Wanavyokabili uhalifu mtaani kupitia biashara ya uundaji mifuko – Taifa Leo


ENDAPO kuna kilichowakereketa maini, ni kuona vijana wenzao wakiuawa kwa kushiriki uhalifu miongo miwili iliyopita. 

Augustine Githaiga na rafikiye, Morris Auka, ambao ni wakazi wa mtaa wa mabanda wa Kawangware, pia walisikitika kushuhudia wengine wakiangamizwa na dawa za kulevya.

Ni matukio wanayokiri yaliwauma moyo, wasijue la dharura kufanya kuokoa nafsi za vijana wenza.

Ukosefu wa ajira na masomo, ulikuwa sababu kuu ya waathiriwa kujipata kukinzana na sheria.

Githaiga na Auka walipiga mahesabu ya haraka, ili kuokoa kizazi kijacho.

Kulingana na Auka, kuwashirikisha kwenye vibarua ikawa jawabu kwao “kuteka nyara” mawazo yao, na walikuwa na chaguo kubahatisha kati ya biashara ya kuunda mifuko ya khaki au mawe ya ujenzi.

Hata hivyo, baada ya kushauriana, anasema waliamua kuanzisha biashara ya mifuko.

Morris Auka, mmoja wa waanzilishi Kawangware Vision Centre, kampuni ya kuunda mifuko mtaani Kawangware, Nairobi akionyesha mfuko mdogo. PICHA|SAMMY WAWERU

“Lengo lilikuwa kazi ambayo vijana wangeingia, wangeifanya hadi jioni wasiwe na muda wa kurandaranda,” Auka anasema.

Ndio, wazo walikuwa nalo ila mtaji wa kutosha ulikuwa kizungumkuti.

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki, na kila mmoja aliweka mezani kidogo alichokuwa nacho kuokoa vijana wenzao – wengi wakiwa marafiki.

“Mfanyabiashara mmoja aliyemiliki duka la bidhaa za urembo, zikiwemo shanga na mikufu, aliyetushawishi kuwazia biashara ya mifuko ya khaki alitupiga jeki, na kwa jumla tukafikisha mtaji wa Sh50, 000,” Auka adokeza.

Walianza kwa mifuko iliyorembeshwa kwa nembo za wanyamapori, biashara ambayo iliunda nafasi za ajira kwa vijana 20.

Githaiga, alijukumika kusaka soko.

Shabaha ilikuwa hoteli na mikahawa ya kifahari Nairobi, wakiiuzia mifuko ya kusambaza vyakula.

Baadhi ya wafanyakazi wa Kawangware Vision Centre wakiunda mifuko ya khaki. PICHA|SAMMY WAWERU

“Mikahawa na hoteli za kifahari tulizoanza nazo, ilituundia jukwaa la kupata wateja zaidi,” Githaiga anaelezea.

Kila mfuko waliotengeza, uliwekwa lebo (tag) kuhamasisha bidhaa walizounda na anwani.

Hivyo ndivyo Kawangware Vision Centre ilivyozaliwa, biashara ambayo imeleta matumaini kwa vijana ambao hasa hawana karo kukata kiu cha masomo.

Miaka 20 baadaye, Githaiga anakiri hakujua endapo biashara waliyoanzisha itakuwa mradi mkubwa – unaosambaza bidhaa zake kwa hoteli na mikahawa ya kifahari nchini, ikiwemo benki, kampuni na mashirika.

“Tumefika tulipo kwa sababu ya bidii na ushirikiano,” anasema.

Kushawishi mikahawa ya kifahari, Githaiga anasema haikuwa rahisi hasa ikizingatiwa kuwa ni biashara inayoendelezwa mtaa wa mabanda unaohusishwa na uhalifu.

Kawangware Vision Centre, kampuni inayosaidia kukabiliana na uhalifu mtaani Kawangware, hutengeneza mifuko inayotumika na mikahawa na maduka ya jumla kupakia bidhaa. PICHA|SAMMY WAWERU

Kando na kuunda mifuko yenye nembo ya wanyamapori, sasa huweka logo za mashirika.

Begi, mifuko na bahasha wanazounda hutumia mikono pekee, kuanzia kubuni hadi kuweka nembo, logo, na ukamba.

Malighafi ni roli za karatasi za khaki au nyeupe zilizoundwa kwa bidhaa zilizotupwa au kukataliwa (madaftari, magazeti, shashi…), kutoka eneo la Viwandani (Industrial Area), Nairobi.

Badala ya mashine za kisasa kurembesha bidhaa, wanatumia skrini (screen printer) walizojiundia wenyewe.

Kwa siku, kulingana na Auka wanaunda mifuko 1, 000, soko lao likiwa la kijumla.

Francis Maina, 24, mmoja wa vijana walionufaika kupitia Kawangware Vision Centre, akipaka rangi kwenye skrini ya kuweka nembo kwenye begi. PICHA|SAMMY WAWERU

“Huunda kwa mujibu wa oda, na mfuko mdogo tunauza Sh20, na ule mkubwa Sh60,” akasema wakati wa mahojiano katika kiwanda chao Kawangware 56, Nairobi.

Tuliwapata wakishughulikia oda za Sands at Nomad, mkahawa mkubwa Kisiwa cha Diani, Pwani, na benki ya ABC.

Kando na hoteli, mikahawa, pia wana wateja wenye maduka Nairobi, Nakuru na Kisumu.

Asubuhi, wanapoingia, Auka aliambia Akilimali kwamba huanza kwa maombi, kisha kukagua oda zilizoingia.

Kwa sasa, wana jumla ya wafanyakazi 13 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 32.

Vilevile, kuna vibarua wa kuunda kamba (handles).

“Wanaounda kama hufanyia kazi nyumbani na kutusambazia,” anasema Zipporah Mukalo, msimamizi wa wafanyakazi.

Zipporah Mukalo, msimamizi wa wafanyakazi Kawangware Vision Centre, akionyesha mfuko wa maridadi. PICHA|SAMMY WAWERU

Francis Maina, 24, ni mmoja wa vijana walionufaika kupitia Kawangware Vision Centre.

Alijiunga na mradi huo 2019 baada ya kukosa karo kusoma shule ya upili.

“Nusra nitekwe nyara na kero ya dawa za kulevya na kunywa pombe,” anasema, akiridhia mradi huo kuokoa maisha yake.

Maina sasa anakiri kuwa na kila sababu ya kutabasamu kwani anamudu kukithi mahitaji muhimu ya kimsingi.

Wakitathmini jinsi kiwango cha uhalifu kilikuwa awali Kawangware 56, Auka na Githaiga wanaona mabadiliko makubwa.

“Vijana tunaoajiri, hutoka kazini wakiwa wamechoka hivyo basi hawana muda wa kuzunguka”.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*