SADC sasa yakubali kukutana na marais wa EAC kujadili vita nchini DRC – Taifa Leo


VIONGOZI wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamekubaliana kukutana na wenzao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujaribu kumaliza mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo waasi wanadhibiti eneo kubwa.

Viongozi wa SADC, ambao walifanya mkutano wa dharura jijini Harare, Zimbabwe, mnamo Ijumaa walielezea wasiwasi wao kuhusu kudorora kwa hali ya usalama nchini DRC baada ya waasi wa M23 kushambulia walinda amani kutoka jumuiya ya kanda na kuuteka mji wa Goma wiki iliyopita.

Taarifa ya viongozi hao ilitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na mazungumzo kufanywa ili kumaliza mzozo huo ambao umesababisha mamilioni ya watu kuhama makwao.

“Kikao hicho kilitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa pamoja wa SADC na EAC ili kujadiliana kuhusu hali ya usalama nchini DRC,” ilisema taarifa hiyo.

Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, ambaye Jumatano alisusia mkutano wa marais wa EAC kujadili vita hivyo nchini mwake, alihudhuria mkutano wa Harare.

Rais Felix Tshisekedi wa DRC mnamo Desemba 2024. PICHA | REUTERS

Mnamo Januari 22, waasi hao walishambulia kikosi cha nchi za Afrika Kusini na SADC kinacholinda amani DRC na kuua wanajeshi 13 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa. Wanajeshi watatu wa Malawi pia waliuawa katika shambulizi hilo.

Mkutano wa Harare, ulioongozwa na mwenyeji Rais Emmerson Mnangagwa “ulilaani vikali” mashambulizi hayo. Aidha, viongozi hao walikiri kwamba kikosi cha kulinda amani cha SADC kilichorithi kile cha EAC miaka miwili iliyopita, kimeshindwa kufikia malengo yake. Kikosi cha SADC kinajumuisha wanajeshi wa Malawi, Afrika Kusini, Tanzania na wenyeji DRC.

Rais Tshisekedi anashutumu Rwanda – nchi mwanachama wa EAC – kwa kuwapa waasi wa M23 silaha na kutuma vikosi vyake kupigana pamoja na waasi hao ndani ya DRC.

Chimbuko la M23

Kundi la M23 lilianzishwa mwaka 2012 kutoka kundi jingine la waasi, na malengo yake ni kupinga dhuluma dhidi ya watu wa kabila la Tutsi mashariki mwa DRC, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi.

Rwanda – ambayo pia imeshutumu DRC kwa kuhusiana na makundi kadha ya waasi na wahusika wa mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994, ambao kisha walikimbilia DRC – imekana vikali madai kwamba inawapa silaha waasi.

Katika mkutano uliofanyika nchini Zimbabwe mnamo Desemba mwaka jana, viongozi wa SADC walikubali kuongeza muda wa kikosi cha kudumisha amani DRC kwa mwaka mwingine. Kikosi hicho cha kanda kinajumuisha wanajeshi wa Malawi, Afrika Kusini, Tanzania na wenyeji DRC.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*