ILIKUWA kisa cha kushangaza na kustaajabisha Januari 16, 2024 jioni katika uwanja wa Jevanjee jijini Nairobi watu zaidi ya 1000 waking’ang’ania chakula cha msaada.
Kile ambacho ungeona ni vumvi huku ‘wenye nguvu’ wakipambana wenyewe kwa wenyewe angalau wapate ‘riziki’ yao ya siku.
Pindi tu Rais wa Bunge la Mwananchi Francis Awino aliposema kuwa, “sasa ni wakati wa kugawa bidhaa hizi,” wale ambao walijiona ‘wadhaifu’ walianza kutoka mmoja baada ya mwingine wenye nguvu wakiachiwa uwanja.
Wengi waliumia wengine wakibaki wakipigania baadhi ya bidhaa hizo.
Hata Bw Awino mwenyewe alilazimika kukimbilia usalama wake kwani ‘wangepita naye’.
Baadhi ya bidhaa hizo ni sukari kilo mbili, unga wa ugali na wa chapati kilo mbili mtawaliwa na mafuta ya kupikia lita tatu.
Baada ya sekunde moja tu, uwanja ulikuwa safi.
Kile ambacho ungeona ni unga wa ugali uliotapakaa kila mahali huku watoto wa mitaani wakiuzoa unga uliomwagwa na waliokuwa wakipigana.
“Mwenye nguvu mpishe. Hapa kama huna nguvu hutatoboa. Unaona mimi nimejinyakulia,” akasema mwanaume mmoja huku akikimbia na sukari na mafuta ya kupikia.
Kabla ya bidhaa hizo kuanza kusambazwa, rais Bw Awino alisema walizungumza na gavana wa Nairobi Johnson Sakaja mnamo Desemba 21, 2024 ambaye alikubali kuwapa bidhaa hizo kama njia ya kuwasaidia wanachama 500.
Bw Awino pia alimshukuru Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja, kwa kuunga mkono juhudi hiyo.
“Tunamshukuru sana gavana wetu mpendwa, ambaye alijitolea ili nasi tupate kitu hii Jnauari,” alisema Bw Awino.
“Tunafahamu kuwa hali ya kiuchumi ni ngumu, na ndiyo maana kupitia gavana wetu tumeamua kugawa msaada huu wa chakula kwa wanachama wetu. Ni njia yetu ya kuwasaidia kukabiliana na changamoto za kiuchumi za sasa,” alisema Bw Awino.
Haya yanajiri huku bei ya sukari ikitarajiwa kupanda hivi karibuni jambo ambalo pia litafanya gharama ya maisha kupanda zaidi.
Kando na hayo, Bw Awino pia alithibitisha tena dhamira yake ya kuhakikisha serikali inawajibika hadi itakapotimiza ahadi zake kwa wananchi.
Hata hivyo, Francis Awino alielezea kutoridhishwa na serikali ya sasa akibainisha kuwa Bunge la Mwananchi litajitwika jukumu la kuwa sauti ya upinzani.
“Hatufurahishwi na jinsi serikali imetekeleza majukumu yake hadi sasa, na tuko tayari kuchukua nafasi ya kuwa ‘chama’ rasmi cha upinzani ili kuhakikisha masuala ya wananchi yanasikilizwa na kushughulikiwa,” alisema Awino.
Leave a Reply