HAFLA ambayo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Kiongozi wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua walitangaza kuzika tofauti zao ni sehemu ya mpango mpana wa kuleta upinzani pamoja kuelekea 2027.
Ni mpango unaosukwa kwa umakinifu na wanamikakati wa kisiasa nyuma ya pazia wanaoungwa mkono na wadau wanaohisi utawala wa Kenya Kwanza haufai kuruhusiwa kuhudumu kwa muhula wa pili, duru za ndani na wadadisi wanasema.
Wanasema kwamba kabla ya wawili hao kukutana hadharani, kulikuwa na mazungumzo ya kina yaliyofanikishwa na watu mashuhuri kutoka ndani na nje ya Mlima Kenya.
Jamvi la Siasa imebaini kuwa mazungumzo hayo yalianza baada ya Gachagua kutimuliwa serikalini na umaarufu wake kuongezeka katika eneo la Mlima Kenya.
Duru hizo zinasema kwamba mazungumzo hayo yaliibuka wakati mmoja na yaliyofanikisha jamii ya Wakamba kujumuishwa katika muungano wa Gema unaoleta pamoja jamii za eneo la Mlima Kenya.
“Ilikuwa muhimu kuonekana kuwa Gachagua anaunganisha ngome yake kwanza na mengi zaidi yanajiri,” alisema mwandani mmoja wa Bw Gachagua ambaye alihudhuria hafla ya Jumamosi wiki jana nyumbani kwa Karua kaunti ya Kirinyaga.
Viongozi wa Gema na wa kidini walitekeleza jukumu muhimu la kujumuisha jamii ya Wakamba katika Gema, muungano ambao kwa miaka mingi umehusisha Gikuyu, Meru na Embu.
“Japo uamuzi wa kuzika tofauti zao za kisiasa ulikuwa wao wenyewe, kulikuwa na mazungumzo mapana yaliyofanikishwa na watu mashuhuri ambao wanataka kuona eneo hilo limeungana kisiasa kabla ya kuungana na maeneo mengine,” alisema mwanasiasa mmoja anayefahamu muundo wa mkakati wa upinzani.
Alisema kila kiongozi anayeingizwa kwenye mpango huo anaruhusiwa kudumisha chama chake cha kisiasa.Mwanasiasa mwingine alisema kwamba wanamikakati waliotwikwa jukumu hilo na wanaofanya kazi kwa usiri mkubwa wamefikia aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i miongoni mwa viongozi wengine wakuu wasiofurahishwa na utawala wa sasa.
“Litakapoiva, litakuwa vuguvugu kubwa la kitaifa,” alisema na kukumbusha Taifa Jumapili kauli ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka hawawezi kuanika mikakati yao yote mapema.
Mapema wiki hii, Bw Gachagua aliungana na Bw Musyoka na viongozi wengine katika hafla ya kuzindua ofisi mpya za chama cha DAP- Kenya cha aliyekuwa waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa.
Viongozi hao walisema wataungana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 huku Gachagua akirai wenzake kutozingatia nyadhifa bali wawe na nia ya kubandua Rais Ruto mamlakani kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Katika hafla iliyofanyika nyumbani kwa Karua, Gichungu, kaunti ya Kirinyaga, kiongozi huyo wa Narc- Kenya alisisitiza hilo akisema sio lazima awe katika chama kimoja na Bw Gachagua kufanikisha ajenda yao.
Bw Gachagua anatarajiwa kutangaza chama chake cha kisiasa wakati wowote wiki ijayo.’
“Martha tunajivunia wewe na nataka niseme kutoka ndani ya moyo wangu hata tulipokuwa tunashindana, bado nilikuwa naupenda sana uongozi wako na kutamani ungekuwa kwenye timu yetu, sasa tupo pamoja tu tutaunda timu kubwa na Wakenya wengine,” alisema Gachagua.
Karua aliongeza: “Watu wakiazimia kudhulumu kundi la watu, watu wanaoazimia kuleta ukombozi ni lazima wajipange upya. Ndio maana Wakenya wote wenye nia njema lazima tushikane mikono. Ni lazima tuungane.”
Akizungumza katika hafla ya kuzindua ofisi za DAP- Kenya mapema wiki hii, Gachagua na Kalonzo walifichua mpango mpana wakisema utazoa hata eneo la Magharibi ambalo Rais Ruto aligeukia baada ya kupoteza umaarufu wake Mlima Kenya.Alisema watu kutoka Mlima Kenya wamechukua mwelekeo tofauti wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, akiwataka viongozi wa upinzani kusalia na umoja.
“Tunachotaka ni umoja wa watu wetu,” alisema na kuashiria kuwa mpango wao unalenga kumfanya Rais Ruto azipenye ngome za kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye alisaidia Kenya Kwanza kumng’oa kama naibu rais.
“Vuguvugu lijalo litakuwa na nguvu. Litazuia Ruto magharibi, mashariki na pwani. Sehemu ya Kisii Nyanza imeenda na Ukambani imemponyoka Raila. Kuna wimbi la Tawe kule magharibi na mazungumzo yanaendelea kabla ya sura halisi ya muungano wa upinzani kujitokeza,” akasema mmoja wa wanamikakati ambaye aliomba asitajwe jina kwa sababu ya jukumu lake katika shughuli hiyo.
Leave a Reply