MSEMO kwamba usione simba amenyeshewa ukadhani ni paka ulipata maana baada ya wenyeji Nottingham Forest kuandikisha ushindi wao mkubwa kabisa katika historia ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), walipobomoa Brighton 7-0 ugani City Ground, Jumamosi.
Vijana wa kocha Nuno Espirito Santo waliingia mchuano huo wa raundi ya 24 wakiuguza kipigo kikali cha 5-0 kutoka kwa Bournemouth hapo Januari 25.
Forest almaarufu Tricky Trees, ambao pia hawakuwa wamepata ushindi dhidi ya Brighton ligini mara tatu mfululizo ikiwemo kulemewa 3-2 msimu 2023-2024 ugani City Ground, walipata mabao yao kupitia kwa Chris Wood (matatu), Morgan Gibbs-White, Neco Williams na Jota Silva na Lewis Dunk aliyefunga.
Beki wa Brighton, Dunk alianzisha mvua hiyo ya magoli kwa kujifunga akiondosha krosi kutoka kwa Gibbs-White dakika ya 12. Gibbs-White aliongeza bao la pili 2-0 dakika ya 25 kupitia kichwa baada ya Anthony Elanga kuchanja kona safi. Wood alifanya magoli kuwa 3-0 dakika ya 32 kupitia kichwa chake baada ya kukutana vyema na krosi ya Elanga.
Brighton walifanya badiliko mapema katika kipindi cha pili wakijaza nafasi ya Kaoru Mitoma kwa kuingiza Simon Adingra kuokoa jahazi. Hata hivyo, wembe ulikuwa ule ule, Wood akitetemesha nyavu kutokana na pasi nyingine murwa kutoka kwa Elanga dakika ya 64.
Wood aliandikisha historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa Forest kupata hattrick tangu Nigel Clough mwaka 1987, alipoona lango dakika ya 69 kupitia penalti baada ya Tariq Lamptey kuangusha Gibbs-White ndani ya kisanduku. Williams na Silva walifungia Forest mabao mawili ya mwisho dakika za lala-salama.
Forest wanasalia salama ndani ya nne-bora katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 47 kutokana na michuano 24. Brighton wanasalia nambari tisa kwa alama 34.
Leave a Reply