Dalili za kampeni kura 2027 kuanza – Taifa Leo


HAFLA na matamshi ya viongozi wa kisiasa kote nchini zaashiria kwamba kampeni za uchaguzi mkuu wa 2027 zimeanza.

Japo uchaguzi mkuu utafanyika miaka mitatu ijayo, kuanzia kuungana kwa vyama vya kisiasa au kutangaza mipango ya kuungana hadi ziara zinazosemekana kuwa za kuzindua miradi ya maendeleo, kauli za viongozi zinaonyesha kuwa wanajipigia debe kwa uchaguzi mkuu wa 2027.

Huku wale wa upinzani wakieleza wazi kuwa lengo lao ni kuweka mikakati ya kung’oa serikali ya Kenya Kwanza mamlakani, wale wanaogemea upande wa serikali wanasingizia kuwa wanazindua au kukagua miradi ya maendeleo ili kujipigia debe.

Rais William Ruto, Naibu wake Kithure Kindiki na wanasiasa wanaoegemea serikali hawaepuki siasa katika ziara zao. Katika ziara ya siku tano ya Rais Ruto eneo la Magharibi, siasa za uchaguzi mkuu wa 2027 zilitawala huku akiwataka wapinzani wake kujiandaa kushindwa katika uchaguzi huo.

Wadadisi wa siasa wanasema serikali inarushia maeneo minofu kwa njia ya maendeleo kama chambo cha kuvutia wapiga kura.

“Hata ile bonasi ya wakulima wa miwa ni sehemu ya kampeni. Kumbuka ilijiri baada ya Rais Ruto na Mkuu wa Mawaziri kuunganisha vyama vyao. Ulimuona rais akikata miwa na huo ni mkakati wa kujipendekeza kwa mwananchi wa kawaida,” asema Francis Wekesa, mchanganuzi wa siasa.

Rais amekuwa akizindua miradi mashinani ambayo kwa kawaida inapaswa kuongozwa na maafisa wa serikali wa ngazi za chini.

Katika hafla ambazo wadadisi wanasema ni za kupenya mashinani baada ya kupoteza eneo la Mlima Kenya kufuatia kuondolewa serikalini kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, washirika wa rais hukemea wanaodai ataongoza kwa muhula mmoja.

Baadhi ya washirika wake akiwemo mwandani wake Oscar Sudi, ambaye ni mbunge wa Kapsaret, wamekuwa wakizungumzia wazi uchaguzi wa 2027 na kuapa watafanya kila wawezalo Rais ashinde muhula wa pili.

Washirika wake kutoka chama cha ODM waliojiunga na serikali wamekuwa wakitangaza hadharani kwamba, watamuunga mkono kwa muhula wa pili 2027, ingawa mawaziri hawafai kujihusisha na siasa.

Katika siku za hivi majuzi, Naibu Rais Kithure Kindiki amekuwa akikutana na jumbe kutoka maeneo tofauti kupigia debe serikali huku akikosoa wanaodai Ruto atakuwa rais wa muhula mmoja.

Jana, Profesa Kindiki na kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichungwah walisisitiza kuwa wakati wa kampeni haujafika huku matamshi yao yakiashiria kuwa wanapigia debe kiongozi wa nchi kwa muhula wa pili.

Profesa Kindiki aliongoza maafisa wa serikali katika hafla ya kuchangia wanabodaboda katika kaunti ya Embu ambako alitangaza kuwa Rais atazuru eneo hilo.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na Bw Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka wametangaza kuwa wataungana wakilenga kushinda Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Wakizungumza walipoungana katika uzinduzi wa makao makuu mapya ya chama cha DAP- K, kinachoongozwa na Eugene Wamalwa, viongozi hao walisema watahakikisha Ruto atakuwa rais wa muhula mmoja.

Bw Gachagua alizika tofauti zake na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua ambapo walitangaza kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, kila upande unajitahidi kuonyesha ubabe kuelekea 2027 hasa baada ya Bw Gachagua kuondolewa.

“Kila hatua iwe mradi au hafla ya kisiasa Kenya huwa inalenga kampeni za uchaguzi mkuu ujao. Kwa sasa kampeni imepamba moto kufuatia tofauti za Rais Ruto na Bw Gachagua,” akasema.

Kulingana naye, muungano wa chama tawala cha UDA na ANC cha Musalia Mudavadi na Gachagua na Karua kuzika tofauti zao ni baadhi dalili za kampeni za mapema za uchaguzi mkuu wa 2027.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*