Kipchoge, 40, tayari kurejea kwa kishindo London Marathon mwezi Aprili – Taifa Leo


BINGWA mara nne wa mbio za London Marathon mwaka 2015, 2016, 2018 na 2019 Eliud Kipchoge, ameingia makala ya 45 yatakayofanyika Aprili 27.

Kipchoge aliyesherehekea kutinga umri wa miaka 40 hapo Novemba 5, 2024 ni binadamu wa pekee kuwahi kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili, baada ya kuandikisha 1:59:40 katika mbio maalum za INEOS1:59 Challenge jijini Vienna, Austria, mnamo Oktoba 2019.

Mara ya mwisho Kipchoge alishiriki London Marathon ilikuwa mwaka 2020 wakati alisema kufunga kwa sikio lake la kulia kulichangia matokeo mabovu siku hiyo baada ya kukamata nafasi ya nane.

Kipchoge akata utepe kushinda London Marathon jijini London, Uingereza, mnamo Aprili 28, 2019. Atarejea jijini London kwa marathon yake ya kwanza mwaka huu. PICHA | AFP

Wengi wanaamini Kipchoge ndiye mtimkaji mwenye mafanikio makubwa katika historia ya marathon – maarufu kama Greatest Of All Time (G.O.A.T) kwa Kimombo.

Bingwa huyo anajivunia kushinda mataji ya Olimpiki mwaka 2016 jijini Rio de Janeiro, Brazil, na 2021 nchini Japan. Pia ametwaa mataji 11 kwenye Marathon Kuu Duniani (WMM).

Kipchoge ametawala Berlin Marathon mara tano ikiwemo kuweka rekodi mbili za dunia za 42km (saa 2:01:39 mnamo Septemba 2018 na 2:01:09 mnamo Septemba 2022) kwenye mbio hizo za Ujerumani. Pia amezoa mataji ya Chicago Marathon na Tokyo Marathon.

“Nafurahi kuwatangazia kuwa mbio zangu zijazo zitakuwa London Marathon. Ni mbio zilizo na mvuto wa kipekee moyoni mwangu, zilizojaa kumbukumbu nzuri. Ninasubiri kwa hamu kuweka historia hata zaidi,” akasema Kipchoge.

Kipchoge asherehekea baada ya kushinda Berlin Marathon jijini Berlin, Ujerumani, mnamo Septemba 25, 2022. Ni hapa alipoweka rekodi nyingine ya dunia ya saa 2:01:09, ambayo ilifutwa na marehemu Kelvin Kiptum mwaka uliofuata jijini Chicago, Amerika. PICHA | AFP

Amewataka maelfu ya washiriki wanaojitokeza wakati wa mbio hizo kufurahia ukimbiaji.

“Ni heshima kubwa kushirikiana katika safari hii na kila mtu ili kupata matokeo mazuri kabisa,” akaongeza Kipchoge anayeamini amepumzika ya kutosha tangu alipojiuzulu kabla kukamilisha marathon kwenye Michezo ya Olimpiki jiini Paris, Ufaransa, mnamo Agosti 2024.

“Baada ya mapumziko nimerejea mazoezini nikiwa mwenye nguvu mpya na malengo thabiti. Nahisi niko shwari kabisa kuonyesha tena ubabe jijini London,” alieleza Kipchoge.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*