MNAMO 2023, mbunge wa Mathira Eric Wamumbi alizindua mpango ambao ulipaswa kutoa karo kwa shule zote za upili za kutwa katika eneo bunge hilo.
Iwapo mpango huo ungefaulu, kila mmoja wa wanafunzi 14,000 katika shule 30 angelipa Sh1,000 badala ya Sh7,000 zinazolipwa kwa muhula.Awali, mpango huo ulitengewa Sh30 milioni ambazo zilipaswa kuongezwa baadaye.
Hata hivyo, mpango huo ulitibuka huku wakuu wa shule wakisema bado hawajapokea hata shilingi moja kutoka kwa mpango huo uliopigiwa debe. Baadhi ya shule zilikuwa zimeruhusu wanafunzi kuendelea na masomo kwa matumaini kwamba pesa hizo zingelipwa ilivyoahidiwa.
Lakini zaidi ya mwaka mmoja, hakuna hata shilingi moja iliyoingia kwenye akaunti za benki za shule.Wakuu wa shule waliozungumza na Taifa Leo kwa sharti la kutotajwa majina yao kwa kuhofia kudhulumiwa, walisema taasisi hizo zimekuwa zikihangaika kuwahudumia wanafunzi na sasa wamekata tamaa.
“Wanafunzi wana hadi mwisho wa wiki hii kulipa malimbikizo yote ya karo ya Sh21,000 kwa kila mwanafunzi la sivyo watarudishwa nyumbani,” alisema mkuu mmoja wa shule.Wakuu hao hata hivyo walisema baadhi ya wazazi walilipa karo baada ya mpango huo kufeli.
“Kati ya wanafunzi 14,000, wanafunzi wasiopungua 7,000 wanadaiwa Sh21,000 kila mmoja,” alisema mwalimu mwingine.Wazazi sasa wanamshutumu mbunge huyo kwa kutotimiza ahadi yake baada ya shule kuanza kutoa notisi za kuwarudisha watoto wao nyumbani kutokana na malimbikizo ya karo.
Bw Wamumbi kwa upande wake anadai kiasi cha Sh30 milioni ambazo zilikusudiwa kufadhili mpango huo ‘zilielekezwa’ kwa miradi mingine na maafisa wa NG-CDF eneo hilo, akiongeza kuwa afisi yake iko katika harakati za kutenga pesa katika bajeti ya 2025-2026 kuhakikisha mpango huo unaofahamika kama ‘Masomo kwa wote’ unafanikiwa.
Sherehe ya uzinduzi mnamo Agosti 2023, iliadhimishwa kwa shangwe katika uwanja wa Karatina na ilihudhuriwa na mamia ya wanafunzi na wazazi na kupambwa na wanamuziki kadhaa.Wanafunzi katika shule za kutwa na za bweni walipangwa kunufaika na mpango huo.
Aidha, ilitangazwa kuwa ungeshughulikia chakula kwa shule za eneo bunge hilo ambapo wanafunzi wangepata githeri kwa siku tatu za githeri na mchele kwa siku tatu .
Pia katika programu ilikuwa kuanzishwa kwa mlo siku za Jumamosi kwa wanafunzi wote.Mlo huo, kulingana na mbunge huyo, ungejumuisha chai au uji saa nne asubuhi na chakula cha mchana kama njia ya kuboresha masomo.
Akiongea na Taifa Leo Jumatano, Bw Wamumbi’ hata hivyo alisema mpango huo ulikabiliwa na changamoto kadhaa baada ya baadhi ya maafisa wa NG-CDF kuelekeza pesa hizo kwa miradi mingine bila mamlaka yake, na kuongeza kuwa maafisa hao wamesimamishwa kazi.
“Nawahakikishia wazazi kuwa mpango bado utaendelea na tunatenga pesa mwaka huu wa kifedha,” alisema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply