Guatemala yatuma wanajeshi 150 Haiti kuwasaidia polisi 400 wa Kenya kupambana na magenge – Taifa Leo


GUATEMALA CITY, Guatemala

KIKOSI cha wanajeshi 150 wa Guatemala kimewasili nchini Haiti kupiga jeki juhudi za kurejesha utulivu katika nchi hiyo inayozongwa na machafuko yanayotekelezwa na magenge ya wahalifu.

Kundi la kwanza la wanajeshi 75 liliwasili Ijumaa na lingine lenye wanajeshi 75 likifika Jumamosi jioni, kulingana na taarifa iliyotolewa na serikali ya Guatemala.

Wanajeshi hao wako nchini Haiti kupiga jeki vikosi vya walinda usalama vinavyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN) vikiongozwa na Kenya lakini ambavyo vimefeli kuzuia mashambulio kuendelea.

Mnamo Juni na Julai mwaka jana, Kenya ilituma jumla ya maafisa 400 wa polisi Haiti kusaidia polisi wa nchi hiyo kupambana na wahalifu.

Hawa ndio walikuwa maafisa wa usalama wa kwanza, sehemu ya kikosi cha maafisa 2,500, kutoka mataifa mbalimbali ya nje waliotarajiwa kushiriki shughuli za kulinda usalama Haiti.

Idadi ndogo ya walinda usalama kutoka Jamaica, Belize na El Salvador pia wako nchini humo kwa kibarua hicho kilichoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) huku Amerika ikiwa mfadhili wa shughuli hizo.

Rais wa Kenya William Ruto ametangaza kuwa serikali yake inalenga kuwatuma Haiti maafisa wengine 600 wa polisi kuanzia Januari mwaka huu.

Maafisa hao wamekuwa wakipokea mafunzo maalum tangu mwaka jana, katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi wa Utawala (AP) kilichoko Embakasi, Nairobi.

Hali ya hatari imedumu nchini Haiti huku utawala wa nchi hiyo ukipambana na magenge ya wahalifu ambayo yamedhibiti sehemu kubwa ya jiji kuu Port-au-Prince.

Kwa mfano, mnamo Machi 2024, magenge yenye silaha hatari yalevamia magereza mawili makubwa nchini Haiti na kuwaachilia huru karibu wafungwa 3, 700.

Nchini hiyo iliyoko eneo la Caribbean imekumbwa na misukosuko na majanga ya kimaumbile ndani ya miongo kadhaa iliyopita hali iliyopelekea taifa hilo kuwa mojawapo ya mataifa masikini zaidi katika eneo zima la Caribbean.

Utovu wa uthabiti ulianza kushuhudiwa Haiti baada ya kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mnamo 2021. Kiongozi huyo aliuawa na watu wenye bunduki na wasiojulikana.

Tangu wakati huo, nchini hiyo imezongwa na utovu wa usalama, kudorora kwa uchumi, ukosefu wa udhibiti kiuongozi na kisiasa na ongezeko la visa vya mashambulio ya magenge ya hatari ya wahalifu.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*