JOMO Kenyatta, rais mwanzilishi wa Kenya, alikuwa akipenda kubarizi nyumbani kwake Ichaweri na mrithi wake Daniel Moi alipenda kualika jumbe na kupanga mikakati yao ya kisiasa katika Kabarak.
Rais William Ruto kwa wakati huu anatumia shamba lake la Narok na kiongozi wa ODM Raila Odinga hutumia shamba la Opoda, Bondo. Mara nyingi, wanasiasa hutumia majina ya vijiji vyao kuteka hisia za kitaifa.
Na sasa, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ameleta msisimko katika kijiji cha Wamunyoro, Mathira, kaunti ya Nyeri.Bw Gachagua anaendelea kushamiri kisiasa kutokana na idadi ya wajumbe anaopokea nyumbani kwake Wamunyoro.
Miongoni mwa jumbe alizopokea hivi majuzi ni kutoka Ukambani, Kajiado na Kisii na kuibua shauku kutoka kwa wafuasi wa Rais Ruto ambao wanafuatilia kwa karibu shughuli zake Wamunyoro.
Ingawa baadhi ya jumbe ni za watu wasiojulikana kisiasa, Bw Gachagua na timu yake wanasisitiza ni mwanzo tu.Akihutubia ujumbe kutoka Kaunti ya Nyandarua mnamo Alhamisi, Bw Gachagua alisema: “Tunaendelea kuvutia maeneo mengine mengi ambayo hayajaridhishwa na jinsi nchi inavyoendeshwa na baada ya muda itathibitishwa hiki ni kitovu cha utaifa.”
Leave a Reply