Wakenya wengi wamekata tamaa ya kumiliki nyumba, ripoti yasema – Taifa Leo


WAKENYA sita kati ya kumi ambao wangependa kumiliki nyumba hawana mpango wowote wa kutimiza ndoto hiyo, ripoti mpya inayoonyesha jinsi hali ngumu ya kiuchumi imewaacha wengi bila matumaini imefichua.

Ripoti hiyo kuhusu hali ya makazi miongoni mwa Wakenya inaonyesha kuwa kati ya wananchi wasiomiliki nyumba na ambao kwa sasa ni wapangaji japo wangependa kumiliki makazi yao wenyewe, asilimia 62.6 hawana mpango wowote.

Hii ni kumaanisha kuwa japo wangependa kuishi katika nyumba wanazomiliki, hakuna lolote wanalofanya ili kuafikia ndoto hiyo, ufunuo huu ukitolewa wakati Wakenya wengi wamekua wakingangana na hali ngumu ya maisha na kuishia kumudu mahitaji ya kila siku pekee.

“Asilimia 62.6 ya wapangaji waliotaka kumiliki nyumba hawakua wameweka mipango kuhusu umiliki wa nyumba. Hata hivyo, asilimia 11.2 walikuwa wakiweka akiba kwa lengo la kujenga nyumba, huku asilimia 10.7 wakiweka akiba kununua ardhi,” ripoti ya Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) kuhusu hali ya makazi nchini inasema.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa asilimia 5.9 ya wapangaji wengine wenye azma ya kumiliki nyumba tayari wamenunua ardhi, asilimia 4.3 wanaweka akiba kununua nyumba, asilimia 2.5 wanaendelea na ujenzi na asilimia tu wanachukua mikopo ya ujenzi.

KNBS inasema kuwa takwimu zake zinaonyesha kuwa umiliki wa nyumba nchini uko juu katika  maeneo ya mashambani (asilimia 85.5) ikilinganishwa na mijini ambapo asilimia 22.8 ya familia zinamiliki nyumba.

“Idadi ya familia zinazomiliki nyumba iko juu Isiolo (asilimia 98), Marsabit (asilimia 97.5), na Baringo (asilimia 96.9), lakini katika maeneo ya miji umiliki wanyumba ulikua juu zaidi Wajir ambapo asilimia 87 ya familia zinamiliki,” KNBS ikasema.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa miongoni mwa Wakenya wanaomiliki nyumba kwa sasa nchini, zaidi ya nusu (asilimia 52.8) walizijenga kwa mpigo mmoja ilhali asilimia 27 walizijenga hatua kwa hatua huku wakichukua mapumziko.

Asilimia 13.2 waliridhi nyumba wanamoishi, asilimia 4.2 walipewa kama zawadi na asilimia 2.5 walinunua nyumba.

“Kitaifa, asilimia 91.4 ya umiliki wa nyumba zilifadhiliwa na pesa taslimu ama akiba na asilimia 5.5 kwa mikopo,” ripoti hiyo ikasema.

Na japo serikali imekuwa ikiendeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ikilenga kujenga nyumba 200,000 kila mwaka ili kuzidisha idadi ya Wakenya wanaomiliki nyumba, ripoti hiyo inaonyesha kuwa takriban Wakenya milioni 13 hawana habari kuhusu mpango huo.

Kati ya Wakenya milioni 28 ambao KNBS ilihoji kuhusu ikiwa wanafahamu kuhusu mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, asilimia 53.5 walisema kuwa wanafahamu ila asilimia 46.4 walisema hawafahamu.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*