WAZIRI Mteule wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Mutahi Kagwe, ameonekana kuwa na maoni tofauti na Rais William Ruto kuhusu zoezi la utoaji wa chanjo ya mifugo kote nchini.
Wakati Rais anasisitiza kuwa wakulima wote lazima wahakikishe mifugo wao wanapatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa FMD na Peste des Petits Ruminants (PPR), Bw Kagwe anasisitiza kwamba hakuna mkulima atakayelazimishwa mifugo wake wapate chanjo hiyo.
Isitoshe, Waziri huyo wa zamani wa Afya amesisitiza kwamba dawa zitakazotumika zitatengenezewa hapa nchini Kenya.
Serikali inapania kutoa chanjo kwa ng’ombe wapatao milioni 22, na kondoo na mbuzi milioni 50.
Jumanne, Januari 14, 2024, akipigwa msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi, Waziri Kagwe alisisitiza kuwa, endapo ataidhinishwa na kutwaa mikoba ya Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, ni wakulima watakaokubali mifugo wao watapewa chanjo.
“Hakuna atakayelazimishwa. Huwezi kulazimishwa kwa bunduki, wala hakuna atakayekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi kwa kukataa mifugo wako wapewe chanjo,” Bwe Kagwe alisisitiza.
“Mifugo ni mali ya watu binafsi, sio wa serikali. Ikiwa una mbuzi, tutakuuliza ikiwa unataka wapewe chanjo. Ikiwa utakubali, tutamchanja. Ikiwa utakataa, hatutamchanja. Sawa na ng’ombe, tutakuuliza iwapo unataka apewe chanjo. Ikiwa utakubali, basi tutampa,” aliongeza Kagwe.
Waziri huyo alionya kuwa kulazimisha wakulima mifugo wao wapate chanjo kutazua fujo wakati wa zoezi hilo.
“Hebu tafakari migogoro ambayo itazuka kwa kushinikiza wafugaji! Hiyo sio njia sahihi,” aliiambia kamati iliyoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Moses Wetangula.
Hata hivyo, Waziri mteule huyo alihakikishia wabunge kwamba chini ya uongozi wake, Wizara ya Kilimo itahakikisha kuwa wakulima wanapata maamuzi yaliyo sahihi na yenye mashiko.
Rais William Ruto, amenukuliwa awali akielezea kughadhabishwa kwake na wanaokosa zoezi hilo akiwataja kama “adui wa maendeleo”.
Baadhi ya wakulima wametoa onyo dhidi ya kulazimishwa mifugo wao kupata chanjo.
Mdahalo kuhusu zoezi la chanjo kwa mifugo umegaragazwa mitandaoni, ambapo Wakenya wanatilia shaka kuhusu uhalisia wa dawa zitakazotumika.
Shughuli hiyo ya kitaifa inatarajiwa kuanza mwezi huu, Januari 2025.
Bw Kagwe alihakikishia umma kwamba chanjo zitakazotolewa zinaundiwa nchini na KEVEVAPI, taasisi ya kiserikali inayohusika na utengenezaji wa chanjo za mifugo.
KEVEVAPI imekuwa ikizalisha chanjo ya magonjwa kama vile FMD na PPR kwa zaidi ya miaka 12.
“Nitashirikiana na wataalamu wanaoelewa suala hili vizuri, ikiwemo KEVEVAPI, inayounda chanjo za mifugo,” alieleza Waziri Kagwe.
Kagwe alisisitiza kwamba chanjo itakayotumika ni iliyotengenezwa na KEVEVAPI pekee, na kwamba hakuna dawa zitakazoagizwa nje ya nchi.
Aidha, aliahidi kuweka mikakati bora ya mawasiliano ili kukabiliana na kile alichokiita “taarifa potovu mitandaoni”.
Wakosoaji wa zoezi hilo wanadai kwamba serikali ina ajenda fiche, wakihoji linafadhiliwa na mabwanyenye kutoka ng’ambo wenye tamaa za kibinafsi.
Serikali nayo kwa upande wake, inasema hatua hiyo itasaidia kufungua soko la bidhaa za mifugo haswa nyama, katika masoko ya ng’ambo.
Kwa sasa, ni karibu asilimia 10 pekee ya mifugo wanaopewa chanjo, na serikali inapania kuongeza idadi hiyo kwa kufanya shughuli hiyo kuwa la kitaifa.
Huduma za Kilimo na Maendeleo ya Mifugo ni jukumu la serikali za kaunti, baada ya sekta hiyo kugatuliwa na Katiba ya sasa iliyopitishwa 2010.
Akihojiwa kuhusu msimamo wake wa bidhaa za GMO, na vilevile dawa za kilimo zenye kemikali zilizopigwa marufuku kutumika katika mataifa yaliyoziunda, ikiwemo fatalaiza, Bw Kagwe alisisitiza kuwa hilo halitakubalika Kenya.
Baadhi ya dawa zenye kemikali – zilizopigwa marufuku kutumika katika mataifa asili, zimepata mianya kuingia nchini.
“Sisi si vyombo vya kufanyiwa majaribio. Hatutakubali kutumika,” alisema.
Mwaka jana, 2024 Mahakama Kuu ilitupilia mbali mseto wa kesi zilizowasilishwa kortini kusimamisha kuondolewa kwa marufuku iliyowekwa pembeni kuzuia usambazaji wa bidhaa za GMO.
Rais William Ruto aliondoa marufuku hiyo ya miaka kumi, 2022 miezi michache baada ya kutwaa uongozi kutoka kwa mtangulizi wake Bw Uhuru Kenyatta – ambaye kwa sasa ni Rais Mstaafu.
Leave a Reply