Kabogo ajitenga na ulanguzi wa mihadarati, asema ‘amegusa panadol pekee’ – Taifa Leo


WAZIRI Mteule wa ICT na Uchumi wa Dijitali William Kabogo Jumanne, Januari 14, 2025, alijitenga na ulanguzi wa mihadarati akieleza kuwa hajawahi kugusa aina zozote za dawa hizo za kulevya.

Alikuwa ajibu swali kutoka kwa Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed aliyetaka kujua ikiwa ni kweli kwamba yeye ni mlanguzi wa mihadarati ilivyoelezwa kwenye ripoti iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Waziri marehemu George Saitoti.

Bw Kabogo alisisitiza kuwa uchunguzi ulioendeshwa na asasi za usalama, ambao matokeo yake yaliwasilishwa bungeni, haukumhusha na uovu huo.

“Asasi za usalama, ikiwemo polisi, ziliendesha uchunguzi wa kina na baadaye zikaandaa ripoti. Ripoti hiyo, iliyowasilishwa katika bunge hili, haikunitaja. Kwa hivyo, sijawahi kuhusika na dawa zozote maishani mwangu,” Bw Kabogo akasisitiza alipokuwa alipigwa msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi.

Ndipo Spika Moses Wetang’ula akauliza kwa mzaha ikiwa Bw Kabogo hajawahi kugusa dawa kama vile “Panadol” ya kupunguza maumivu.

“Sidhani ikiwa Junet alikuwa akirejelea Panadol, alikuwa akizungumzia dawa za kulevya kama kokeni. Ikiwa ni Panadol, basi ninazo tembe kadhaa mfukoni mwangu sasa hivi,” Gavana huyo wa zamani wa Kiambu akaeleza huku wanachama wa kamati hiyo wakiangua kicheko.

Bw Kabogo alisema kuwa madai hayo yamemharibia sifa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyombo vya habari viliyachukulia kama ya kweli.

“Nilishtaki vyombo kama hivyo kwa kuniharibia jina na nikalipwa kiwango fulani cha pesa” akasema.

Bw Kabogo pia alifichua kutokana na madai hayo baadhi ya Wakenya walimnasibisha na kiongozi wa genge la walanguzi wa mihadarati nchini Colombia, Medellin, Pablo Emilio Escabar Gaviria.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*