RAIS William Ruto anaendelea kukwepa Mlima Kenya, eneo ambalo lilikuwa kama ‘nyumbani’ kabla na baada ya uchaguzi wa 2022 huku tofauti kati yake na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua zikiendelea kushamiri.
Kufikia leo, Rais Ruto hajatia guu Mlima Kenya kwa siku 56, huku maswali yakiendelea kuzuka iwapo anahofia kutembelea eneo hilo kutokana na kuhofia ghadhabu za wakazi baada ya Bw Gachagua kuondolewa afisini.
Mara ya mwisho ambapo Rais Ruto alikuwa Mlima Kenya ni mnamo Novemba 16 ambapo alihudhuria hafla ya kusisimkwa kwa Askofu wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Embu Peter Kimani.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Bw Gachagua pamoja na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki. Wakazi wa Embu wakati wa hafla hiyo walimzomea Rais huku wakimshangilia Bw Gachagua kila mara jina lake lilipotajwa japo hakupata nafasi ya kutubu.
Tangu Bw Gachagua abanduliwe mamlakani mnamo Oktoba 9, Rais Ruto hajakuwa na lake Mlima Kenya huku wananchi wakionyesha wazi ghadhabu dhidi ya utawala wake.
Kinyume na hapo awali ambapo Rais alikuwa akizuru mlimani kila mara, akigawa kitita kwa makanisa na kujihusisha na raia, mambo yamekuwa tofauti huku wakazi wakikerwa na hata kukataa kusomwa kwa hotuba yake.
Mnamo Janauari 3, wakazi wa Mbeere Kaskazini, Embu walimzomea Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi alipojaribu kusoma hotuba ya rais kwenye mazishi ya mwanawe aliyekuwa Seneta wa Embu Lenny Kivuti.
Licha ya Bw Muturi kuwauliza umma mara kadhaa wamruhusu asome rambirambi hiyo, wakazi walikataa na akalazimika kuipa familia nakala ya ujumb huo wa pole. Ilipofika wakati wa Bw Gachagua kuhutubu, walimshangilia kishujaa hasa alipowakosoa viongozi wanaounga mkono serikali.
Hali ilikuwa hivyo hivyo, mnamo Novemba 24 waombolezaji walipokataa kusomewa rambirambi za Rais Ruto na Profesa Kindiki, wakati wa mazishi ya diwani mteule katika Bunge la Kaunti ya Murangá Mark Wainaina.
Gavana wa Murangá Irungu Kangáta alilazimika kukabidhi familia risala hizo za rambirambi za Rais na Profesa Kindki. Mshauri wa rais kuhusu masuala ya kiuchumi Moses Kuria naye alizomewa baada ya kuonekana akitoa matamshi yanayosifu serikali.
Naye mnamo Oktoba 11, Gavana wa Nakuru Susan Kihika naye alizomewa akisoma rambirambi ya Rais Ruto kwenye hafla moja ya mazishi eneobunge la Bahati
Wabunge kutoka Mlima Kenya ambao waliunga mkono hoja kumbandua Bw Gachagua wamekuwa wakipata wakati mgumu kuandaa mikutano maeneo yao wakihofia kuzomewa.
Bw Gachagua ameonekana kushughulishwa na Rais Ruto kuhepa Mlima Kenya na mnamo Disemba 22 alimwaambia wazi wakazi wamekasirika naye na aje awaombe msamaha.
“Bwana Rais, usisubiri ghadhabu zishuke kwa sababu zinaendelea kupanda. Watu wa Mlima walikupenda lakini umewasaliti, ukawachukia na kuwanyanyasa. Njoo uwaambie kwa nini umewafanyia haya yote,” akasema Bw Gachagua katika hafla moja ya mazishi Kaunti ya Nakuru.
Baada ya kuipa kisogo mlimani, Rais amekuwa akimakinikia sana ziara eneo la Nyanza, Magharibi na Bonde la Ufa, hasa kutokana na kunoga kwa ushirikiano wake na Bw Odinga.
Kwa mujibu wa Wakili Njiru Ndegwa, Rais Ruto saa hii anaweza kuzuru mlimani kama tu rais wa Kenya wala si rafiki ya eneo hilo kwa sababu wanafuata mkondo mwingine wa siasa.
“Aliharibu mkataba kuwa atauchunga mlima na ataheshimu kura zetu ambazo zilimpa mamlaka. Amevunja mkataba na Riggy G na sasa watu wameamua hawamtaki na hata akiomba msamaha, hawezi kuaminika,” akasema Bw Ndegwa.
Katika uchaguzi wa 2022, asilimia 47 za kura 7.1 ambazo Rais alipata zilitoka Ukanda wa Mlima Kenya. Hizo ni zaidi ya kura milioni 3.5 ambazo Rais sasa lazima apambane kuhakikisha anazirejesha mnamo 2027.
“Pia watu wa mlima hawataki mtu wa uongo, Ruto si mwaaminifu na tulidhani ni mmoja wetu lakini ni fisi amevaa ngozi ya kondoo,” akaongeza.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Profesa Macharia Munene anasema kuwa Rais Ruto hata akizuru mlimani hakutaleta mabadiliko ndiposa ameona amakinikie ngome za Raila.
“Gachagua si sababu kwa sababu hasira zilianza mapema na suala la lake limeongezea tu chumvi. Madai kuwa Ruto alisimamisha miradi iliyoanzishwa na utawala wa Uhuru yaliibua ghadhabu kuwa anafinyilia mlima,” akasema Profesa Macharia.
“Uchumi umekuwa ukizorota na kufutwa kwa watu wao pamoja na taratibu hasi kwenye sekta za afya, kilimo na elimu pia zimetamausha wakazi wa mlimani na hata katika ngazi ya kitaifa,” akaongeza.
Msomi huyo anasisitiza kuwa makosa ya Rais Ruto yalianza tu baada ya utawala kuchukua usukani na itakuwa vigumu kwake kupenya hata maeneo mengine iwapo utawala wake hautatimiza miradi.
Leave a Reply