NDOA ina pandashuka nyingi ikiwemo kipindi cha wachumba kukosa kuchangamkiana kama siku za mwanzo za uhusiano wao.
Hii inafanyika kwa wanaochukulia ndoa kama kitu cha kawaida.
Wanaohisi kwamba baada ya kufunga pingu za maisha, wana haki ya kumiliki wachumba wao.
Hisia hizi ziko mbali sana na ukweli wa mambo kwa kuwa zinachozaa ni watu kuchoshwa na uhusiano wao.Ndoa ni kama mti, unapopandwa, unafaa kupapaliwa, kuwekwa mbolea na kunyunyuziwa maji kila wakati ili uweze kunawiri na kuchanua maua yenye harufu ya kuvutia.
“Usipotunzwa vyema, mti hauwezi kuchanua maua yenye afya na hauwezi kuzaa matunda mema ya kufurahia. Ndivyo ilivyo kwa ndoa, lazima itunzwe kila wakati ili iweze kunawiri,” asema mtaalamu wa masuala ya ndoa Jane Muthoni.
Hivyo basi, asema, ndoa ikikosa kupaliliwa na wahusika huwa inachokesha. Hii inahitaji wachumba kuwa wabunifu sana kwa kila hali. Mume asiwe mtu katili na mdhalimu wa mchumba wake. Watu huwa wanachoshwa na tabia ya kugombezwa na kulaumiwa kila wakati na wachumba wao.
“Watu wanaojua kupalilia ndoa huwa hawagombezi wachumba wao, huwa wanawapa mwelekeo. Hakuna asiyechoshwa na mchumba anayemtusi na kumlaumu kwa kila kitu kibaya kinachotendeka katika uhusiano wao,” aeleza Muthoni.
Lakini mtu hawezi kuchoshwa na mchumba anayemnyenyekea, kumjali na kumkosoa kwa hekima akidumisha heshima kwake. Kuepuka kuchokana kunahitaji mke anayejua kumtunza na kumhudumia mumewe.
Wanaume hupagawishwa na mambo madogo sana kama vile kumvua koti na kumkumbatia akitoka kazini. Mwanamume hawezi kuchoshwa na mke anayemuomba ushauri na ruhusa ya kwenda kuhudhuria mkutano wa chama.
Ajabu ni kuwa wanawake wengi huwa wanaacha mambo kama hayo wakidai wamemea mizizi katika ndoa na wao ni wenye hisa sawa na waume wao katika ndoa.
Wachumba wanaoheshimiana hawawezi kutuhumiana na kuchokana. Wanajua kuwa tuhuma ni sumu kwa mapenzi na huzaa vurugu. Kuna akina dada ambao wakiingia kwa ndoa huwa wanageuka kuwa simba marara, kiasi cha kuwapokonya waume wao nafasi yao katika ndoa.
Vile vile, kuna wanaume wanaogeuka kuwa katili katika ndoa zao ilhali walikuwa wenye mioyo safi na maneno matamu walipokuwa wakitafuta warembo wa kuoa.Watu wanaofanya hivi huwa wanajiweka katika hatari ya kuchokwa na wachumba wao.
Wanaume wengi, na kuna ushahidi wa kutosha, wamegeukia ulevi wa kupindukia kutokana na mfadhaiko wanaosababishiwa na wake wao.Ili kuepuka kuchokana, wachumba wanafaa kuomba pamoja, kuepuka kurushiana lawama au kulazimisha mambo.
“Lawana zinachosha, hazijengi na mara nyingi chanzo chake huwa ni mambo yanayoweza kutatuliwa kila mmoja akitambua nafasi yake katika uhusiano wa kimapenzi na kujitahidi kuuboresha zaidi,” aeleza Muthoni.
Leave a Reply