Muturi awasha moto kwa kuanika wanaohusika na utekaji nyara nchini – Taifa Leo


UFICHUZI  wa Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi kwamba, mwanawe alitekwa nyara na maafisa wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) umewasha moto, viongozi na mashirika ya kutetea haki za binadamu yakitaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Noordin Haji ajiuzulu.

Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka amelaumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kusimamia utekaji nyara nchini na kumtaka Rais Ruto kuchukua hatua au ajiuzulu.

Viongozi wanaounga serikali nao wamemlaumu Bw Muturi na kumtaka ajiuzulu. Mnamo Jumanne, Bw Muturi alidai kuwa Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Noordin Haji, ndiyo iliyohusika na utekaji nyara wa Wakenya.

Alifichua haya alipoandikisha taarifa katika Kituo cha Polisi cha Kilimani Jumanne, Januari 14. Muturi alikuwa amekashifu serikali kuhusu kutekwa nyara kwa mwanawe.

Katika taarifa yake, Muturi alifichua kwamba, alilazimika kukutana binafsi na Rais William Ruto kufahamu alikokuwa mwanawe, Leslie Muturi. Hii ilifuatia kufeli kwa juhudi zake za kuwasiliana na aliyekuwa Inspekta Jenerali Japhet Koome, Waziri wa zamani wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki, Katibu wa Usalama wa Ndani Raymond Omollo, na mkurugenzi wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) Kiprotich Mohamed, ambazo hazikufua dafu.

 

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka

Bw Musyoka alisema ufichuzi wa Bw Muturi umeanika wahusika wa utekaji nyara.

“Ufichuzi wa Waziri Muturi kuhusu kiongozi wa utekaji nyara ni wa kufurahisha sana. Ikiwa Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Kenya hawezi kupata majibu kuhusu aliko mwanawe, nani anaweza? Ikiwa simu za Mwanasheria Mkuu haziwezi kupokewa na wafanyakazi wa chini kama vile Mkurugenzi wa NIS na Mkurugenzi wa DCI, nani anaweza? Iwapo aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Ndani wa wakati huo Prof Kithure Kindiki na Katibu Raymond Omollo waliambiwa uongo na wadogo wao, je serikali ya Kenya Kwanza iko katika hali gani?’ Bw Musyoka alihoji jana.

Alisema taarifa ya Muturi iliyotiwa saini kwa uwazi ilielekeza lawama kwa “mhalifu” mkuu wa utekaji nyara.

“Mtu aliyetania, aliyepuuza utekaji nyara na maandamano ya Gen Z; mwanamume aliyepiga simu moja kutoka Ikulu ya Nairobi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji na kufanya Leslie Muturi kuchiliwa ndani ya saa moja. Huyo mtu tumeeleza hapo awali ni William Samoei Ruto,” Bw Musyoka alisema.

Jana, kundi la watetezi wa haki za kibinadamu la Justice Alliance, lilimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji kujiuzulu kutokana na visa vya utekaji nyara na kutoweka kwa watu nchini.

Kundi hilo, kupitia kwa mratibu wake, Kennedy Omulo, lilisema inasikitisha NIS ilihusika na kutekwa nyara kwa Leslie Muturi, inavyodaiwa na babake mwathiriwa, ambaye ni Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi.

Shirika hilo lililaumu NIS kwa kuwateka nyara watu ilhali jukumu la kulinda maisha ya Wakenya na kuwakamata inapobidi ni la Huduma ya Kitaifa ya Polisi.

“Kufuatia ufichuzi wa Bw Muturi, sasa tunajua ni nani na shirika gani la serikali limekuwa likiwateka nyara vijana wetu. Kwa hivyo, tunatoa wito wa kujiuzulu mara moja kwa Mkurugenzi Mkuu wa NIS, Noordin Haji na kuomba mamlaka husika kumchunguza na kubaini ni jukumu gani alitekeleza katika visa vya utekaji nyara,” Omulo alisema.

 

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi. PICHA| MAKTABA

Naye Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, jana alimkashifu Bw Muturi baada ya kufichua aliyehusika na utekaji nyara nchini. Katika taarifa, Sudi alimsuta Bw Muturi, akimshutumu kwa kulenga kutimiza maslahi ya kisiasa.

“Hatua hii ilichukuliwa sasa kwa kuwa taaluma yako ya kisiasa imefifia, ni jaribio la wazi la vitisho” Sudi alisema. Sudi, pia alitilia shaka kutekwa nyara kwa mwanawe Muturi wakati wa maandamano ya Juni-Agosti yaliyoongozwa na Gen Z akidai kuwa ni ‘mzee’.

“Kuhusu masaibu ya mwanao wa rika langu kwani alishikwa bure?” Sudi aliuliza. Kauli za Sudi zinajiri siku mmoja baada ya wabunge wawili wa Muungano wa Kenya Kwanza kumtaka Bw Muturi kujiuzulu. Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro na mwenzake wa Aldai Bi Marianne Kitany walimwambia Bw Muturi ajiuzulu la sivyo afutwe kazi.

Bw Osoro alimkashifu Bw Muturi kwa mashambulizi yake makali dhidi ya utawala wa Rais William Ruto, akisema kufanya hivyo ni kama kutikisa meli akiwa ndani. Mbunge huyo alimpa Bw Muturi chaguo la kuomba msamaha ikiwa anataka aendelee kuhudumu katika utawala wa Kenya Kwanza la sivyo, watamshughulikia sawia na walivyomfanyia aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

 

Rais William Ruto akizungumza awali. Picha|Maktaba

“Wewe ni waziri. Unaketi katika baraza la mawaziri. Unaketi na rais kila siku, unaongea na polisi kila siku, unaita mkutano wa wanahabari kulia kuhusu polisi. Justin Muturi unajua sheria. Ulikuwa spika. Leo mimi nakwambia, mbele ya hawa watu wangu. Ile kiboko tulipiga Gachagua, ndio inakuja kwako. Ujiuzulu ama tukutoe,” alisema Bw Osoro.

Bi Kitany, alitishia kuwasilisha hoja ya kumsuta Bw Muturi kufuatia matamshi yake ya kukosa serikali kuhusu visa vya utekaji nyara nchini.Bi Kitany pia alimtaka Bw Muturi ajiuzulu, akimlaumu kwa kukosoa serikali ambayo anahudumia.

“Waziri Justin Muturi anafaa kujiuzulu. Hawezi kuikosoa serikali ambayo yeye ni sehemu yake; haiwezekani. Ikiwa hatajiuzulu, nitafadhili hoja ya kumsuta bungeni,” Bi Kitany alisema.

Lakini akizungumza jana baada ya kuandikisha taarifa kuhusu kisa cha kutekwa kwa mwanawe mwaka jana, Bw Muturi alisema haogopi kufutwa huku akisisitiza hapingi serikali. “Ni rahisi sana kufutwa kazi kama waziri na nilifahamu hayo nilipokubali kazi hii,” alisema Bw Muturi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*