MABILIONI ya fedha kutoka kwa serikali na haja ya kuunda miungano na vyama vikubwa ndio sababu kuu zinazochangia wanasiasa wengi kutaka kusajili vyama vipya vya kisiasa.
Taifa Leo imebaini kuwa, Afisi ya Msajili wa Vyama Vya Kisiasa (ORPP) sasa inashughulikia karibu maombi 30 kutoka kwa watu wanaotaka kusajili vyama vipya kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Aidha, baadhi ya watu ambao hawana nia ya kuwania nyadhifa za kisasa wanapania kuvisajili vyama vipya kwa nia ya kuviuza kuelekea uchaguzi huo mkuu.
Uuzaji na ununuzi wa vyama vya kisiasa umeibuka kuwa biashara kubwa, haswa kutokana na hofu wa wanasiasa kunyimwa haki wakati wa kura za mchujo.
Baadhi ya viongozi wakuu wa kisiasa pia wameishia kusalia bila vyama baada ya makundi pinzani kutoroka na vyeti vya vyama vyao.
Visa kama hivi vimelazimisha wanasiasa wenye ndoto za kushiriki katika chaguzi kuu kuwa na vyama vyao ili baadaye washiriki mazungumzo ya kuunda muungano na vyama vikubwa.
Sheria inayoilazimu Serikali Kuu kutoa ufadhili wa mabilioni ya fedha kwa vyama vya kisiasa, imefanya uendeshaji wa shughuli za vyama kuwa biashara kubwa.
Angalau vyama 48 vya kisiasa vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu wa 2022 vinapokea mamilioni ya pesa za umma kufadhili shughuli za kuviendeleza.
Tangu wakati huo, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu ametoa usajili wa muda kwa vyama sita vya kisiasa. Aidha, afisi ya Bi Nderitu imetoa notisi ya kutoa cheti cha muda cha usajili kwa vyama vingine vitatu.
“Kando na hayo, afisi yake sasa inashughulikia maombi ya usajili kutoka kwa vyama 30 vipya. Shughuli hiyo iko katika hatua mbalimbali,” akasema.
Bi Nderitu alisema hayo siku chache baada ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kufichua nia yake ya kutangaza chama chake kipya ndani ya wiki mbili zijazo.
Tangu atimuliwe mwaka jana, Bw Gachagua amekuwa akisikitikia hatua yake ya kushirikiana na Rais William Ruto bila chama chake cha kisiasa.
Afisi ya ORPP imetoa notisi kuhusu usajili wa muda wa vyama vipya vya; Forum for Economic Development Agenda (FEDA), Kenya United Generation Party (KUG) na The Future Party (TFP).
Rangi za chama cha FEDA ni samawati, dhahabu na nyekundu huku nembo yake ikiwa lango.
Kimeorodhesha Stephen Tinga, Lucy Wambui, William Keloi, Christine Ndegwa, Benard Koskei na Risper Awuor kama wanachama waanzilishi wake.
Chama cha KUG –kina rangi ya kijani, kahawia na samawati kama rangi zake huku nembo yake ikiwa alama ya mviringo.Wanachama waasisi wa chama hicho ni; Jared Nyabuto, Sammy Mwanyaa, Sharon Jepkorir, Fredrick Wafula, Purity Mumbe, Vicky Chebet, Hezbon Oluoch, Cynthia Wangui, Joshua Mwonga na Frejustus Kiima.
Nacho chama cha TFP kimeteua rangi za kijani, nyeupe na samawati na maua kama nembo yake.
Kimeorodhesha Mercy Chiluyi, Benerd Mutie, Jesse Thuo, Deolata Ngatho, Diana Kemunto, Ibrahim Moses, Daniel Mwangi, Eunice Barasa, Imelda Nyongesa, Robinson Makokha, Annastacia Jelimo, Francis Maina and Eric Wanyama kama wanachama waanzilishi wake.
Vyama sita ambavyo vimepata vyeti vya muda ni pamoja na chama cha The We Alliance Party (TWAP), ambacho alama yake ni sahani na kijiko huku rangi zake zikiwa samawati na manjano.
Chama hicho tayari kimewasilisha maombi ya kutaka usajili kamili, kulingana na afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.
Vyama vingine vilivyopewa vyeti vya usajili wa muda ni; People’s Forum for Rebuilding Democracy (PFRD), Imarisha Uchumi Party (IUP), African Development Congress (ADC), Kenya Ahadi Party (KAP) na chama cha Democracy for Citizens Party (DCP).
Leave a Reply