MBUNGE wa Dadaab, Bw Farah Maalim, amejipata katika dhoruba ya lawama kufuatia matamshi aliyotoa katika hafla ya Rais William Ruto hivi majuzi eneo la Rift Valley akitetea serikali.
Katika matamshi yaliyojaa maneno ambayo hatuwezi kuchapisha ili kulinda maadili yetu kama gazeti la kitaifa na familia, Bw Maalim alisuta wanaopinga sera za serikali ya Rais Ruto huku akimtetea vikali kiongozi wa nchi na kubashiri atashinda muhula wa pili katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“Halafu washenzi wengine wanasema eti Kasongo Ruto aende( tunadondosha matusi), kwani anakalia kiti ya mama yao? Anakalia kiti yetu, ni sisi tulimchagua na tutamrudisha kwa kura nyingi,” alisema mbunge huyo katika video inayosambazwa mtandaoni.
Jana, Bw Maalim alikanusha kuwa kibaraka wa serikali na akahusisha matamshi yake na ‘kuteleza kwa ulimi’ lakini akaongeza kuwa kiongozi wa Taifa anafaa kuheshimiwa.
“Nasikitika kwa kuteleza ulimi lakini sijuti kwa matamshi yangu kwa kuwa ni lazima tuunganishe nchi hii anavyofanya rais. Amefanyia nchi hii mambo mengi mazuri ndani ya miaka miwili na anafaa kupatiwa muda wa kuendeleza ajenda yake nzuri bila kutatizwa,” Bw Maalim aliambia Taifa Jumapili kwa simu.
Alisisitiza kuwa nchi hii inafaa kuunganishwa na akahimiza viongozi kuepuka siasa za ukabila.
“Kupachika rais majina kama Kasongo sio busara. Hakujengi nchi na ni tabia inayofaa kulaaniwa kwa kuwa inagawanya nchi,” aliongeza.
“Hii ni mara ya kwanza yangu kuunga serikali iliyo mamlakani tangu enzi za serikali ya Muungano nilipokuwa naibu spika na ni kwa sababu nimeona mambo mazuri inayokusudia kufanyia Wakenya,” alisema.
Naibu spika huyo wa zamani ambaye katika bunge la sasa anahudumu katika jopo linalosaidia spika, alisema utawala wa Rais Ruto umefanya mengi katika muda wa miaka miwili kuliko serikali zilizotangulia na kwamba, kiongozi wa nchi anastahili kupongezwa.
Japo wadadisi wanasema ana haki ya kutoa maoni yake, wanahisi kama kiongozi wa hadhi yake anapaswa kupima maneno yake hasa ikizingatiwa mwaka jana alikasirisha wengi kwa kauli zake kuhusu vijana waliokuwa wakiandamana dhidi ya serikali.
Matamshi yake yanamsawiri kama kibaraka wa serikali licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya chama cha upinzani cha Wiper.Kulingana na seneta wa Busia Okiya Omtatah, matamshi ya hivi majuzi ya Bw Maalim yanaonyesha kutowajibika kwake kama kiongozi na ni hatari.
“Viongozi lazima waendeleze amani, heshima, na umoja, sio kuchochea vurugu au migawanyiko. Ni wakati wa kusimama pamoja dhidi ya matamshi ya sumu,” alisema Bw Omtatah kupitia X.
Wakili Donald Kipkorir alishangaa Bw Maalim amekuwa kibaraka wa kutetea serikali zaidi ya viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya chama tawala.
“Sisi ni wazee wa umri wa kutosha na pia wanafunzi wa historia ya siasa kujua kuwa katika kila msimu wa siasa, tuna watu kama Farah Maalim ambao kila wakati wanataka kuomboleza kwa sauti kubwa katika mazishi hata bila kujua aliyekufa ni nani au kucheza kwa nguvu zaidi kwenye harusi bila kujua bw harusi. Historia inatuambia jinsi taaluma ya kisiasa na maisha ya watu kama hao huisha. Inasikitisha kwamba mtu aliyechaguliwa kwa kura 3,000 anafikiri anaweza kuwashinda Wakenya 60 milioni kuhusu suala lolote,” alisema Bw Kipkorir.
Mwanaharakati Jerotich Seii alimtaja mbunge huyo kama kiongozi mwenye mdomo chafu anayeweza kuzua vurugu.
“Baada ya kupendekeza kudhuru vijana, sasa anajadili (tunaondoa neno) ya nani? Ruto anapaswa kufunza Farah Maalim maadili,” akasema akiandika kwenye X.
Bi Seii alikuwa akirejelea matamshi ya mbunge huyo mwaka jana yaliyokosolewa vikali aliyodai vijana waliokuwa wakipinga serikali hawakufaa kuhurumiwa.
“Farah ni mmoja wa viongozi wakorofi nchini Kenya. Kila akifungua kinywa chake hutapika chuki na migawanyiko. Ikiwa hiyo ndiyo tabia yake hadharani, najiuliza yukoje ana kwa ana. Amewahi kunukuliwa akiapa kudhuru vijana 5000 kwa siku. Inasikitisha sana,” akasema mtumiaji mwingine wa X.
Bw Maalim amekuwa akiangaziwa kufuatia hisia zake za kuudhi zilizomfanya asutwe na chama cha Wiper, hata hivyo, mbunge huyo alipuuza kikao cha nidhamu akisisitiza kuwa hajuti kuunga serikali na Rais William Ruto.
Leave a Reply