Chimbuko la uhasama kati ya Ruto na Tshisekedi unaolemaza juhudi za amani DRC – Taifa Leo


RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi aliwashangaza wengi kwa kususia mkutano wa dharura ulioitishwa na Rais William Ruto kujadili njia za kukomesha ghasia nchini mwake.

Mkutano huo wa marais wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika mtandaoni Jumatano jioni ulijadili mikakati ya kurejesha usalama mji mkuu mashariki wa DRC, Goma, uliotekwa na waasi wa M23 Jumatatu, Januari 27, 2025.

Dkt Ruto aliitisha, na kuongoza, mkutano huo kwa misingi ya kwamba ndiye mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo kuanzia Desemba 2024.

Lakini Rais Tshisekedi alihiari kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika nchini Zimbabwe Alhamisi, Januari 30, 2025 kujadili suala hilo hilo la utovu wa usalama mashariki mwa DRC.

Mkutano huo wa marais na viongozi wanachama wa SADC unafanyika jijini Harare chini ya uenyekiti wa Rais wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa.

Lakini kuhusu mkutano wa EAC ulioitishwa na Rais, Tshisekedi, kupitia msemaji wake, Tina Salama, alisema hangeuhudhuria kwani  “unakinzani na shughuli zake zingine zilizoratibiwa.”

Hii ni licha ya kwamba alipoitisha mkutano huo, Rais Ruto alisema kuwa mahasimu katika mzozo huo – Rais Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, walikubali kuhudhuria mkutano huo.

“Ningependa kuwashukuru marais Tshisekedi na Kagame kwa kuthibitisha kuwa watahudhuria mkutano huo,” akasema.

Rwanda imetuhumiwa kwa kuunga mkono na kufadhili waasi wa M23, lakini imekana madai hayo.

Sasa swali ni je, mbona Rais Tshisekedi alisusia mkutano wa EAC uliotishwa na Rais Ruto na akaamua kuhudhuria ule wa SADC unaoongozwa na Rais Mnangagwa?

Kulingana na wachanganuzi wa masuala ya kidiplomasia, sababu kuu iliyochangia Rais Tshisekedi kutohudhuria mkutano wa EAC ni chuki dhidi ya Rais Ruto na kutotaka kujihusisha na masuala ya jumuiya hiyo.

“Sio kweli alivyosema msemaji wa rais wa DRC Tina Salama kwamba kiongozi huyo hangeweza kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Dkt Ruto kwa sababu ulikinzana na ratiba yake. Tshisekedi anamchukia rais huyu wa Kenya kutokana na dhana kuwa Dkt Ruto anaunga mkono Rwanda anayoamini kuwasaidia waasi wa M23,” anasema Profesa Macharia Munene.

“Wanasiasa wenye ushawishi na hata raia wengi wa DRC pia wanaamini kuwa Kenya inapendelea waasi hao. Hii ndio maana ubalozi wa Kenya ni miongoni mwa balozi za kigeni zilizoshambuliwa na waandamanaji jijini Kinshasa waliokuwa wakilaani kutekwa kwa mji wa Goma na M23,” anaongeza msomi huyo ambaye anafundisha kozi ya Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU), bewa la Afrika.

Itakumbukwa kuwa mnamo Julai 26 mwaka jana, Rais Tshisekedi alimshutumu Rais Ruto kwa kuchukua udhibiti wa mchakato wa kuleta amani nchini humo uliokuwa ukiongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa udhamini wa EAC.

Rais huyo wa DRC alishikilia kuwa Bw Kenyatta ndiye alifaa kuendelea kuongoza mchakato huo huku akisema hivi:

“Sharti niseme wazi, Rais Ruto anaunga mkono Rwanda na siwezi kusema zaidi ya hayo.”

Baada ya Tshisekedi kutoa kauli hiyo, DRC ilimrejesha nyumbani balozi wake nchini Kenya John Kalunga Nyakeru.

