Nani aliteka Gen Z hawa watano walioachiliwa huru serikali ikikana kuhusika? – Taifa Leo


HUKU watano kati ya vijana sita walioripotiwa kutoweka baada ya kutekwa nyara mwezi jana wakiachiliwa huru, swali kuu linasalia: Ni nani aliwatendea ukatili huo.

Hii ni baada ya polisi, ikiwemo Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kujitenga na utekaji nyara. Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja pia alisema hakuna kituo chochote cha polisi kilichokuwa kikiwazuilia vijana hao na Rais William Ruto akasisitiza kuwa serikali yake haihusiki na vitendo vilivyo nje ya katiba na sheria.

Jana, familia za Billy Munyiri Mwangi, Ronny Kiplagat, Benard Kavuli na Peter Muteti zilithibitisha kuwa walipatikana wakiwa hai. Mchora vibonzo Gideon Kibet, almaarufu Kibet Bull, naye aliripotiwa kutelekezwa katika eneo la Luanda, Vihiga majira ya saa tisa usiku.

Hata hivyo, mateka mwingine Steve Mbisi bado hajulikani aliko tangu Desemba 20, 2024 alipotoweka. Bw Mwangi, Kiplagat, Kavuli na Muteti waliachiliwa huru katika sehemu mbalimbali nchini Jumatatu.

Kijana Billy Munyiri Mwangi ambaye aliachiliwa jana na waliomteka nyara. Picha|Hisani

Bw Mwangi, ambaye alitekwa nyara mjini Embu, alifika nyumbani kwao asubuhi na kuungana na familia yake huku Bw Kiplagat aliyetekwa eneo la Kikuyu aliachiliwa huru katika kaunti ya Machakos.

Naye Bw Kavuli, aliyepigwa na kuchukuliwa kwa nguvu akiwa Ngong Desemba 24, 2024, alipatikana Kitale ilhali Bw Muteti aliyetekwa nyara eneo la Uthiru akiachiliwa na watekaji wake katikati mwa jiji la Nairobi.

Kwa ujumla, watu 25 waliotoweka baada ya kudaiwa kutekwa nyara tangu Juni mwaka jana wakati wa maandamano ya Gen Z, bado hawajulikani waliko.Katika ripoti yake ya hivi punde iliyotolewa mwishoni mwa Desemba 2024, Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNHRC) ilisema kuwa angalau visa 82 vya utekaji nyara vimeripotiwa tangu Juni 2024.

Peter Muteti

Bw Mwangi, Bw Kavuli, Bw Muteti na Kiplagat waliachiliwa huru, na watu wasiojulikana, jana asubuhi wakati ambapo wazazi wao na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu walikuwa wakijiandaa kufanya maandamano kote nchini kuishinikiza serikali ielezee waliko.

Utawala wa Rais William Ruto umekana kuhusika na visa hivyo vya utekaji nyara, kiongozi wa taifa akisema Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) inapasa kusema waliko watu hao waliotekwa nyara.

Ijumaa wiki jana, aliwahutubia waombolezaji wakati wa mazishi ya mamake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Dkt Ruto alimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kutoa majibu kwa familia za waliotekwa nyara.

“Huduma ya Kitaifa ya Polisi, ni asasi huru, inaweza kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo,” Rais Ruto akasema katika eneo bunge la Kabuchai, kaunti ya Bungoma. Mwangi, aliyetoweka mnamo Desemba 21, baada ya kutekwa na wanaume wanne waliojifunika nyuso, mjini Embu, aliwasili nyumbani akiwa mchovu na dhaifu na hangeweza kuzungumza kwa ufasaha.

Naye Kiplagat aliyetoweka baada ya kuhudhuria ibada Kanisani katika eneo la Kikuyu, Kiambu mnamo Desemba 25, 2024, aliambia familia yake kwamba alitelekezwa katika kaunti ya Machakos. Dadake Mercy Cherutich aliambia Taifa Leo kwamba alipiga simu jana asubuhi, akisema ameachiliwa huru na yu njiani kuelekea Nairobi.

