SHULE za umma kote nchini zinakabiliwa na hali ngumu kifedha baada ya serikali kuchelewa kutoa fedha kabla ya muhula wa kwanza kuanza ilivyokuwa imeahidi.
Ucheleweshaji huo umeweka zaidi ya shule za Msingi za umma 23,000 na karibu shule 10,000 za sekondari katika hali mbaya ya kifedha, na hivyo kulazimu nyingi kukopa kukidhi shughuli za kimsingi.
Hii inafuatia kutotimizwa kwa ahadi ya Waziri wa Elimu Julius Ogamba kuwa pesa hizo zingetolewa kabla ya shule kufunguliwa, huku Waziri wa Fedha John Mbadi akitoa hahakikisho kuwa fedha za muhula wa kwanza zingetolewa ndani ya wiki ahadi ambayo haijatimizwa.
“Wiki ijayo Hazina itatoa Sh48.8 bilioni ambayo ni asilimia 50 ya mgao wa mwaka huu kufadhili mfumo wetu wa elimu,” alisema Waziri Mbadi mnamo Januari, 17, 2025.
Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi nchini Kenya (KEPSHA) Johnson M. Nzioka ameeleza wasiwasi wake kuhusu matatizo ya kifedha yanayokabili shule za umma, akisema kucheleweshwa kwa fedha kumeongezea presha wasimamizi wa shule.
Bw Nzioka alilalamika kuwa serikali haijatimiza ahadi yake jambo ambalo limeacha shule nyingi na changamoto tele.
“Serikali ilituhakikishia kwamba fedha zingetolewa kabla ya muda kuanza, lakini haikuwa hivyo, tuliahidiwa fedha zingetolewa ndani ya wiki moja, bado wiki imegeuka mwezi, sasa hivi shule zinaendeshwa kwa mkopo, na hii inaathiri pakubwa ari ya walimu na ubora wa elimu,” alisema.
Kulingana na Bw Nzioka, shule za msingi za umma zinatatizika kukidhi mahitaji ya kimsingi, ikiwa ni pamoja na kulipa wauzaji bidhaa na kudumisha huduma muhimu. Walimu pia wanateseka.
“Serikali inatarajia shule zifanyeje? Tulifunga shule bila fedha jam,bo ambalo ni aibu. Wauzaji wanakuja ofisini kwetu wakitaka malipo,” akasema Bw Nzioka.
Aliomba serikali kuharakisha kutoa fedha ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi akisema kuna umuhimu wa kuwa na mkakati endelevu wa kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati. Alionya kuwa tatizo la fedha lililopo sasa linaweza kusababisha madhara ya muda mrefu kwa sekta ya elimu.
“Hatuwezi kuendelea kufanya kazi namna hii, shule ziko katika hali mbaya na imani katika mfumo wa elimu inapungua, tunahitaji hatua za haraka,” akasema Bw Nzioka.
Mwalimu mkuu mmoja katika kaunti ya Bungoma alieleza hali mbaya ya shule katika eneo hilo kutokana na ukosefu wa rasilimali muhimu na usaidizi kutoka kwa serikali.
“Sijui jinsi serikali inataka tufanye kazi kwa sababu hakuna vitabu, hatuna hata lango, na walinzi wawili walijiuzulu. Niko kwa shida kwa sababu walimu hawana hata chaki. Inabidi wachangie pesa ili tununue chakula cha mchana. Ni aibu kusema,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya (KESSHA) Willy Kuria ameitaka Wizara za Fedha na Elimu kulipa malimbikizi ya Sh64 bilioni ambazo haijalipa kwa muda wa miaka minne.
Alisema kuwa shule nyingi zinadaiwa kuanzia Sh20 milioni hadi Sh70 milioni, huku baadhi ya wakuu wa shule wakiaibishwa na wauzaji bidhaa.
“Serikali lazima iachilie Sh64 bilioni kusaidia shule kulipa madeni. Tunatatizika kulipa madeni na bili kama vile za maji na umeme,” akasema Bw Kuria.
Leave a Reply