Kilio tumbili wakishambulia na kujeruhi wakazi Lessos – Taifa Leo


WATU kadhaa wanauguza majeraha mabaya baada ya kushambuliwa na tumbili katika eneo la Lessos, Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.

Tumbili hatari kutoka Msitu wa Bidii wamekuwa wakiwahangaisha wakazi kwa kuwashambulia na kuwauma.Wanawake na watoto ndio walioathirika zaidi huku visa kadhaa vikiripotiwa kuhusu wahasiriwa wanaouguza majeraha kutoka kwa tumbili mwitu katika majuma machache yaliyopita.

Wahasiriwa zaidi ya 15 wamejeruhiwa huku wakazi wakihofia huenda wameambukizwa maradhi hatari.Kulingana na wakazi, tumbili hao hawashambulii wanaotembea kwa makundi bali wanalenga mtu aliye pekee yake hususan wanawake na watoto.

Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS) kwa ushirikiano na Huduma ya Msitu Nchini (KFS) imeanzisha oparesheni ya kuwatuliza tumbili hao.

Bi Elizabeth Ngotho 38, alijeruhiwa vibaya mapajani na kupelekwa kudungwa sindano ya kichaa katika hospitali ya Rufaa ya Wamalwa Kijana (WKRH], baada ya kushambuliwa na tumbili Jumatano iliyopita.

“Nilipiga mayowe nilipogeuka na kugundua tumbili amenishambulia. Mwanzoni nilidhani ni mbwa. Dada yangu alikuja kuniokoa lakini tumbili hakutoroka alisimama tu kututazama. Nilishtuka sana,” alisimulia.

Bw James Mseti, mwendeshaji bodaboda eneo hilo alisema tumbili mwitu hao wamegeuka tishio kwa wakazi, wengi wao wakilazimika kukaa ndani wakihofia kushambuliwa.“Baadhi ya watu wameshambuliwa na tumbili hawa na tunashuku sio tumbili wa kawaida.

Serikali ichukue hatua kwa sababu tunaishi kwa hofu na huenda watu wakaambukizwa ugonjwa hatari,” alisema.Katika mkutano wa hadhara huko Lessos, wakazi walisema serikali inapaswa kuwalipa fidia walioshambuliwa na kujeruhiwa na wanyamamwitu.

Wakazi na wahasiriwa walioshtuka walisema mashambilizi hayo si ya kawaida kwa sababu tumbili wamekuwepo tangu mbeleni lakini hawakuwa wakiwashambulia na wakataka tumbili hatari kutulizwa ili wapate amani.

Kufuatia malalamishi hayo, Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS) kwa ushirikiano na Huduma ya Msitu Nchini (KFS) imeanzisha oparesheni ya kuwatuliza tumbili hao.

IMETAFSIRIWA NA MARY WANGARI



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*