MAJIRA ya asubuhi mnamo Januari 8 mwaka huu, 2025, Simon Mwangi Githinji, mkazi wa kijiji cha Kinyaiti, Kaunti ya Nyeri aliondoka kwenda kusaka riziki.
Bw Mwangi, 55, mhudumu wa bodaboda, alimwahidi bintiye kwamba angerejea baada ya saa moja ili ampeleke shuleni.
Lakini akiwa umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani, akiokota kuni karibu na Ranchi ya Solio, alisimamishwa na wanaume wanne wenye mavazi ya kiraia na waliojihami kwa marungu.
“Walidai wao ni maafisa wa usalama wanaoshika doria katika ranchi na wananishutumu kwa kuingia humo bila idhini. Niliwaambia kuwa sikuwa nimeingia humo bali nilitumia njia inayotumiwa kila siku na wakazi. Lakini hawakusikia maelezo yangu,” akasema.
Bw Mwangi alishangaa wanaume hao walipomwagiza aandamane nao hadi afisini ambako usimamizi ungesikiza kesi yake.
Mwanabodaboda huyo alikubali, bila kufahamu madhila ambayo yalimsubiri.
Baada ya kutembea umbali wa mita chache, wanaume hao walimweka pingu, wakatwaa simu yake na kuchukua Sh13, 000 zilizokuwa mfukoni mwake, pesa alizotenga kulipa karo ya bintiye.
Bw Mwangi alipohoji vitendo vyao, walijibu kwa kumcharaza.
“Walianza kunipiga wakinuburuta hadi ndani ya msitu ambapo walifunga mikono na miguu yangu kwenye mti,” akasema, akiongeza kuwa walimvua jaketi, na gambuti.
Bw Mwangi alisema alikaa msituni kwa siku mbili kwenye baridi na bila chakula.
“Waliziba mdomo wangu kwa kitambaa ili nisipige mayowe. Nyakati za usiku ningewasikia fisi wakinguruma na kucheza karibu, hali iliyoniogofya zaidi. Niliomba Mungu anusuru maisha yangu kwani baadhi ya fisi walipita karibu zaidi na mahala nilipokuwa,” akaeleza.
Mkewe Bw Mwangi, Irene Mwangi, alieleza walivyomsubiri arejee ili ampeleke binti yao shuleni.
Lakini kufikia saa sita adhuhuri mumewe hakuwa amerejea.
“Niliendelea kumpigia simu kila mara. Mwanzoni, hakujibu lakini baadaye simu yake ilizima,” Bi Mwangi anasema.
Januari 9, familia ya Mwangi iligundua kuwa pikipiki yake ilitelekezwa katika shamba moja lililoko umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwao, lakini karibu na ranchi hiyo.
Hapo ndipo wanakijiji walianza kumsaka na wakapiga ripoti katika kituo cha Polisi cha Kanyagai.
Hata hivyo, walilamika kuwa polisi walikuwa wakijivuta kuchukua hatua.
“Tulipiga ripoti kuhusu suala hilo mwendo wa saa nne za asubuhi Alhamisi lakini kufikia saa kumi jioni hawakuwa wamechukua hatua yoyote,” Bi Irene akaeleza.
Lakini jioni hiyo wanakijiji walipata simu ya Mwangi eneo fulani katika ranchi hiyo. Ajabu ni kwamba haikuwa na unyevunyevu ilhali mvua ilikuwa imenyesha sehemu hiyo siku iliyotangulia.
Kupatikana kwa simu ya Bw Mwangi, kuliwafanya wakazi kuamini kuwa wafanyakazi wa ranchi hiyo ndio waliohusika na kutoweka kwake.
Wakazi walipandwa na hasira na kupelekea wao kuamua kufanya maandamano Ijumaa, Januari 10.
Waliziba barabara ya Nyeri- Nyahururu kwa zaidi ya saa tano, wakitaka majibu kuhusu kutoweka kwa Mwangi.
Hatimaye Mwangi aliachiliwa siku hiyo mwendo wa saa kumi na moja jioni na akakimbizwa hospitalini mara moja kwa matibabu.
“Tangu aliporejea nyumbani maisha hayajakuwa sawa,” Irene akasema
“Ni vigumu kwake kulala kwa utulivu. Bado haamini kuwa aliponea. Isitoshe, binti yetu mwenye umri wa miaka 15 hajarejea shuleni kwani wahuni hao walitwaa karo.
Wakazi walisema uhusiano kati yao na walinzi wa Ranchi ya Solio haujakuwa mzuri kutokana na visa vya wenzao kuhangaishwa na walinzi wa hifadhi hiyo.
Leave a Reply