Bw Tshisekedi alionekana kukasirishwa na kauli aliyotoa Rais Ruto mnamo Mei 24, 2024 iliyoitetea Rwanda kuhusiana na lawama kwamba ndio inaunga mkono na kutoa ufadhili kwa M23.

Kwenye mahojiano na mashirika ya habari ya Jeune Afrique na Africa Report wakati wa Mkutano wa Maafisa Wakuu Kampuni za Afrika (African CEO’s Forum) jijini Kigali, Rais Ruto alitaja lawama hizo kama “zisizo na msingi wowote kwa sababu wanachama wa M23 ni raia wa DRC.”

“Mbona isemekane kwamba Kagame ndiye amesababisha kero la M23. Chimbuko la changamoto hii ni DRC kwa sababu wapiganaji ni raia wa nchi hiyo,” Dkt Ruto akasema, kauli ambayo ilionekana kumkera Rais Tshisekedi na serikali yake.

“Kama marais, wakati wa mkutano mmoja, tuliuliza hivyo, je wanachama wa M23 ni raia wa Rwanda au DRC? Na DRC ikatuambia: Wao ni raia wetu. Kwa hivyo, mbona wanahusishwa na Rwanda?” akaongeza.

Hata kabla ya Rais Ruto kutoa kauli hiyo ya kukera, Rais Tshisekedi alikuwa ameanza kuibua tashwishi kuhusu utendakazi wa kikosi cha jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) kilichotumwa DRC kulinda amani huku kikiongozwa na wanajeshi wa Kenya.

Wakati wa ziara yake nchini Botswana mnamo Mei 23, 2023, Tshisekedi alidai wanajeshi hao walikuwa “wakishirikiana” na waasi badala ya kukabiliana nao.

“Rais amesema matokeo ya utendakazi wa wanajeshi wa EACRF walioletwa kuokoa DRC hauridhishi na kwamba watahitajika kuondoka kutoka himaya ya Congo,” ikasema taarifa kutoka Ikulu ya Rais Tshisekedi, baada ya kiongozi huyo kukutana na mwenyeji wake wa Botswana wakati huo, Mokgweetsi Masisi.

Ni katika mkutano huo ambapo Rais Tshisekedi aliiomba Jumuiya ya SADC itume wanajeshi wake Goma kusaidiana na wanajeshi wa DRC kupambana na waasi wa M23.

Hatimaye wanajeshi wa EACRF (wakiwemo 900 kutoka Kenya) waliondoka mwishoni mwa 2023 na nafasi yao ikachukuliwa na kikosi cha SADC kikiongozwa na wanajeshi wa Afrika Kusini.

Ikumbukwe kuwa Dkt Ruto alianza kuikera DRC hata kabla ya yeye kuingia Ikulu.

Miezi michache baada ya nchi hiyo kushawishiwa na Bw Kenyatta ijiunge na jumuia ya EAC mnamo 2022, Ruto (akiwa naibu rais) alidai raia wa DRC hawawezi kufuga ng’ombe wa maziwa.

Huku akitoa wito kwa Wakenya kuwekeza katika ufugaji ngombe wa maziwa kwani kuna soko kubwa la maziwa, na bidhaa nyinginezo, nchini DRC, Dkt Ruto alidai kuwa uraibu mkubwa wa raia wa DRC ni kuvalia long’i ndefu za kucheza muziki.

Viongozi wa kisiasa wa DRC waliishutumu Kenya kufuatia kauli hiyo hadi balozi wa Kenya nchini humo wakati huo John Masafu akaomba msamaha.

Dkt Ruto alipoingia mamlakani na kuteua Kanali Shem Amadi kuwa balozi mpya wa Kenya nchini humo kuchukua nafasi ya Dk Masafu, Rais Tshisekedi ameonekana kukataa kupokea stakabadhi zake.

Kanali Amadi amekuwa akisubiri kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu Novemba 2023 alipoteuliwa. Kwa hivyo, ubalozi wa Kenya uliovamiwa Jumatatu haujakuwa na kiongozi tangu wakati huo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*