ALEXANDER Mutiso aliendelea vyema na matayarisho ya kutetea taji lake la London Marathon baada ya kuibuka bingwa wa Kagawa Marugume Half Marathon nchini Japan, Jumapili.
Naye Dolphine Omare Nyaboke alihifadhi umalkia wake kwenye mashindano hayo ya kilomita 21.
Mutiso, ambaye alitawala makala ya 2023 ya Kagawa Marugume Half kwa rekodi ya dakika 59 na sekunde 17, alinyakua taji la pili kwa rekodi mpya ya 59:16.
Bingwa huyo wa London Marathon 2024, ambaye amethibitisha kutetea taji hilo nchini Uingereza mwezi Aprili, alifuatwa kwa karibu na Mkenya mwenzake Emmanuel Maru (59:19) na Mjapani Tomoki Ota (59:27).
Wakenya wengine katika mduara wa 20-bora kitengo cha wanaume ni James Mutuku (saa 1:00:30), Ledama Kisaisa (1:00:36) na Bedan Karoki (1:00:40) waliokamata nambari nane, 13 na 14 mtawalia.
Nyaboke alishinda taji la kinadada kwa mwaka wa pili mfululizo akiimarisha rekodi yake ya Kagawa Marugume Half kutoka 1:06:07 hadi 1:06:05. Alimaliza mbele ya Muingereza Calli Hauger (1:06:58), Isobet Batt-Doyle wa Australia (1:07:17) na Mkenya mwenzake Pauline Kamulu (1:07:33) mtawalia.
Naye Vincent Kipchumba aliibuka mshindi wa Beppu-Oita Mainichi Marathon mjini Oita, Japan. Kipchumba alitwaa ubingwa kwa saa 2:06:01, mbele ya Wajapani Hiroki Wakabayashi (2:06:12) na Shohei Otsuka (2:06:38).
“Nafurahia kufuta rekodi ya Beppu-Oita Mainichi Marathon,” akasema Kipchumba ambaye mara ya mwisho alikuwa amemaliza mbio za kilomita 42 ni wakati wa London Marathon mwaka 2021 alipotimka muda wake bora wa 2:04:28.
Mnamo Jumamosi, Alex Matata ameibuka mshindi wa mbio za kilomita 21 za Ras Al Khaimah baada ya kukata utepe kwa dakika 59 na sekunde 20 katika Milki za Kiarabu (UAE).
Bingwa huyo wa Antrim Coast na Bucharest Half Marathon 2024 alikimbia vizuri kabla kuchukua uongozi hatua za mwisho mwisho na kutwaa taji, akiimarisha muda wake bora kwa sekunde 17 kutoka 59:37 hadi 59:20.
Alimaliza sekunde tano mbele ya Muethiopia Gemechu Dida (59:25) naye Isaia Lasoi akafunga tatu-bora kwa 59:26. Mkenya mwingine ndani ya 10-bora katika kitengo cha wanaume ni Hillary Kipkoech katika nafasi ya saba kwa 59:53.
Wakenya wanne – Judy Kemboi (saa 1:06:34), Jesca Chelangat (1:06:53), Veronica Loleo (1:08:06) na Brillian Jepkorir (1:08:48) – walikamilisha ndani ya 10-bora katika kitengo cha wanawake katika nafasi ya pili, tatu, saba na tisa, mtawalia.
Ejgayehu Taye, aliyekuwa ametangaza atavizia rekodi ya dunia ya Muethiopia mwenzake Letesenbet Gidey (1:02:52), alitwaa taji kwa 1:05:52.
Wakimbiaji 10 wa kwanza kwenye Ras Al Khaimah Half walituzwa Sh2.5 milioni, Sh1.2m, Sh775,200, Sh646,000, Sh516,800, Sh452,200, Sh387,600, Sh323,000, Sh258,400 na Sh129,200, mtawalia.
Kibet apigwa breki 800m ya Miramas Metropole
Kwingineko, mshindi wa zamani wa nishani ya shaba wa Riadha za Dunia za Ukumbini mbio za mita 800, Noah Kibet aliridhika na nafasi ya tatu katika shindano la Meeting Miramas Metropole nchini Ufaransa, Ijumaa.
Kibet aliyepigiwa upatu kutawala mbio hizo za 800m, aliandikisha dakika 1:46.05, nyuma ya Mmoroko Abdelati El Guesse (1:45.57) na Mfaransa Yanis Meziane (1:45.87). Mshindi alipokea Sh160,620 nao nambari mbili na tatu wakaridhika na Sh133,850 na Sh107,080, mtawalia.
Leave a Reply