KUONGEZEKA kwa mauaji ya kikatili ya wanawake nchini kunaonyesha kuwa, kuna tatizo kubwa ambalo limekuwa likipuuzwa na ambalo linapaswa kushughulikiwa kwa dharura.
Kiwango ambacho visa hivi vinaongezeka kinaashiria jamii ambayo inadharau wanawake kiasi cha kuwachukulia kama viumbe wasio na thamani ambao maisha yao yanaweza kukatizwa kiholela.
Inaatua moyo kwamba, ukatili huu unatendeka katika karne ya 21 ambayo watu wamestaarabika na uhai wa binadamu unafaa kuthaminiwa zaidi. Ishara zote zinaonyesha jamii inayokolewa na taasubi ya kiume inayopuuza mchango wa wanawake katika kuendeleza na kukuza kizazi na mchango wao kwa ujenzi wa taifa licha ya ukweli kwamba, nchi zinazothamini, kutambua na kuwa na imani katika wanawake zimepiga hatua kimaendeleo.
Inaonyesha jamii ambayo inarudi nyuma badala ya kusonga mbele, inadhihirisha kuwa kuna masuala ya kijamii yanayopuuzwa na wanaopaswa kujukumika kupalilia na kukita maadili wakiwemo viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii.
Mauaji haya, yakiwemo ya watoto wasio na hatia hadi ya akina nyanya yanaakisi kiwango cha kutisha cha mmomonyoko wa maadili, kuongezeka kwa matatizo ya akili yanayotokana na kudorora kwa uchumi na kwa jumla, kukosa kwa viongozi kutambua na kudumisha haki za wanawake inavyofafanua katiba.
Mfano ulio hai ni Bunge kukosa kupitisha sheria ya kuhakikisha thuluthi mbili za wawakilishi haitoki jinsia moja. Kwa kujivuta kutimiza hitaji hili, tabaka la wanasiasa wanaume lilionyesha dharau kwa wanawake.
Kukabiliana na ongezeko hili la mauaji ya wanawake, kunahitaji nia njema na uchunguzi wa dhati pasipo siasa.
Leave a Reply