WANAUME wakongwe ambao hunywa sharubati ya zabibu (grape juice) wanapunguza uwezekano wa kuandamwa na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume, Utafiti umebaini.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Tianjin, Kaskazini mwa China, walisema kuwa wanaume ambao walikunywa sharubati ya zabibu mara tano kwa siku au hata zaidi kwa wiki, walipunguza tatizo la kukosa hamu wakati wa tendo la ndoa.
Wanaume 300 wenye tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume walihusishwa na wengine 300 ambao wako sawa. Ilibainika kuwa wale waliokunywa sharubati ya zabibu kwa zaidi ya mara tano waliimarisha uweledi wao wa kusakata ngoma chumbani kuliko jinsi ambavyo walikuwa hapo awali.
Ukosefu wa nguvu za kiume ni tatizo ambalo huwakumba sana wanaume wazee hasa wenye umri wa miaka 60 na zaidi.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Kenya, asilimia 95 za wanaougua ugonjwa wa moyo huwa wana tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.
“Sharubati ya zabibu haina kemikali hatari na ina madini ambayo yana manufaa kiafya. Ile ya zabibu nyekundu ni nzuri zaidi kwa sababu ina kemikali ambazo zinazuia seli muhimu kuharibiwa,” utafiti huo ulioendeshwa na kikosi cha wataalamu na watafiti wakiongozwa na Liwei Wua ulieleza.
Watafiti hao pia walichunguza umuhimu wa sharubati ya nyanya, matunda, machungwa, limau na paipai lakini ile ya zabibu ndiyo ilipatikana kuwa na manufaa kwa waliopungukiwa na hamu ya kufanya mapenzi.
Aidha watafiti pia walichunguza maziwa na aina mbalimbali za soda lakini bado wakapata sharubati ya zabibu ndiyo huwasaidia wanaume kuongeza ashiki.
Wakati wa utafiti huo, ilipatikana sharubati nyekundu ya zabibu pia husaidia kuepesha magonjwa ya moyo kwa kuimarisha usambazaji wa damu mwilini kwa kuzuia mishipa kuzibwa kwa mafuta.
Leave a Reply