MIENENDO ya wanasiasa kugeuza mikutano ya amani kuwa majukwaa ya kutoa matamshi ya chuki imesababisha Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kubuni sheria kali inayotoa mwongozo kuhusu suala hilo.
Tume hiyo, kwenye mapendekezo yake kwa Mswada kuhusu Uwiano na Utangamano wa Kitaifa wa 2023, inataka wabunge waipe mamlaka zaidi ili iweze kubaini uhalisia wa mikutano halisi ya amani.
NCIC inataka iwe na usemi katika utoaji idhini kwa shirika au watu wanaotaka kuandaa mikutano ya amani, ikiwemo kuwalazimisha kufichua wafadhili wa mikutano kama hiyo.
Hatua hiyo, kulingana na tume hiyo, itaiwezesha kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa watu wanaojihusisha na mipango ya kupalilia amani katika ngazi za kaunti, hawachochei chuki na uhasama katika eneo lolote lile.
Masharti hayo yanayopendekezwa na NCIC yanalenga kuzima mienendo ya mashirika na watu binafsi kujificha kwa ajenda ya kuleta amani ila mikutano yao inaishia kuwa ya kisiasa au yenye kuchochea chuki za kikabila nchini.
Mikutano mingine kama hiyo pia imeishia kuwa majukwaa ya kutoa mafunzo ya itikadi kali haswa kwa vijana, kwa misingi ya kidini, hatua ambayo husababisha migawanyiko nchini.
Wakati huu, tume ya NCIC chini ya Kipengele cha 27 cha Katiba imetwikwa wajibu wa kutoa uhamasisho kuhusu haja ya watu kuishi kwa amani, kuvumilia, kuheshimiana, kuelewana na kukubaliana, bila kuzingatia makabila yao.
NCIC pia ina wajibu wa kuhakikisha kuwa watu wa makabila yote wanaelewa katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kitamaduni na kisiasa. Tume hiyo pia imetwikwa kibarua cha kuhakikisha kuwa watu wa makabila yote wanapata huduma za serikali na asasi za kibinafsi bila kubaguliwa kwa misingi ya kikabila, kidini, au asili yao.
Isitoshe, Katiba inaipa NCIC kibarua cha kuunda sera za kuendeleza maadili ya kitaifa na utawala bora.Mapendekezo ya tume hiyo kwa Bunge la Kitaifa yanalenga Kifungu cha tano cha Mswada huo kinachohusiana na majukumu yake.
NCIC inataka wabunge waiongezee mamlaka ili iweze kuandaa masharti ya kuzingatiwa na watu wanaolenga kujihusisha katika mipango ya kupalilia amani nchini. Kabla ya shirika au mtu yeyote kuanzisha mipango kama hiyo, tume hiyo sasa inapendekeza kuwa ipokezwe majina ya maafisa husika na mipango hiyo na maelezo mengi ambayo inahitaji.
Wale wanaotaka kuendesha mipango ya kupalilia amani nchini pia watahitajika kuwasilisha kwa NCIC ithibati kuhusu iwapo wameendesha shughuli kama hiyo katika jamii lengwa na matokeo yake.
Shirika au watu wanaopania kuendesha mipango ya amani pia watahitajika kutoa ratiba ya shughuli wanazolenga kutekeleza, muda wa kutekeleza mipango hiyo, wafadhili wa mpango huo na taarifa kuhusu iwapo kuna mgongano wowote wa kimasilahi.
Watu kama hao pia watahitaji kuwasilisha taarifa kwa NCIC kuhusu mahala ambapo shughuli hiyo itaendeshwa, jamii lengwa na malengo ya shughuli nzima.
Leave a Reply