MIPANGO inayoendelea ya kufufua kiwanda cha kutengeneza sukari cha Mumias inatishiwa na uhasama wa ndugu wawili wanaozozana kudhibiti sekta ya utengenezaji kemikali ya ethanol.
Ndugu hao ni Jaswant Singh Rai anayeendesha na kusimamia kiwanda cha sukari cha West Kenya, na mdogo wake Sarbjit Singh Rai anayesimamia kile cha Mumias.
Wawili hao wana uhasama wa ndani kila mmoja akilenga kudhibiti sekta ya sukari na kilimo cha miwa eneo la magharibi mwa nchi.
Uhasama na ubabe wa kudhibiti uzalishaji wa ethanol kati ya Jaswant na Sarbjit Rai unajiri siku chache baada ya Rais William Ruto kutoa bonasi ya Sh150 milioni kwa wakulima waliowasilisha miwa yao katika kiwanda cha Mumias. Wakulima watakaonufaika ni wale waliopeleka zao lao kiwandani humo kati ya Januari na Desemba 2024.
Rais Ruto pia aliagiza wizara za kilimo, fedha na kawi kuhakikisha kuwa Mumias sasa itazalisha kemikali yake ya ethanol.
“Tunataka kutumia rasilimali ya molasses kutoka kiwanda hiki kuanza kutengeneza ethanol,” akasema Rais huku akisisitiza mpango huo uharakishwe mara moja.
Siku tatu baada ya ziara ya Rais, kiwanda cha West Kenya kilitangaza kuwa kitafufua mpango wa kutengeneza ethanol kwa kutumia mashine yake iliyoko kiwanda cha Mumias kama njia ya kutii amri ya rais.
Viongozi wa kisiasa wameingilia suala hilo wakisema hawatakubali West Kenya iingilie utendakazi wa Mumias na kuzalisha ethanol katika kiwanda hicho.
Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya na madiwani wote wa Bunge la Kaunti ya Kakamega wamepinga mpango huo wa West Kenya.
“Ili Mumias isalie imara kundi la Rai linastahili kukoma kuingilia utendakazi wake. Mpango wa kuruhusu West Kenya izalishe ethanol kwa kutumia mashine zake ndani ya kiwanda Mumias, utalemaza shughuli ya kufufua kiwanda chenyewe (Mumias),” alisema Gavana Barasa.
Bw Salasya alisema kuwa hatakubali West Kenya idakie baadhi ya miradi ya Mumias, akisema hatua hiyo itahujumu mwekezaji wa sasa ambaye amefanya juhudi kubwa kufufua kampuni hiyo kuu ya sukari nchini tangu 2018.
“Nakataa adui (West Kenya) kuendesha shughuli Mumias. Iwapo hawataki Mumias itumie mashine zao kuzalisha ethanol basi wazichukue au waziharibu,” alihoji Bw Salasya.
Akaongeza: “Sitanyamaza. Ninahimiza wananchi wajitokeze kupinga udikteta huu wa umiliki wa West Kenya.”
Mnamo Jumamosi, madiwani kutoka Matungu, Mumias Magharibi na Mumias Mashariki wakiwa pamoja na baadhi ya wakulima wa miwa waliandamana hadi kiwanda cha Mumias.
Walipofika hapo walifurusha walinzi ambao walikuwa wametumwa na West Kenya kulinda mashine zake mbili za kuzalisha ethanol.
Wandamanaji hao walisitisha shughuli kwenye barabara ya Bungoma-Mumias huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kukemea na kuonya wamiliki wa West Kenya kuhusu mipango yake.
Leave a Reply