KENYA imebadilika kuwa nchi ya magenge ya wahuni wanaovamia kuteka na kuua wakazi na kuwafanya raia kuchukua sheria mikononi ikiwa ni pamoja na kuvamia vituo vya polisi kuadhibu washukiwa.
Wakazi wanahisi kuwa mfumo wa sheria hauwajibiki na sasa wameamua kuwa walinda usalama, waendesha mashtaka, mashahidi na mahakimu na watekelezaji wa hukumu huku wakishambulia na kuua washukiwa.
Visa vya watu kuuawa na umati vimekuwa jambo la kawaida katika maeneo mbalimbali ya nchi katika miezi ya hivi majuzi.
Katika kile ambacho kimegeuka kuwa janga la mauji, washukiwa wanavamiwa na umati wa watu na kupigwa mawe, kuchomwa moto au kupigwa kwa marungu hadi kufa.
Cha kushangaza ni kwamba baadhi ya waathiriwa huburutwa kutoka kwa vituo vya polisi na kuuawa mchana peupe.
Wengi wa waathiriwa hao wanashukiwa kufanya uhalifu kama vile wizi, mauaji, unyanyasaji wa jinsia, kupora simu za rununu na vipochi barabarani.
Kuongezeka kwa matukio haya kunaonyesha hali inayotia wasiwasi ambapo waathiriwa wanatendewa haki papo hapo bila mchakato unaostahili wa mahakama kama inavyotarajiwa kisheria.
Ingawa idara za usalama zimeonya kwamba mwelekeo huo ni hatari, jamii zinasema kuwa ndiyo njia bora ya kukabiliana na wahalifu wanaowatishia raia wasio na hatia bila huruma.
Kwa mfano, latika kisa cha hivi punde zaidi mnamo Januari 3, 2025, zaidi ya wakazi 3000 waliokasirika wa Tinderet katika Kaunti ya Nandi, walivamia Kituo cha Polisi cha Chemase, wakamtoa mshukiwa wa mauaji kabla ya kumpiga mawe hadi kufa na kisha kuchoma mwili wake.
Mtuhumiwa Victor Kimutai (30), alikuwa amezuiliwa kwa kushukiwa kuhusika na mauaji ya kikatili ya mwanamume mwenye umri wa miaka 38, ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umekatwakatwa.
Kamanda wa Polisi wa Tinderet Johnson Mwariga, alisema mshukiwa alikiri kutekeleza uhalifu huo, na hata kuwasindikiza maafisa wa uchunguzi hadi alikoripotiwa kuficha kichwa na sehemu nyingine za mwili wa mwathiriwa.
Wakazi hao walivamia na kuteketeza gari la polisi kabla ya kuwazidi nguvu askari hao na kuingia ndani ya seli ambapo walimkabili mshukiwa.
Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) Dkt Resila Onyango anaonya umma dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao.
Tunawaomba wananchi wajizuie kuchukua sheria mikononi mwao na kuruhusu sheria kuchukua hatua pindi mshukiwa anapokamatwa
“Uharibifu wa mali ya polisi kama ilivyoshuhudiwa katika Kituo cha Polisi cha Chemase wakati gari la polisi lilipoteketezwa na wananchi wenye hasira unatatiza tu ufanisi wa polisi katika kutoa huduma zinazohitajika kwa umma. Kwa mtazamo wa polisi jamii, tunawaomba wananchi kushirikiana na polisi ili kuimarisha usalama katika maeneo yetu,” aliongeza.
Afisa mkuu wa polisi, ambaye haruhusiwi kuhutubia wanahabari aliambia Taifa Leo: “Polisi wanafanya kazi ndani ya mipaka ya sheria na hatutaruhusu kuuawa kwa washukiwa kwa tuhuma kwamba wamefanya uhalifu. Ni mwelekeo hatari ambao haututaruhusu kuota mizizi nchini na tunaweka wazi hilo.”
Mwanaharakati wa Haki za Kibinadamu David Kuria ambaye ni mkurugenzi wa wa Nakuru Human Rights Network (Nahurinet) pia aliwataka wananchi kuepuka kuchukua sheria mkononi.
‘Washukiwa wote wanapaswa kufikishwa kwa polisi ili wafunguliwe mashtaka. Tuna sheria ambayo inafaa kuchukua mkondo wake, kumuua mshukiwa ni kosa la jinai kuu,’ akasema Bw Kuria.
