawafai kufikiria kuwa wanaweza kuchukua nafasi ya Bw Gachagua ambaye alitushawishi kumpigia kura Rais’.

Watu waliokataliwa na wapiga kura

“Unawezaje kuteua watu waliokataliwa na wapiga kura? Tunajua kwamba baadhi ya watu hao wanataka kuwa serikalini kwa ajili ya maslahi yao ya kibinafsi huku wengine wakitafuta ulinzi. Athari za kuteuliwa kwao serikalini hazitazingatiwa. Kwa vyovyote vile hatutaki mtu yeyote atuchanganye kwa kuwa tuko nyuma ya kiongozi wetu Rigathi Gachagua,” Bw Kahiga alisema.

Bw Wahome Kamoche, katibu wa Jubilee kaunti ya Nyandarua alisema kwa sasa, eneo la Mlima Kenya linahitaji marekebisho kamili ya tabaka la kisiasa, akisema viongozi wa sasa ‘wamepoteza mawasiliano’ na wapiga kura.

Alisema viongozi akiwemo Bw Kahiga, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Githunguri Gathoni wa Muchomba, John Methu (Seneta wa Nyandarua) Lenny Kivuti (aliyekuwa Seneta wa Embu) na aliyekuwa gavana wa Meru Peter Munya walikuwa na uwezo wa kutoa mwelekeo wa baadaye ya kisiasa ya Mlima Kenya.

“Tunataka viongozi wapya watupe mwelekeo tutakaochukua kwa sababu tumechoka kuwarejelea wanasiasa walewale wanaokataa kushughulikia na masilahi ya wakazi,,”Bw Kamoche alisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*