Mwanaharakati ataka Mkurugenzi Mkuu wa KeRRA Kiprop Kandie kuondolewa – Taifa Leo


MWANAHARAKATI wa haki za binadamu Francis Awino anataka uteuzi wa Philemon Kiprop Kandie kama Mkurugenzi Mkuu (DG) wa Mamlaka ya Barabara za Vijijini nchini (KeRRA) kutupiliwa mbali.

Katika ombi hilo, Bw Awino ambaye ni Rais wa Bunge la Mwananchi anaitaka mahakama ifuate uamuzi wa Jaji James Rika wa Mahakama ya Leba kuwa halali tangu alipobatilisha notisi ya Gazeti la Serikali iliyomteua Bw Kandie kuwa DG.

Bw Awino anashangaa ni kwa nini Bw Kandie ameendelea kutekeleza majukumu yake na kupata mshahara kutoka kwa hazina ya umma, ilhali uteuzi wake ulifutiliwa mbali 2023.

Katika kesi hiyo, Bw Awino anamtaka hakimu Enoch Chacha Mwita kusisitiza tena matokeo ya hukumu ya Mei 31, 2023 ambapo Bw Kandie aliondolewa afisini kufuatia kubatilishwa kwa Notisi ya Gazeti Namba 4309.

Jaji Rika aliamua, “Amri iliyotolewa katika mahakama hii na kufuta Notisi ya Gazeti Namba 4209 ya Aprili, 13, 2022 inayomteua Philemon Kiprop Kandie kama Mkurugenzi Mkuu wa KeRRA.”

Katika maombi mapya, Mahakama Kuu inahimizwa kumwondoa afisini Bw Kandie kama ilivyoagizwa awali na Mahakama ya Leba.

Uteuzi wa Bw Kandie kama DG ulipingwa na Samson Nzivo Muthiani ambaye alidai kuwa uteuzi wake ulifanyika haraka kinyume na sheria na utaratibu.

Bw Muthiani alikuwa amemweleza hakimu kwamba tangazo la wadhifa wa DG KeRRA lilifanywa haraka na kwamba waliotuma maombi walipewa siku 13 pekee za kuyatuma.

Alimweleza Hakimu Rika kwamba tangazo la wadhifa huo halikuwekwa katika tovuti ya tume ya utumishi wa umma, hivyo basi kuwafungia wengi nje.

Bw Muthiani alimweleza hakimu kwamba suala la jinsia pia halikuzingatiwa katika mchakato huo kulingana na Katiba.

“Matokeo yaliamuliwa mapema. Uteuzi, kutangaza kwenye Gazeti la Serikali na kutia saini mkataba na Bw Kandie ulifanyika siku moja baada ya mahojiano kukamilika. Hili litawezekana tu ikiwa matokeo yameamuliwa mapema,” Jaji Rika aliamua.

Jaji Mwita ameagiza Bw Awino awasilishe karatasi hitajika mnamo au kabla ya Machi 2025 kesi hiyo itakaposikizwa.

Katika kesi hiyo, Awino anaitaka mahakama kutoa agizo la kumshinikiza Bw Kandie kurejesha pesa na marupurupu yote aliyopokea katika kipindi hicho.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*