PALM BEACH, FLORIDA
RAIS mteule wa Amerika Donald Trump, Jumanne alikataa kusema hatatumia hatua za kijeshi au kiuchumi kutwaa Panama Canal na Greenland, sehemu ya ajenda ya upanuzi ambayo amekuwa akiendeleza tangu aliposhinda uchaguzi wa Novemba 5.
Trump, ambaye anaingia madarakani Januari 20, pia alizua wazo la kugeuza Canada kuwa jimbo la Amerika, akisema angedai matumizi ya juu zaidi ya pesa kutoka kwa washirika wa NATO na kuahidi kubadilisha jina la Ghuba ya Mexico hadi Ghuba ya Amerika.
Zikiwa zimesalia siku 11 kabla ya kushika wadhifa huo, Trump ameanza kuelezea sera ya kigeni bila kujali masuala ya kidiplomasia au wasiwasi wa washirika wa Amerika.
Alipoulizwa katika mkutano wa waandishi wa habari katika eneo lake la mapumziko la Florida ikiwa anaweza kuuhakikishia ulimwengu kuwa hatatumia nguvu za kijeshi au kiuchumi anapojaribu kudhibiti Panama Canal na Greenland, Trump alisema, “Hapana, siwezi kukuhakikishia kati ya hizo mbili, lakini naweza kusema hivi, tunazihitaji kwa usalama wetu wa kiuchumi”.
Trump alikosoa matumizi ya bidhaa za Amerika kwa Canada na msaada wa kijeshi kwa Canada, akisema Amerika haipati faida yoyote kutokana na kufanya hivyo, na kuuita mpaka kati ya nchi hizo mbili “mstari uliochorwa kwa njia isiyo halali.”
Alipendekeza atawekea ada Denmark ikiwa itapinga toleo lake la kununua Greenland, ambayo alisema ni muhimu kwa usalama wa kitaifa wa Amerika.
Muda mfupi kabla ya maoni ya Trump, mwanawe Don Jr aliwasili Greenland kwa ziara ya kibinafsi.
Denmark imesema Greenland, sehemu inayojitawala ya ufalme, haiuzwi.
“Sidhani kama ni jambo zuri la kuonyeshana uwezo wa kifedha wakati sisi ni washirika wa karibu,” Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen alisema Jumanne akijibu maoni ya Trump.
Waziri wa Masuala ya Nje wa Canada, Melanie Joly, alisema kwenye X, “Maoni ya rais mteule Trump yanaonyesha kutoelewa kabisa sababu ya Canada kuwa nchi yenye nguvu. Uchumi wetu uko imara. Watu wetu wako imara. Hatutarudi nyuma kamwe tukikumbwa na vitisho.”
Mwanadiplomasia mkuu wa Panama pia alipuuza tishio la Trump la kuchukua tena njia kuu ya kimataifa ya maji, ambayo Amerika ilikuwa imeunda na kumiliki kabla ya kuikabidhi nchi hiyo ya Amerika ya Kati mnamo 1999.
“Mikono pekee inayodhibiti Panama Canal ni ya Panama na hivyo ndivyo itakavyoendelea kuwa,” Waziri wa Masuala ya Nje Javier Martinez-Acha aliwaambia waandishi wa habari Jumanne.
Balozi Daniel Fried, mwanadiplomasia mstaafu wa Amerika ambaye kwa sasa anafanya kazi katika Baraza la Atlantiki, alisema maoni ya Trump yanatoa taswira ya “beberu wa karne ya 19.”
Kutwaa Greenland, Fried alisema, “kutaharibu NATO, kwa sababu kutatufanya tusiwe tofauti na Vladimir Putin,” rais wa Urusi.
Waziri wa Uchumi wa Mexico, Marcelo Ebrard, ambaye anatarajiwa kuchukua jukumu muhimu katika masuala ya biashara ya Amerika na Mexico, alionekana kutupilia mbali wito wa Trump wa kubadilisha jina la Ghuba la Mexico.
“Leo nitakuambia ikiwa tutaonana baada ya miaka 30, Ghuba ya Mexico bado itaitwa Ghuba ya Mexico,” alisema, na kuongeza kuwa serikali ya Mexico haitavutwa kwenye mjadala huo.
Leave a Reply