“Hakuweza kusema zaidi. Alisikika mwenye woga zaidi,” alieleza.Bw Kavuli alipatikana umbali wa kilomita 400 kutoka mji wa Ngong, alikochukuliwa kwa nguvu na wanaume wasiojulikana.

“Hamjambo watu wetu. Kaka yangu yu salama na tunashukuru Mungu kwa kumlinda. Asanteni marafiki wetu kwa usaidizi wenu na maombi,” dadake Mary Kavuli akasema jana kupitia ujumbe kupitia mitandao ya kijamii.

Bw Mwangi aliyetekwa na wanaume wanne waliomchukua kwa nguvu, alipokuwa akisubiri zamu kunyolewa katika kinyozi kimoja mjini Embu, mnamo Desemba 21 alipokelewa jana kwa furaha na familia, jamaa na marafiki.

Wazazi walimkumbatia Mwangi ambaye alikuwa anaongea kwa sauti ya chini huku akionekana dhaifu.Hakuelewa alivyofika nyumbani kwani alionekana kuchanganyikiwa na mwenye woga.Majirani wenye furaha pia waliungana na familia hiyo kusherehekea kurejea kwa Mwangi saa kadhaa jana.

“Tumefurahi kwamba mtoto wetu amerejea nyumbani akiwa hai,” akasema Bw Gerald Karicha, babake mwanafunzi huyo.Mwangi, ambaye alijitokeza siku 16 baada ya kutoweka, alielezea kwa machungu jinsi alifungiwa katika chumba kisicho na mwangaza na kutendewa aina mbalimbali za dhuluma.

Udhaifu wake kimwili ulioashiria kuwa mateka wake hawakumpa chakula cha kutosha walikomzuilia; bila kumruhusu kuwasiliana na familia yake.Mwangi aliambia familia yake kwamba, watekaji nyara wake walimzuilia katika chumba kidogo kilichokuwa na giza siku zote alizokuwa ametoweka.

Bernard Kavuli

“Alirejea nyumbani akiwa pekee yake saa mbili za asubuhi. Nilikuwa nyumbani na mamake nilipomwona akiingia. Yuko sawa na tunashukuru Mungu. Tunawashukuru wote waliotuliwaza na kutusaidia kupitia maombi,” akasema Bw Karicha.

Alieleza kuwa walimkimbiza katika hospitali moja ya kibinafsi viungani mwa mji wa Embu ambako aliongezewa maji na kupewa matibabu. Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji alimtembelea Mwangi hospitalini na kulaani kutekwa kwake.

“Tunashutumu vikali kutekwa nyara kwa Mwangi kwani huo ni ukatili uliokithiri mipaka,” akasema huku akitaka vitendo hivyo vikomeshwe. Bw Mukunji alipendekeza kuwa sheria ifanyiwe marekebisho ili serikali iwajibikie kikamilifu visa vya utekaji nyara raia.

“Sheria inaweka utaratibu ambao unapasa kufuatwa endapo mtu ametenda aina yoyote ya uhalifu. Kwamba mshukiwa wa uhalifu akamatwe na kuwasilishwa kortini sio kuzuiliwa kusikojulikana. Kwa hivyo, tunapendekeza sheria ibadilishwe ili mtu yoyote anapotekwa nyara serikali iwajibike badala ya kujiondolewa lawama,” akaeleza.

Mnamo Januari 2, mwaka huu Bw Karicha aliambia Mahakama Kuu Nairobi kwamba, waliomteka mwanawe wamekuwa wakimfuata kwa siku kadhaa kabla ya kutoweka kwake. Bw Karicha aliambia Jaji Bahati Mwamuye kwamba, mwanawe alichukuliwa na kusafirishwa kwa gari aina ya Toyota Fielder, double cabin yenye nambari ya usajili ya KDG 527 D.

“Ndio Mheshimiwa, gari hilo lilikuwa limezunguka nyumbani kwangu kwa siku tatu. Gari lingine lilikuwa aina ya Pick-up na ilikuwa nyuma ya hiyo Toyota Fielder,” akaelezea huku akilia kwa uchungu.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*