Jinsi kufunza wanafunzi kilimo kulivyomvunia Orina uteuzi wa Mwalimu Bora Duniani – Taifa Leo


DOMINIC Ming’ate Orina si mgeni kwa Wakenya, hasa wale wanaopenda sana kilimo.

Kabla ya kuorodheshwa kwa Tuzo ya Mwalimu Bora Duniani, mwalimu huyu ambaye pia ni mkulima, tayari alikuwa amejipatia umaarufu katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii kupitia mafunzo yake ambayo yanahusu mbinu bunifu za kilimo.

Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ilimtuma katika Shule ya Msingi ya Kugerwet, eneobunge la Konoin, katika Kaunti ya Bomet.

Mwalimu huyo ambaye ana mizizi yake Kaunti ya Nyamira, mara moja alianza safari ya kuelekea kituo chake kipya cha kazi huko Bomet.

Akiwa Nyamira, Orina alikuwa amezoea lishe bora, iliyojumuisha aina mbalimbali za mboga na matunda.

Hata hivyo aligundua kuwa kulikuwa na uhaba wa vyakula hivi huko Konoin kwani wenyeji walijishughulisha zaidi na ukuzaji wa chai na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Alikodisha chumba katika kituo cha kibiashara cha Satiet na siku chache baada ya kutulia, hamu ya kuanzisha bustani ndogo ya jikoni, ambapo angeweza kupanda mboga kwa matumizi yake mwenyewe, ilianza na kukua.

Kwa muda mfupi, mboga zake zilichanua na kuvutia majirani. Aliendelea hadi 2020 wakati nchi ilikumbwa na janga la Covid-19.

Ni wakati huu ambapo Orina alipata mafanikio. Alionyesha picha za mradi wake wa bustani ya jikoni kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na kuvutia hisia za Wakenya ambao walivutiwa na ubunifu wake.

Kwa sababu ya maswali mengi, alianzisha ukurasa wa Facebook na kuuita “Vidokezo vya Bustani ya Magunia” ambao ulikua kwa kasi zaidi na kwa sasa unajivunia kuwa na wafuasi zaidi ya 470,000.

Hatimaye shule zilipofunguliwa mwaka wa 2021, Orina aligundua kuwa mfumo mpya wa elimu nchini Kenya, mtaala unaozingatia Umilisi na Utendaji (CBC), ulikuwa umesisitiza haja ya wanafunzi kufahamu kilimo cha ubunifu.

Alichukua wazo lake la kutengeneza bustani jikoni hadi Shule ya Msingi ya Kugerwet. Kwa msaada wa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Orina alianzisha mradi wa kilimo kwenye sehemu ya shamba la shule ambapo, pamoja na wanafunzi, akuza mboga na kufuga sungura.

Orina na wanafunzi wake baadaye walianzisha kilabu ya 4K.

Mbali na kuwasaidia wanafunzi wake kukumbatia kilimo katika ujana wao, Orina ana mpango mwingine unaoitwa “Nivalishe” ambapo amewapa zaidi ya wanafunzi 150, hasa wale wanaotoka katika mazingira duni, sare mpya.

Hatua hii imesaidia wanafunzi kuhudhuria shule bila kukosa.

Amefanikisha hili kupitia usaidizi anaopokea kutoka kwa mashabiki wake mtandaoni na watu wanaomtakia heri. Pia ni chini ya mpango huu ambapo ameweza kusambaza sodo na vifaa vya kusoma kwa wanafunzi wasio na uwezo.

Kabla ya uteuzi wa tuzo ya kimataifa, Orina alikuwa ametunukiwa tuzo na Wizara ya Elimu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Tuzo ya UNESCO ilikuwa ya huduma zake mashuhuri kwa jamii.

Wizara ya Elimu ilimtambua kama mwalimu bora zaidi wa ubunifu katika CBC katika eneo la Cheptalal.

Pia aliibuka wa pili katika tuzo tatu chini ya Optiven Foundation 2021.

Orina ni Mkenya wa tatu ambaye amefanikiwa kuingia katika orodha ya mwisho ya walimu 50 kwa tuzo hiyo ya kimataifa tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2015.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*