WAZIRI Mteule wa Teknolojia na Mawasiliano, na Uchumi wa Kidijitali William Kabogo atakuwa miongoni mwa mawaziri mabilionea endapo wabunge watamwidhinisha kwa wadhifa huo.
Akijibu maswali kutoka kwa wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi Jumanne, Januari 14, 2025, Bw Kabogo alifichua anamiliki mali ya thamani ya Sh3.01 bilioni.
Gavana huyo wa zamani wa Kiambu atakuwa waziri nambari mbili kwa utajiri nyuma ya Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye aliambia kamati hiyo mnamo Oktoba 17, 2022 kwamba anamiliki mali ya thamani ya Sh4 bilioni.
Bilionea mwingine katika Baraza la Mawaziri ni Waziri wa Madini na Uchumi wa Kidijitali Ali Hassan Joho. Mnamo Agosti 4, 2024, Gavana huyo wa zamani wa Mombasa aliiambia kamati hii inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kwamba thamani ya mali yake ilikuwa Sh2, 361, 332, 249.
Jumanne, Bw Kabogo aliiambia kamati hiyo ya uteuzi kwamba mali yake inajumuisha ardhi ya thamani ya Sh700 milioni, magari ya thamani ya Sh40 milioni na nyumba za thamani ya Sh756 milioni.
Aidha, anazo Sh64 milioni katika akaunti za benki na hisa za thamani ya Sh1.5 bilioni katika kampuni na mashirika mbalimbali.
“Kwa ujumla, utajiri wangu ni wenye thamani ya Sh3.01 bilioni, kwa wastani,” Bw Kabogo akasema huku wabunge wanachama wa kamati hiyo wakionekana kupigwa na mshangao.
Mbunge wa Tharaka George Gitonga Murugara aliuliza ikiwa Bw Kabogo angali anamiliki ndege aina ya helikopta.
Waziri huyo mteule alijibu kwa kukubali alimiliki chombo hicho cha usafiri angani miaka ya nyuma lakini akaiuza.
“Ndio, nilimiliki helikopta zamani nilipokuwa kijana. Nilikuwa nikiiendeshwa kwa sababu mimi ni rubani. Lakini ilifika wakati ambapo niliamua kuiuza na nikawekeza pesa hizo katika biashara zingine,” Bw Kabogo akajibu.
Mwanzoni mwa kikao hicho, Bw Kabogo ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Juja, aliiambia kamati hiyo kuwa kando na kuwa mwanasiasa, yenye ni mfanyabiashara shupavu.
Leave a Reply