Bob Munro akumbukwa kwa kulea vipaji vingi kupitia kituo cha MYSA – Taifa Leo


RISALA za rambirambi zinaendelea kumiminika kutokana na kifo cha Robert Donald ‘Bob’ Munro, mwanzilishi wa Mathare United FC chini Kituo cha Michezo cha Vijana wa eneo la Mathare (MYSA), lililoasisiwa mnamo 1987.

Marehemu Munro aliyelelewa Ontario, Canada, alifahamika kwa ukuzaji wa talanta za vijana kupitia michezo katika mtaa huo wa mabanda wa Nairobi, alifariki Jumapili katika makazi yake mtaani Westlands, Nairobi akiwa na umri wa miaka 82.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na mkewe, Ingrid Munro, marehemu alikuwa na matatizo ya kupumua akitibiwa na kutoka hospitalini kwa muda wa miezi sita kabla ya kuaga dunia, mwishoni mwa wiki.

Wengi wamemsifu Munro kama jagina aliyeacha urithi wa kudumu katika soka nchini na maendeleo mengine miongoni mwa jamii.

Safari ya Munro nchini ilianza mwaka wa 1987 alipohamia Nairobi na mkewe Ingrid na kuamua kuingia vitongoji duni vya mtaani Mathare na kuanzisha MYSA kwa lengo la kuwasaidia vijana kukuza talanta zao kupitia spoti.

Tangu wakati huo, MYSA imesaidia katika kuboresha maisha ya familia nyingi, mbali na kukuza vipaji vya vijana wa maeneo mengine nchini Kenya kwa jumla.

Lakini mchango wake mkubwa ulitambuliwa zaidi kupitia azima yake ya kuinua soka ya mashinani, pamoja na kuifanya ligi kuu ya Kenya kuendeshwa kitaaluma, hatua ambayo ilimpa jina la “Baba wa KPL”.

Katika hali ya kutambua mchango wake, Rais William Ruto alimpokeza tuzo ya kishujaa ya Elder of the Order of the Burning Spear (EBS) wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 60 tangu Kenya ijipatie uhuru kutoka kwa Mkoloni.

Kwenye taarifa yake, Rais Ruto alisema urithi wa marehemu utaendelea kupitia maelfu ya wahitimu wa MYSA wanaoendelea kuwa viongozi katika sekta mbalimbali za jamii nchini.

“Kujitolea kwake kuliwapa vijana wengi ajira kupitia michezo, huku akiacha urithi usiofutika katika nyanja ya soka nchini,” aliongeza rais Ruto.

Waliokuwa wachezaji wa Mathare United, Francis Kimanzi, Anthony Kimani, Patrick Mutheu miongoni mwa wengine walimsifu Munro kama mtu aliyebadilisha maisha yao kwa njia mbalimbali kuanzia utotoni.

Kimani alikuwa nahodha wa Mathare United walipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2008. Kimanzi ndiye kocha mkuu wa kikosi cha Harambee Stars.

Mipango ya mazishi inaendelea huku ripoti zikieleza kuwa huenda akachomwa wikendi hii Nairobi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*