Gachagua aanza mikakati ya kubomoa UDA – Taifa Leo


ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua yu mbioni kukibomoa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) huku akikaribia kutangaza chama chake kipya mwishoni mwa mwezi huu.

Baada ya kuonekana kukilemaza chama hicho katika eneo la Mlima Kenya, sasa Bw Gachagua ameelekeza kurunzi yake katika kaunti ya Kajiado eneo la Rift Valley.

Mnamo Jumatatu, wiki hii, Bw Gachagua aliupokea ujumbe wa wabunge na wanasiasa wengine wa UDA kutoka kaunti hiyo nyumbani kwake kijiji cha Wamunyororo, eneo bunge la Mathira, kaunti ya Nyeri.

Baada ya kutimuliwa mwaka jana, mwanasiasa huyo sasa amegeuza boma hilo kama kituo chake cha kufanya mikutano ya kupanga mikakati yake ya kisiasa.

Hapo ndipo Bw Gachagua ambaye ni mbunge wa zamani wa Mathira amekuwa akikutana na jumbe za wanasiasa kutoka maeneo mbalimbali, kupanga namna ya kulemaza UDA inayoongozwa na Rais William Ruto.

Ujumbe kutoka Kajiado uliongozwa na Mbunge wa Kajiado Kaskazini Onesmus Ngogoyo na Seneta wa kaunti hiyo Samuel Seki.

Ulishirikisha madiwani kadhaa wa UDA na hata Mbunge wa Kajiado Kusini Samuel Parashina aliyechaguliwa kwa tiketi ya ODM.

Bw Ngongoyo alishikilia kuwa hawatatishwa na msimamizi wa Ikulu Katoo Ole Mitito ambaye, kulingana naye, amekuwa akizunguka kote katika kaunti ya Kajiado akipendekeza wanasiasa wanaopasa kuchaguliwa kwa nyadhifa zote tano za kisiasa, 2027.

“Tunaungana kukabiliana na mrengo huo wa Ole Metito debeni 2027. Tunajipanga kujijenga nje ya mwavuli wa UDA na muungano wa Kenya Kwanza kwa sababu serikali ya sasa imewafeli Wakenya. Tunaungana na raia wenzetu kutoka kote nchini kurekebisha makosa ambayo yalifanyika katika uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema Bw Ngongoyo.

Bw Gachagua amefaulu kugawa chama cha UDA kuwili katika kaunti ya Kajiado.

Kambi yake inaongozwa na Bw Ngongoyo na Seneta Seki huku nyingi ikiongozwa na Bw Ole Metito, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Ruto.

Seneta Seki ndiyo amependekezwa na kambi ya Gachagua kuwania ugavana wa Kajiado 2027 huku Bw Ole Metito akitangaza wazi kwamba ndiye atawania kiti hicho kwa tiketi ya UDA.

Wengine walioko katika kambi ya Gachagua ni wakili Daniel Kanchori kutoka Kajiado Mashariki anayepigiwa upatu kuchukua nafasi ya Seki kama Seneta wa Kajiado, Moses Birisha aliyeshindwa na Bw Memusi Kanchori katika kinyang’anyiro cha ubunge cha Kajiado ya Kati, Moses Konana kutoka Kajiado Magharibi, Bw Parashina (Mbunge wa Kajiado Kusini) na idadi kubwa ya madiwani waliochaguliwa kwa tiketi ya UDA.

Kwa upande mwingi, Bw Ole Metito akaongoza kambi ya Rais Ruto ambayo pia inashirikisha Mwakilishi wa Kike Leah Sankaire, Mbunge wa Kajiado Magharibi George Sunkuiya miongoni mwa wengine.

Katika eneo la Mlima Kenya na Nairobi, Bw Gachagua amewatambua wanasiasa kadhaa atakaowaunga mkono kuwaondoa wabunge waliounga mkono hoja ya kumtimua mamlakani mwaka jana.

Kwa mfano, katika kaunti ya Nyeri, viongozi wakiongozwa na Gavana Mutahi Kahiga wameweka wazi kuwa wanasubiri Bw Gachagua atangaze chama ili wahame UDA.

Bw Kahiga amenukuliwa akisema kwamba baada ya Gachagua kuondolewa mamlakani na kupokonywa wadhifa wa Naibu Kiongozi, ilikuwa wazi kuwa hawatakiwi katika chama tawala.

Katika eneo la Nyeri Mjini Mbunge wa zamani Ngunjiri Wambugu ananolewa kumwondoa Mbunge wa sasa Duncan Mathenge, huku katika eneo bunge la Othaya Gachagua anaunga mkono Patrick Ngunjiri, almaarufu, Wakili wa Mashinani, kumwondoa Wambugu Wainaina.

Seneta wa Murang’a Joe Nyutu anatarajiwa kuongoza viongozi wa kaunti hiyo kuhamia chama cha Gachagua, sawa na mwakilishi wa wanawake kaunti ya Kirinyanga na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba ambao wamekuwa watetezi wake wakuu.

Katika kaunti ya Nyandarua Bi Sasha Wamae anaandaliwa kumwondoa Mwakilishi wa Kike wa sasa Faith Gitau huku Mercy Nungari akitiwa makali kumwondoa Mwakilishi wa Kike wa Kiambu Anne Muratha.

Mnamo Jumapili, Bw Gachagua alikuwa katika Kaunti ya Laikipia ambapo aliwaambia baadhi ya viongozi waweke wazi msimamo wao iwapo wako mrengo wake wa kisiasa au ndani ya serikali.

Kati ya wale ambao aliwataka wajitokeze na kutoa msimamo ni Gavana wa Laikipia Joseph Irungu. Bw Gachagua anatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa kisiasa kwa eneo la Mlima Kenya mwezi ujao. Anatarajiwa pia kutaja chama kipya cha kisiasa kwa wafuasi wake ambao wamekerwa na UDA baada ya kutimuliwa kwa Bw Gachagua kama naibu rais mwaka jana.

“Tunawaambia viongozi wa Mlima Kenya waliochaguliwa na wale ambao wanamezea mate viti, wajitokeze na kuwa na msimamo sasa. Chama chetu hakitawakaribisha watu ambao wanahama dakika za mwisho,” akasema Bw Gachagua.

Naibu Gavana Reuben Kimari, Katibu wa kaunti Koinange Wahome na waziri wa utawala kwenye kaunti Purity Gitonga walijiunga na wawaniaji wengine 100 kuonyesha uaminifu wao kwa Bw Gachagua wakiwemo wandani wa mbunge wa eneo hilo Mwangi Kiunjuri, Beth wa Diana (mwenyekiti wa Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) na mwaniaji wa kiti cha useneta wa Laikipia mnamo 2022 John Kiama.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*