VIONGOZI 13 wanawake wamejitokeza kumtetea Jaji Mkuu Martha Koome dhidi ya kile walichokitaja kuwa mashambulizi yasiyo ya msingi dhidi ya rais huyo wa Mahakama ya Juu pamoja na majaji wa mahakama hiyo.
Katika taarifa, viongozi hao wanawake akiwemo Dkt Jennifer Riria, Prof Maria Nzomo na Zipporah Kittony, walisema kuna mwelekeo unaoibuka wa kujaribu kuwaangusha wanawake kila wanapopanda nyadhifa za ngazi za juu.
Viongozi hao walisema haikuwa haki kushambulia Jaji Mkuu haswa wakati nchi inakumbwa na “ukiukaji wa sheria usio na kifani, utekaji nyara na mauaji ya wanawake” kati ya maovu mengine.
“Tunaona dharau kwa Mahakama kama hatari kwa uendelevu wa utawala wa sheria na usalama wa raia,” viongozi hao walisema.
Wengine waliotia saini taarifa hiyo ni Daisy Amdany, Grace Musyoka, Mercy Jelimo, Roselindah Andambi, Salome Chege, Brenda Nabututu, Dk Juliet Kimemia, Bilha Joyce, Naomi Njoroge na Mary Njuguna.
“Wanawake wanatambua kwamba mashambulio haya yasiyofaa na ya kikatili dhidi ya Jaji Mkuu, majaji wa Mahakama ya Juu, yanalenga kudharau Idara ya Mahakama na kusababisha Wakenya kukosa imani nayo. Hali kama hiyo inaweza kusababisha machafuko. Kama wanawake, hatuwezi tena kukaa kimya,” waliongeza.
Viongozi hao walisema chini ya uongozi wa Jaji Koome, Mahakama imepiga hatua kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kufanya nafuu haki kupatikana na kuipeleka karibu na wananchi hasa wale wa mashinani.
Walisema kwamba Jaji Mkuu Koome ameanzisha mahakama za haki za kijinsia, kupanua mahakama za madai madogo na kukuza mtazamo wa haki.
Viongozi hao wanawake waliongeza kuwa Jaji Mkuu Koome ameanzisha uwasilishaji wa kesi mtandaoni, kupanua miundombinu ya mahakama na kupunguza mrundikano wa kesi kwa asilimia 25.
“Matokeo haya hapo juu yamepatikana katika kipindi cha miaka minne ya Jaji Mkuu Martha Koome. Hakika, Bibi Jaji Martha Koome ana rekodi ya kuwa na ufanisi, umakini, uwajibikaji, na anaweza kufikiwa,” walisema katika taarifa hiyo.
Viongozi hao wanawake walitoa kauli hiyo wakati Mahakama ikifanya mazungumzo katika vituo vya mahakama kote nchini na wadau mbalimbali kuhusu namna inavyoweza kutumikia mwananchi vyema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply