Wewe Muturi tutakufanyia kama Gachagua, Osoro achemka – Taifa Leo


KIRANJA wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro amemwambia Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi kujiuzulu la sivyo atakabiliwa na hoja itakayolenga kumng’atua katika wadhifa wake.

Bw Osoro amemkashifu Waziri huyo kwa mashambulizi yake makali dhidi ya utawala wa Rais William Ruto, akisema kufanya hivyo ni kama kutikisa meli akiwa angalimo.

Mbunge huyo wa United Democratic Alliance (UDA) pia alimpa Bw Muturi chaguo la kuomba msamaha ikiwa anataka aendelee kuhudumu katika utawala wa Kenya Kwanza.

Akiongea mnamo Jumanne, Januari 14, 2025 katika eneo bunge lake, Bw Osoro alimkashifu Bw Muturi na kuongeza kuwa iwapo atakosa kujiuzulu au kuomba msamaha, watamshughulikia sawia na walivyomfanyia aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Wewe ni Katibu wa baraza la mawaziri. Unaketi kwa cabinet. Unaketi na rais kila siku, unaongea na polisi kila siku, unaita press kulia juu ya polisi Justin Muturi. Na unajua sheria. Ulikuwa Spika. Leo mimi nakwambia, mbele ya hawa watu wangu. Ile kiboko tulipiga Gachagua, ndio inakuja kwako. Ujiuzulu ama tukutoe. Vile tuna-resume bunge, kwa sababu tuko na siku 14 ndo tu-resume bunge, Justin Muturi you have three options. Ya kwanza resign, ya pili apologize tuignore hiyo maneno, ya tatu, we will impeach you. Tutacollect signatures uende nyumbani. Huwezi kuhudumia serikali ya Kenya yenye unalima kila siku

Mwanzoni mwa wiki hii siku ya Jumapili, Bw Muturi aliikosoa serikali alipotaka kukomeshwa kwa visa vya utekaji nyara na mauaji ya watu wanaokisiwa kuwa wakosoaji wa Rais William Ruto na utawala wake.

Akionyesha kusononeka kwake, Waziri Muturi aliibua wasiwasi kwamba watekaji wa mwanawe Leslie Muturi bado hawajashtakiwa katika mahakama yoyote baada ya kumteka miezi sita iliyopita na baadaye wakamwachilia.

Waziri huyo katika kikao na wanahabari alidokeza kuwa hajawahi kupata maelezo kuhusu ni kwa nini mwanawe alichukuliwa mateka licha ya juhudi zake za kuwasiliana na mamlaka husika.

“Ninafahamu kikamilifu fundisho la uwajibikaji wa pamoja, lakini kwa vile mimi pia ni mwathiriwa wa utekaji nyara na sijapata majibu yoyote, nimechukua hatua hii isiyo ya kawaida ili suala hilo lijadiliwe kwa uaminifu na uwazi,” Bw Muturi alisema.

Alipoulizwa ikiwa aliwasilisha waraka wa kujiuzulu kutokana na masaibu yaliyompata mwanawe, Bw Muturi alisema hakuwa amefanya hivyo.

Pia aliongeza kuwa haogopi kufutwa kazi kama waziri kwa kusema mawazo yake.

Waziri huyo alisema ameweka imani yake kwa Mungu iwapo Rais William Ruto ataamua kumuonyesha mlango.

Huku akimshutumu Bw Muturi, Bw Osoro aliongeza kwamba watu kutoka eneo la Mlima Kenya wanafaa kukoma kutoa “kelele zisizo za maana” kwa kiongozi wa taifa na akataja kwamba wao ndio waliofaidika zaidi na serikali yake.

“Nataka kuuliza watu wa Mlima Kenya, kwa nini mnalalamika sana ilhali mmekuwa na marais watatu. Kwa nini humkutatua shida zenu zote wakati mlikuwa na marais hao. Kwa nini wakati Rais Ruto amekuja, ndipo mnaanza kukumbuka hili na lile?” Osoro aliuliza.

Mbunge huyo aliongeza kuwa mlima huo hauna cha kubishana kwani Rais William Ruto amewajumuisha kikamilifu katika serikali yake.

Haiwezekani kwamba watu pekee wanaolalamika ni kutoka eneo moja. Mmeongezewa hata nafasi katika baraza la mawaziri na walioteuliwa wanapigwa msasa leo. Kwa sisi wengine, tupo tu. Unafikiri tuna furaha? Watu kama sisi (Abagusii) tuna nafasi moja pekee ya uwaziri

Mbunge huyo wa awamu ya pili aliongeza kuwa wataidhinisha uteuzi wa William Kabogo (Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali), Lee Kinyanjui (Uwekezaji, Biashara na Viwanda) na Mutahi Kagwe (Kilimo na Mifugo), kuhudumu katika serikali ya Rais William Ruto kama mawaziri.

Watatu hao ni washirika wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta. Uteuzi wao umeonekana kuwa njia moja ya Rais kujaribu kuokoa uungwaji wake mkono unaopungua kwa kasi katika eneo lenye watu wengi la Mlima Kenya.Eneo hilo lilichukizwa na rais kufuatia kutimuliwa afisini kwa aliyekuwa naibu rais wake Rigathi Gachagua.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*