Kulingana na Bw Kuria, matukio kama hayo yana mwelekeo hatari.
“Kunafaa kuwa na kampeni za uhamasishaji kati ya mahakama, polisi na wananchi ili kuwaelimisha kuhusu hatari watu kuungana kwa umati kuua washukiwa,” aliongeza Kuria.
Bw Kuria anaelezea hali hiyo kuwa ya wasiwasi kwamba Wakenya wamekumbatia “utamaduni wa kujichukulia sheria mkononi.”
Makumi ya Wakenya wameuawa na umati katika msururu wa visa nchini.
Mnamo Oktoba 30, 2024, ndugu wawili waliuawa viungani mwa mji wa Thika kwa tuhuma za kumpokonya mtembeaji kwa miguu simu.
Ndugu hao wawili wenye umri wa miaka 19 na 21 waliuawa umbali mfupi kutoka Kituo cha Polisi cha Makongeni.
Wakazi walioshuhudia tukio hilo walisema maafisa wawili waliokuwa wakishika doria walitoroka baada ya kutishiwa na umati huo wenye hasira.
Mnamo Oktoba 27,2024, mshukiwa kuwa mwizi wa pikipiki aliuawa mjini Eldoret huku msako mkali wa polisi dhidi ya kundi la wizi katika eneo hilo ukizidi.
Mnamo Novemba 11,2024, mshukiwa wa kupora simu aliteketezwa na umati katika mji wa Eldoret, kufuatia jaribio la wizi lililohusisha msichana
Mwanamke huyo alipaza sauti iliyovuta wapita njia.
Mnamo Julai 10,2024, wakazi waliokasirika wa kijiji cha Gachocho huko Murang’a walivamia kituo cha polisi na kuwapiga kwa mawe maafisa waliokimbia, kabla ya kumtoa mshukiwa wa mauaji kutoka seli na kumuua.
Wenyeji walisema jicho kwa jicho ndio haki pekee ya uhakika kwao kwani hawana imani na polisi eneo hilo.
Maafisa hao walikimbia kuokoa maisha yao, wakazi walipovamia seli za polisi, wakamtoa mshukiwa na kumpiga mawe hadi kufa.
Mnamo Julai 11, 2024, watu watatu waliuawa kwa kupigwa mawe na kundi la watu katika kisa kinachoshukiwa cha utekaji nyara katika kijiji cha Butere, Kaunti ya Kakamega.
Mnamo Mei 28, 2024, umati wenye hasira huko Nyakach, Kaunti ya Kisumu, uliua mwanamume mmoja baada ya mtoto wake wa miaka 18 kumwita mchawi.
Valentine Ochieng, aliuawa na umati wenye hasira uliovamia nyumba yake.
Umati huo wenye hasira uliteketeza nyumba nne katika boma la mshukiwa.
Mnamo Machi 20,2024, polisi walianzisha uchunguzi kuhusu kifo cha wanafunzi wawili wa shule ya upili, ambao walikuwa miongoni mwa washukiwa watatu wa ujambazi walioteketezwa hadi kufa Kisumu kwa madai ya wizi wa pikipiki.
Waendeshaji bodaboda waliwabana watatu hao katika mtaa wa Manyatta huko Kisumu ambapo umati wa watu uliwavamia.
Mnamo Machi 9 na 10,2024, watu watatu waliuawa kwa kuchomwa moto ndani ya siku mbili, ndani ya Bahati, Nakuru.
Washukiwa wawili wa awali walichomwa katika eneo la Kiamunyeki, huku wa tatu akiteketezwa kiasi cha kutotambulika kando ya barabara ya Nakuru-Subukia katika wadi ya Kiamaina.
Hii ni mifano tu ya matukio ya kuongezeka kwa visa hivi miezi michache iliyopita.
Hata hivyo, wanasheria wanaonya kwamba hali hii ni hatari na ina gharama kubwa kwa kuwa wahusika wanaweza kushtakiwa kwa mauaji, kosa ambalo adhabu yake ni kifo au kifungo cha maisha,
“Ingawa inahitaji kiwango cha juu zaidi cha ushahidi, kwa sababu upande wa mashtaka lazima uthibitishe kesi yao bila shaka yoyote, unaweza kumpeleka mtu jela maisha yake yote,” alifichua wakili Steve Kabita.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply