Gachagua achota wandani wa Kiunjuri Laikipia – Taifa Leo


MBUNGE wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri amejipata kwenye baridi ya kisiasa baada ya baadhi ya wandani wake kumkumbatia aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Mnamo Jumapili, Januari 19, 2025 Bw Gachagua alikuwa katika Kaunti ya Laikipia ambapo aliwaambia baadhi ya viongozi waweke wazi msimamo wao iwapo wapo mrengo wake wa kisiasa au ndani ya serikali.

Kati ya wale ambao aliwataka wajitokeze na kutoa msimamo ni Gavana wa Laikipia Joseph Irungu.

Bw Gachagua anatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa kisiasa kwa Mlima Kenya mwezi ujao, Februari 2025.

Anatarajiwa pia kutaja chama kipya cha kisiasa kwa wafuasi wake ambapo wamekerwa na UDA baada ya kutimuliwa kwa Bw Gachagua kama naibu rais mwaka jana, 2024.

“Tunawaambia viongozi wa Mlima Kenya wale ambao wamechaguliwa na wale ambao wanamezea mate viti, wajitokeze na kuwa na msimamo sasa. Chama chetu hakitakaribisha watu ambao wanahama dakika za mwisho,” akasema Bw Gachagua.

“Sijasikia chochote kutoka kwa Gavana Irungu hadi sasa na natuma naibu wake amwambie amuige mwenzake wa Nyeri Mutahi Kahiga ambaye amekuwa akizungumzia sana umoja wa Mlima Kenya,” akaongeza.

Naibu Gavana Reuben Kimari, Katibu wa kaunti Koinange Wahome na waziri wa utawala kwenye kaunti Purity Gitonga walijiunga na wawaniaji wengine 100 kuonyesha uaminifu wao kwa Bw Gachagua.

Hata hivyo, Bw Kiunjuri alionekana kupoteza pakubwa baada ya wandani wake Beth wa Diana ambaye ni mwenyekiti wa Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) na mwaniaji wa kiti cha useneta wa Laikipia 2022 John Kiama kuhamia mrengo wa Bw Gachagua.

Isitoshe, Diwani Catherine Nyokabi, mwandani wa Bw Kiunjuri pia aliungana na mrengo wa naibu rais huyo aliyebanduliwa.

Watatu hao wamekuwa na mbunge huyo kwenye chama chake cha TSP.

“Kuna baadhi ya watu ambao wanafikiria sitakuunga mkono lakini nakwambia mimi ndiye mfuasi wako sasa na nitauza chama chako. Nina uungwaji mkono wa wapigakura wa Laikipia kwa sababu nilipata kura 45,000 uchaguzi wa 2o22 nikiwania kiti cha mbunge mwakilishi wa kike,” akasema Bi Nyaga.

Bw Kiama ambaye amekuwa mshirika wa Bw Kiunjuri kwa zaidi ya miaka 10 naye alijitangaza kama kaimu mbunge wa Laikipia Mashariki.

Alisema Bw Kiunjuri amewataliki wanaeneobunge lake kwa sababu alipigia kura hoja ya kumng’atua Bw Gachagua.

Kwa wakati mmoja baada ya Bw Gachagua kutimuliwa kulikuwa na madai kuwa wadhifa wa unaibu rais ungemwendea Bw Kiunjuri kutokana na uaminifu wake kwa utawala wa Rais Ruto.

Gachagua akionekana kumlenga Kiunjuri, aliwataka wapigakura watambue viongozi wasaliti kisha wawaondoe mamlakani mnamo 2027.

Wabunge Sarah Lekorere (Laikipia Kaskazini), Wachira Karani (Laikipia Magharibi), Bw Kiunjuri na Mbunge Mwakilishi wa Kike Jane Kagiri wote wapo mrengo wa Rais Ruto.

Ni Seneta John Kinyua na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike Cate Waruguru ndio wapo mrengo wa Bw Gachagua kwenye kaunti hiyo.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*