JINA la Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa Gladys Shollei lilitajwa mahakamani katika kesi inayoendelea kuhusu umiliki wa shamba linalokisiwa kuwa na thamani ya Sh100 milioni linazozaniwa na familia mbili katika Kaunti ya Uasin Gishu.
Jina la Bi Shollei liliwasilishwa katika kesi hiyo na mlalamishi, Bw Abraham Chebii, dereva katika Tume ya Huduma za Mahakama, ambaye Jumatatu aliambia mahakama ya Eldoret kwamba maisha yake yalikuwa hatarini, kufuatia kile alichokitaja kuwa vitisho kutoka kwa Bi Shollei kuhusiana na kesi husika.
Bw Chebii alimwambia Jaji Robert Wananda, kwamba maisha yake yalikuwa hatarini kutokana na mzozo wa shamba la ekari 37 huku akiwasilisha kortini malalamishi dhidi ya Bi Shollei ambaye pia ni Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Uasin Gishu.
Akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo, Bw Chebii aliomba mahakama imhakikishie usalama wake ili aendelee kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo.
Hata hivyo, Bw Chebii anasisitiza kuwa alirithi ardhi husika kutoka kwa marehemu babake, Paul Cherono huku familia ya marehemu Philip Cheruiyot Tumbes kupitia kwa mwanawe mkubwa Cledy Kiprono Cheruiyot ikisisitiza kuwa shamba hilo ni la marehemu baba yao huku akimtaja Bw Chebii kama mgeni katika ardhi hiyo.
Kwa upande wake Bw Chebii aliambia mahakama kuwa marehemu babake alikodisha ardhi hiyo kwa familia ya Tumbe zaidi ya miaka 60 iliyopita kwa vile alikuwa na mali nyingine katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Bw Chebii ambaye anawakilishwa na Wakili Andrew Kiboi alidai kuwa ana ushahidi wa kuonyesha kwamba shamba hilo ni la marehemu babake.
Huku familia pinzani kupitia kwa Cledy Kiprono Cheruiyot ambao wanawakilishwa na wakili Elijah Momanyi wanadai wana hati halisi ya kumiliki mali hiyo na kumtaka Bw Chebii kuwasilisha stakabadhi zake za umiliki ikiwa kweli ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo.
Kulingana na Cheruiyot babake alipata ardhi hiyo katika mpango wa makazi wa Kaptagat mnamo 1965 na kusajiliwa kama ploti no 173 kwa jina Paul Philip Cherono.
Kesi hiyo itaendelea kusikizwa Machi 10.
Leave a Reply