Milango ya gereza inasubiri kumpokea Inspekta Mkuu wa Polisi (IG) Douglas Kanja akikosa kufika kortini kama alivyoamriwa na mahakama.
Mnamo Desemba 31, 2024 Bw Kanja alitakiwa kufika kortini Januari 8, 2025 kutoa taarifa kuhusu kutekwa nyara kwa vijana sita ambao ni wakosoaji wa serikali.
Mbali na Bw Kanja, pia Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usalama wa Uchukuzi Nchini (NTSA) George Njau hawakufika kortini kama walivyokuwa wameamriwa mwisho wa mwaka jana.
Waitwa tena
Kufuatia ukaidi wao, Jaji Bahati Mwamuye aliamuru Mabw Kanja na Amin wafike mbele yake Januari 27, 2025 kuadhibiwa kwa kukaidi maagizo ya mahakama kwamba wawafikishe wahasiriwa sita wa utekwaji nyara.
“Hii mahakama imetilia maanani kwamba IG na DCI wamekosa kufika kortini kutoa ripoti kuhusu visa vya utekaji nyara wa wale wanaotuhumiwa kupinga utawala wa serikali ya Rais William Ruto,” Jaji Mwamuye alisema.
Jaji Mwamuye aliwaagiza Mabw Kanja na Amin wafike kortini Januari 27, 2025 kutegua kitendawili cha jinamizi hili la utekaji nyara wa Wakenya.
Pia, Jaji Mwamuye alisema siku hiyo ya Januari 27, 2025 ndiyo atakayowahukumu wawili hao kwa kukaidi agizo la mahakama la kuwaachilia vijana sita waliotekwa nyara Desemba 2024.
Mahakama ilifahamishwa na wakili Paul Nyamodi anayewawakilisha Mabw Kanja, Amin na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kwamba sio polisi waliwateka nyara vijana hao.
“Umekuwa msimamo wa IG tangu mwanzo kwamba sio polisi waliowateka nyara wanaume hao sita na kwamba hawajui waliowateka nyara ni kina nani,” Bw Nyamondi alimweleza Jaji Mwamuye.
Bw Nyamodi alisema haifai Bw Kanja na wengine – Bw Murkomen, Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji, Mkurugenzi Mkuu wa NTSA George Njau – kushtakiwa kwa jambo wasilolijua.
Mawasilisho yapingwa
Lakini wasilisho hilo lilipata upinzani mkali huku wakili mwenye tajriba pana na aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka na Wakili Martha Karua waliosema “maungamo hayo ya IG yanamaanisha kuna magege ya majambazi yanayowateka nyara wakenya wanaopinga uongozi wa Rais Ruto.”
Vile vile Seneta wa Busia Okiya Omtatah alieleza mahakama kuwa IG hapasi kupewa muda zaidi kwa vile anatakiwa kujua kila kitu kinachoendelea katika sekta ya usalama.
“IG Bw Kanja hafai kupewa siku 14, anatakiwa kupewa hadi Ijumaa Januari 10, 2025 kuwasilisha majibu kuhusu kinachoendelea katika idara ya usalama,” Bw Omtatah alisema.
Seneta huyu alisema kulingana na mawasilisho ya Bw Kanja kupitia kwa wakili Nyamodi kwamba hajui wanaoteka nyara vijana , basi inamaanisha hakuna serikali na pia hakuna usalama nchini. Alisema lazima Bw Kanja anajua kinachoendelea.
Naye Bw Musyoka alielezea mahakama kwamba matamshi ya Bw Kanja yanatia hofu kwa vile ameungama hajui kinachoendelea ilhali ndiye kinara wa usalama katika idara ya polisi.
“Nchi hii sasa inaendeshwa kiujambazi. Hakuna haja ya kupeleka Polisi Haiti kupambana na majambazi ilhali humu nchini watoto wetu wanatekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana,” Bw Musyoka alisema.
Aliomba korti imwamuru Bw Kanja awasilishe majibu kortini kuhusu anayewateka nyara vijana na pia aeleze hatua aliyochukua kusitisha maovu haya.
Mbali na vijana hawa sita, Bw Musyoka alisema kuna Diwani wa Kaunti ya Wajir aliyetekwa nyara Mei 2024 na hadi leo hajulikani aliko.
“Nusra familia yake izike mtu mwingine ambaye maiti yake iliokotwa ndani ya bwawa,” Bw Musyoka alisema.
Naye wakili Martha Karua aliomba mahakama iamuru Bw Kanja awasilishe ripoti Januari 10, 2025 kuhusu utekaji nyara uliokita mizizi nchini.
Wako wapi waliotekwa nyara?
Rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Faith Odhiambo alisema sharti mahakama ishurutishe asasi za usalama kuwatoa waliko wahasiriwa wawili Steven Mbisi Kavingo na Kelvin Muthoni ambao walitoweka Desemba 2024.
Wakili Daniel Maanzo anayewakilisha familia ya Bw Kavingo alimkosoa wakili Nyamodi ambaye pia anamtetea Bw Kanja kwa kudai wahasiriwa wote wa utekaji nyara wameachiliwa.
“Sio ukweli mateka wote waliachiliwa. Steven Mbisi Kavingo hajaachiliwa. Dada yake Stacy Mutua yuko hapa kortini amethibitisha ndugu yake hajaachiliwa,” Bw Maanzo akasema.
Jaji Mwamuye alimhoji Stacy Mutua na kufahamishwa kwamba “ndugu yao hajaachiliwa.”
Pia aliambia Jaji Mwamuye: “Kama familia tunasikitika sana. Mama yangu amekua mgonjwa hata hawezi fika Nairobi. Ombi langu na familia yangu ni wanaomzuilia Steven wamwachilie. Tumemtafuta kila mahali na hatujamwona.”
Mateka mwingine Bernard Kavuli alifika kortini na kueleza mahakama aliachiliwa Januari 6, 2025 eneo la Moi’s Bridge, Trans Nzoia kisha akasafirishwa hadi kituo cha polisi cha Ngong, Kajiado kisha akaunganishwa na familia yake.
Wakili Shadrack Wambui alieleza mahakama kwamba Bw Kavuli “amesema uhai wake ni kwa sababu ya mahakama.”
Vijana muwe macho
Naye Gerald Mwangi Karicha, baba yake Billy Mwangi aliyekuwa ametekwa nyara, alithibitishia mahakama kwamba mwanawe aliachiliwa Januari 6,2025.
“Nathibitisha mwanangu yuko nyumbani. Anapumzika. Aliachwa mjini Nyeri kisha akasafiri hadi nyumbani.”
Akihojiwa na Taifa Leo Bw Karicha aliwashauri vijana kuwa waangalifu kwa vile “wametambua sasa kwamba habari wanazotuma katika mitandao zinaweza kuwaletea shida.”
Akasema katika mahakama kuu ya Milimani baada ya kufika mbele ya Jaji Mwamuye: “Ninawashauri vijana wawe macho na waangalifu.Chungeni mnachotuma katika mitandao ya kijamii.”
Hata hivyo Bw Karicha alisema yeye na familia yake wana furaha kufuatia kuachiliwa kwao.
Mnamo Desemba 31, 2024 Bw Karicha aliangua kilio kortini akiomba “mwanawe Billy Mwangi aachiliwe.”
Lakini Jumatano Bw Karicha alikuwa mwenye furaha kufuatia kuachiliwa kwa mwanawe.
Walioachiliwa kutoka kizuizini kufikia sasa ni pamoja na Peter Muteti, Bernard Kavuli, Billy Mwangi, Gideon Kibet na Ronny Kiplangat.
Kufuatia kufika mahakamani Jaji Mwamuye alimwamuru wakili Abner Mango kuwasiliana nao na kuwapeleka waandikishe taarifa kwa maafisa wa DCI.
Muda wa uchunguzi
Jaji Mwamuye aliwaamuru wapewe muda kupumzika kisha wapelekwe katika makao ya DCI.
IG na DCI walieleza mahakama kupitia kwa mawakili wao kwamba uchunguzi unaendelea kubaini wanaoteka nyara vijana.
Lakini wakili Danstan Omari anayemwakilisha Bw Murkomen alieleza mahakama kuwa kesi hiyo haitakuwa na umuhimu wowote ikiwa waliotekwa nyara wote wataachiliwa.
“Kesi hii ya kuomba kuachiliwa kwa mateka haiwezi kuendelea ikiwa wataachiliwa kutoka waliko,” Bw Omari aliambia mahakama.
Wakili huyo pia alidokeza kwamba Bw Murkomen alishtakiwa kimakosa kwa vile hatekelezi kazi ya polisi ila anatoa mwongozo kuhusu usalama.
Lakini Bw Omtatah alisema Bw Murkomen yuko katika kitengo cha usalama na ameshtakiwa ipasavyo kisheria.
Jaji Mwamuye aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 27,2025.
Mawakili wote waliamriwa wawasilishe ushahidi kabla ya Januari 22, 2025.
Aliamuru kesi hiyo itajwe mbele ya naibu wa msajili wa korti Januari 23, 2025 na pande zote zieleze ikiwa zimewasilisha ushahidi.
Leave a Reply