Kalonzo aunga wito kubuniwe tume kuchunguza utekaji nyara, mauaji – Taifa Leo


KIONGOZI wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Bw Eugene Wamalwa, wamejiunga na wito wa kuundwa kwa tume kuchunguza wimbi la utekaji nyara nchini, huku serikali ya kaunti ikikosolewa kwa namna inavyoshughulikia miili isiyojulikana na jukumu lake katika kufanya familia za watu waliopotea kuwapata wapendwa wao.

Viongozi hao walisema ni lazima tume hiyo ijumuishe wadau kutoka sekta mbali mbali ikiwemo upinzani na mashirika ya kijamii na akatishia kuwa wataunda tume hiyo iwapo serikali itakosa kufanya hivyo.

“Lazima upinzani ushirikishwe. Mauaji haya hayawezi kupuuzwa tu,” alisema Bw Kalonzo.

Kalonzo alifichua kuwa wahudumu wa mochari walidai kutojua chochote kuhusu dai la kupotea kwa miili mingine miwili, akieleza wasiwasi wake kwamba huenda ni ya vijana wawili ambao bado hawajulikani walipo.

“Tunaamini kuwa mili hiyo miwili au mitatu, ni miongoni mwa vijana wetu ambao tunatafuta. Matukio haya ya utekaji nyara na mauaji tunajua yanafadhiliwa na serikali,” aliongeza.

Kwa upande wake, Bw Wamalwa alimkosoa Rais William Ruto kwa kupeleka maafisa wa polisi kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya magenge na watekaji nyara umbali wa kilomita 12,000 kule Haiti, ilhali watoto wa Kenya wanaendelea kuuawa nchini.

Bw Wamalwa alisema kuwa watafanya uchunguzi kutengua kitendawili cha Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kushirikiana na maafisa wa polisi kuficha miili hiyo. Hii ni baada ya madai kuibuka kwamba wafanyakazi wa mochari hiyo waliondolewa.

“Tunafahamu kuwa baadhi ya wafanyakazi wamehamishwa, tutafanya uchunguzi wetu wenyewe. Iwapo anahusika atafika mbele ya Mahakama,” alisema Wamalwa.

Afisa Mkuu wa Afya wa Kaunti ya Nairobi, Bw Tom Nyakaba, alikanusha madai kwamba hifadhi hiyo inahusika kuficha miili. Alifafanua kuwa jukumu la kaunti ni kuhifadhi miili kutoka kwa polisi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*