GAVANA wa Siaya, Bw James Orengo na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wanaweza kufasiriwa kama maajenti wa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua iwapo wataendelea kukashifu uhusiano wa ODM na serikali.
Viongozi hao wawili walionekana kutilia shaka uhusiano wa ODM na utawala wa Kenya Kwanza mbele ya kinara wa chama hicho Raila Odinga wikendi.
Bw Sifuna amekuwa akipinga utawala wa Rais William Ruto na hata kuwashutumu viongozi wa ODM wanaoshirikiana na serikali.
Kiongozi huyo amekuwa katika idhaa moja mara kwa mara ambapo amewahi kunukuliwa akisema Rais Ruto atakuwa kiongozi wa muhula moja.
Wikendi Seneta Sifuna alikemea utawala wa Rais Ruto kwa mara nyingine huku akifanyia stihizai hatua ya ODM kushirikiana na serikali mbele ya Bw Odinga.
Alisema baadhi ya viongozi wa ODM sasa ni vibaraka wa serikali na wamekuwa wakimshutumu wakati ambapo anakosoa ushirikiano huo.
Gavana Orengo naye alisema lazima ODM ilinde utambulisho wake wala haiwezi kufanya hivyo iwapo haikashifu ukiukaji wa sheria ambao unaendelea katika serikali hii.
Kiongozi huyo amekuwa akionyesha vuguvugu akiunga na wakati mwingine kupinga uwepo wa ODM serikalini.
Mwanzo, ni ukweli kuwa utawala wa Rais Ruto una ila zake na inakabiliwa na changamoto tele lakini Mabw Orengo na Sifuna hawafai kudhibiti ODM katika ushirikiano wake na serikali.
Lazima ieleweke kuwa ODM haikuumbiwa upinzani hata kama ilishindwa kwenye uchaguzi wa 2022.
Wakazi wa Nyanza, Pwani, Magharibi mwa Kenya pia wanahitaji miradi ya maendeleo kama tu maeneo mengine yaliyochagua serikali hii.
Haya maendeleo watayapata kupitia ushirikiano na serikali badala ya kupiga siasa za upinzani miaka nenda miaka rudi.
Kwa nini Bw Orengo na Sifuna wanawashwa na kuwataka walioidhinishwa na Raila kuwa mawaziri au hata wasishabikie serikali?
Bw Odinga mwenyewe amenukuliwa mara kadhaa akisema aliwapa ruhusa viongozi wa ODM wateuliwe serikalini.
Mabw Orengo na Sifuna hawana ushawishi wowote wa maana kuliko Bw Odinga na hawana mamlaka ya kujaribu kulemaza ushirikiano na serikali ambao uliidhinishwa na Raila mwenyewe.
Kile ambacho viongozi hawa wanastahili kulalamikia, ni iwapo mawaziri wa ODM hawatimizi hitaji la raia na wamezembea serikalini.
Shinikizo za Mabw Sifuna na Orengo zinastahili kuelekezwa katika kufuatilia utendakazi wa mawaziri wa ODM badala ya kuwapiga vita na kupandisha joto la kisiasa.
Iwapo wataendelea kushutumu ODM na serikali basi wanaweza kufasiriwa kuwa wao ni maajenti wa Bw Gachagua ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali tangu abanduliwe madarakani.
Bw Sifuna anaonekana kuwa na chuki zaidi na serikali hasa Rais Ruto, lakini anastahili kufahamu kuwa siasa haina uadui wa milele.
Asipochunga huenda baadhi ya wandani wa Raila wakaanza kumpiga vita na kumwondoa kama katibu mkuu wa ODM.
Bila Raila na ODM, Sifuna si chochote si lolote katika siasa za Nairobi na anastahili kuenda polepole asijipate akitimuliwa jinsi Ababu Namwamba alivyofanyiwa kwa kufurushwa ODM.
Bw Orengo naye anastahili kukoma uvuguvugu baada ya kukosa kupewa wadhifa wa kaimu kiongozi wa ODM na Profesa Anyang’ Nyong’o kuwahi nafasi hiyo.
Wanaopiga vita ushirikiano wa ODM na Rais Ruto ni wale ambao hawatakii ngome za chama zinufaike kama maeneo mengine kimaendeleo.
Leave a Reply